2016-01-15 10:56:00

Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kuungana na Marabbi wa dini ya Kiyahudi nchini Italia katika ujumbe wao kwa maadhimisho ya Siku ya ishirini ya majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi, wanasisitiza umuhimu kwa waamini wa dini hizi mbili pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa kutambua umuhimu na hekima inayofumbatwa katika majadiliano haya.

Huu ni mchakato wa majadiliano ya kidini ulioanzishwa takribani miaka ishirini iliyopita nchini Italia, ili kuwasaidia waamini wa dini hizi mbili kufahamiana, kuheshimiana na kusaidiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi za kiimani. Kila mwaka, ifikapo tarehe 17 Januari, Baraza la maaskofu Katoliki Italia pamoja na Marabbi wa dini ya Kiyahudi nchini Italia wanaungana kwa pamoja, ili kufanya majadiliano ya kidini, kama sehemu ya makesha ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo Duniani, linaloanza hapo tarehe 18 Januari na kuhitishwa wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, mwalimu na mtume wa mataifa.

Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa mwaka huu, Siku hii itakua na baraka ya pekee, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye anatarajiwa kutembelea kwa mara ya kwanza Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Maadhimisho ya mwaka huu kwa namna ya pekee, yanajikita katika Amri ya kumi ya Mungu, usitamani mali ya jirani yako. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasafisha dhamiri zao, ili ziweze kuendana na mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu.

Viongozi hawa wa kidini katika ujumbe wao, wanalaani na kukemea vitendo vya mauaji, nyanyaso na dhuluma zinazofanywa kwa misingi ya udini, kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vitendo hivi ni kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu na kwamba, si halali kabisa kutumia jina la Mungu kufanya mauaji, kwani Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya wema, uzuri na utakatifu wa maisha. Vitendo hivi ni kielelezo cha kukengeuka kwa binadamu na kuacha maisha adili na kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanpyaisha maisha yako kwa kujikita katika uaminifu katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya kila siku; kwa kuendeleza majadiliano yanayojikita  katika ukweli na uwazi; haki na amani; kwa kukazia na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; ili kwa pamoja, waamini wa dini hizi mbili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Imani, amani na matumaini ni fadhila ambazo zinapata chanzo na utumilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini binadamu amedhaminishwa, ili kuzifanyia kazi katika maisha yake, ili kuchangua na kuambata mapenzi ya Mungu, kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi.

Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, waamini wa dini hizi mbili wamejadili kwa kina na mapana kuhusu Amri za Mungu katika maisha yao na kwa mwaka 2016 wanahitimisha tafakari hii sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu majadiliano ya kidini, Nostra aetate.

Viongozi hawa wanatambua kwamba, kila hatua imekuwa ni sehemu ya mchakato wa kugundua mafanikio, magumu na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa imani na matumaini. Lakini hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya waamini wa dini hizi mbili, ili kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu.

Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Hivi ndivyo viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Wakuu wa Dini ya Kiyahudi nchini Italia wanavyohitimisha ujumbe wao kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya ishirini ya Majadiliano ya kidini kati ya dini hizi mbili.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.