2016-01-15 09:53:00

Maaskofu Katoliki Kenya wanahimiza Umoja wa Wakristo!


Maadhimisho ya Juma la kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu”. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika maadhimisho haya yanayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari, Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, mwalimu na mtume wa mataifa, wanaialika Familia ya Mungu nchini Kenya kusimama kidete katika kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo.

Askofu Alfred Rotich, Mwenyekiti wa Tume ya Majadiliano ya Kiekumene, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake kwa Familia ya Mungu nchini humo anaialika kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanasali na kutafakari kwa pamoja na Wakristo wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Kenya, tayari kuendeleza mchakato wa hija ya pamoja inayojikita katika sala, upendo na mshikamano wa dhati; ili kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu Rotich anaendelea kusema Familia ni chombo, shuhuda wa upendo, huruma na matendo ya Mungu kwa waja wake. Baraza ka Maaskofu Katoliki Kenya linawahamasisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, vitini vya sala na tafakari za kuombea Umoja wa Wakristo vinawafikia walengwa kwa lugha wanayoifahamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakaza kusema, linashirikiana kwa karibu zaidi na Wakristo wa Makanisa na madhehebu mbali mbali katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Kenya.

Ushirikiano huu unajionesha hata katika masuala ya ushauri wa maisha ya kiroho kwa wanafunzi wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu nchini Kenya. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwamba, uhusiano na ushirikiano huu utaweza kupanuliwa zaidi ili kuwafikia wagonjwa na wafungwa, changamoto kubwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kuwataka waamini kujikita katika kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Baraza la Maaskofu Katoliki linawaalika Wakristo wote nchini Kenya, kushikamana kwa dhati katika kuwasaidia na kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi, huduma inayotolewa chini ya usimamizi wa Baraza la Makanisa nchini Kenya. Maadhimisho ya Njia ya Msalaba ya Kiekumene inayofanywa katika baadhi ya miji nchini Kenya wakati wa Ijumaa kuu ni kielelezo cha sala na tafakari ya pamoja kati ya Wakristo.

Maaskofu Kenya wanasema, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika majadiliano ya kiekumene nchini humo, lakini bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo. Waamini wanapaswa kufahamu mambo msingi ambayo Kanisa linayapatia kipaumbele katika majadiliano ya kiekumene na katika maisha na utume wake. Bado hakuna majadiliano ya kitaalimungu na Makanisa pamoja na madhehebu ya Kikristo nchini Kenya. Bado kuna ugumu wa kujadili kwa pamoja masuala kama useja, ushoga, wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavialika vyombo vya mawasiliano ya kijamii kuhakikisha kwamba, vinasaidia kuhamasisha umoja na mshikamano wa Kikristo. Mwishoni, Maaskofu wanasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya, Novemba 2015 ilikuwa ni fursa ya pekee kwa Makanisa kushikamana ili kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazomwilishwa katika uhalisia na vipaumbele vya wananchi wa Kenya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.