2016-01-16 14:27:00

Iweni ni vyombo vya huruma na mapendo ya Mungu kwa watu wake!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari, hivi karibuni amewapongeza Wamissionari wa Consolata kwa kupata Shemasi mpya Dunstan Balayangaki Mushobolozi aliyepata Daraja la Ushemasi mikononi mwa Askofu mkuu Rugambwa. Kanisa linamshukuru Mungu kwa kupata Mashemasi wapya kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao kwa sasa wanajiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu la Upadre.

Mashemasi wapya ni baraka na neema ya Mungu wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mashemasi wanapaswa kuwa ni vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo aliyekuja duniani kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Mama Kanisa anaendelea kusali, ili Mwenyezi Mungu aweze kulijalia Kanisa lake wataumishi hodari na watakatifu, watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Protase Rugambwa anawataka Mashemasi wapya wajitahidi kumtumikia Mungu katika ukamilifu wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Wakleri wakishaonja huruma ya Mungu na kuimarishwa katika maisha na utume wao; wawe tayari kuwahurumua Watu wa Mungu kwa kuwagawia Mafumbo ya Kanisa, hususan, Sakramenti ya Upatanisho, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kuwashirikisha wengine huruma hii inayobubujika kutoka kwa Kristo, Sura ya Baba mwenye huruma

Askofu mkuu Protase Rugambwa amewapongeza kwa namna ya pekee Wamissionari wa Shirika la Consolata kwa bidi, juhudi, ari na moyo mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu sehemu mbali mbali za dunia. Wanashirika wapya wa Consolata waendelee kuiga mfano bora kutoka kwa wanashirika wenzao, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha hadi miisho ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.