2016-01-16 12:05:00

Askofu Titus Mdoe awaambia Mashemasi wapya: Useja ni zawadi yenye changamoto!


Mashemasi wanapewa Sakramenti ya Daraja kwa ajili ya utume mahususi ndani ya Kanisa. Wanaitwa kumwakilisha Kristo Yesu, Mtumishi kwa Jumuiya nzima ya waamini, haswa kwa kuhubiri Injili, kuwasaidia Mapadre na Maaskofu katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa pamoja na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Daraja Takatifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linapewa umuhimu wa pekee kwani Wakleri wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa kweli ni mashuhuda na “majembe” ya huruma ya Mungu inayogusa, inayoponya na kutakatifuza watu katika hija ya maisha yao ya kiroho. Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, kabla ya kuondoka kuelekea Mtwara, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, aliwapatia Mafrateri watatu, Daraja la Ushemasi kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Hawa ni Shemasi William Sindano, Shemasi James Ngonyani pamoja na ShemasiFrancisco Josè Giron Anguiozar wa Jumuiya ya Ukatekumeni mpya. Askofu Mdoe katika mkesha wa Siku kuu ya Tokeo la Bwana aliwakumbusha Mashemasi hawa umuhimu wa zawadi ya useja katika maisha na utume wa Kanisa. Hakuna mtu anayelazimishwa kuwa mseja, bali hii ni zawadi ambayo Wakleri wanaipokea kwa imani na matumaini, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila kufungwa na makandokando mengine ya kifamilia. Kanisa linaikumbatia zawadi hii, lakini pia linatambua changamoto zinazowakabili Wakleri ndani ya Kanisa.

Katika Ibada ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana iliyohudhuriwa pia na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania pamoja na Askofu msaidizi Euzebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa niaba ya Kardinali Pengo, Askofu msaidizi Nzigilwa alimshukuru Askofu Titus Josph Mdoe kwa utume na huduma makini alizitoa kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam tangu alipowekwa wakfu hapo Mei Mosi, 2013. Amekuwa kweli ni shuhuda na chombo cha faraja kwa Watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam na chachu ya utendaji wa shughuli za kichungaji kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu pasi na makuu.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Titus Joseph Mdoe anasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara, Jumapili tarehe 17 Januari 2016. Ibada hii inahudhuriwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ujumbe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ukiwa umeongozana na Askofu Titus Mdoe, umeondoka Parokia ya Kibiti, Jimbo kuu la Dar es Salaam, tayari kushiriki katika Ibada ya Masifu ya Jioni na kushuhudia Askofu Titus Mdoe akikabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Mtwara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.