2016-01-14 11:20:00

Tanzania na Rwanda kuendelea kudumisha mahusiano na urafiki uliopo!


Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watanzania kujikita katika kuimarisha miundombinu ili kukuza uchumi, kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa shughuli mbalimbali mfano kilimo na biashara. Akizungumza na wadau wakati akifungua mkutano wa Miradi ya Ubia katika Ujenzi wa Miundombinu kati ya Tanzania na Japan (TANZANIA -JAPAN PUBLIC -PRIVATE QUALITY INFRASTRURE CONFERENCE) uliofanyika Alhamisi, tarehe 14 Januari 2016, katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam, amesema sekta binafsi inasaidia katika ujenzi wa miundombinu na sekta ya usafirishaji kwa ujumla, ambapo ni muhimu kwa vile inasaidia kuboresha maisha ya watanzania.

“Serikali kupitia Kituo cha uwekezaji nchini (TIC) imeandaa mazingira mazuri ya biashara inayosaidia wawekezaji kuja kuwekeza nchi, matumaini yetu ni kwamba kutokana na mkutano huu   wawekezaji wa ndani  mtapata  fursa ya kujifunza na kujiunga katika   kampuni ambazo zitawasaidia  kushirikiana na kampuni za kijapani  na kuweza kupata ujuzi,  utaalamu wa kiutawala na uwezo wa  kuwa wabunifu zaidi hasa katika masuala ya miundombinu.”  amesema Waziri Mkuu. Ameendelea kwa kusema mkutano huu utaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japani, na kutoa fursa ya kubadilishana ujuzi kwa wakandarasi, washauri, kampuni za biashara na uhandisi kutoka Japani na Tanzania, vilevile utawawezesha kujenga mtandao kwa kushirikiana na makampuni ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wa miundombinu na usafirishaji, Tanzania ina ukubwa wa barabara zinazofikia kilomita 87,581, kutokana na sera na jitihada mbalimbali kwa kipindi cha miaka 10 (2005-2015) jumla ya kilomita 17,762 zimefikia hatua mbalimbali za ujenzi. Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema, Tanzania ina mifumo miwili ya reli, reli ya kati yenye kilomita 2,706 na reli ya ‘Tanzania Zambia Railway Authority’ (TAZARA) yenye kilomita 975. Pia, ina Bandari kuu za Dar es salaam, Tanga na Mtwara .

Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa (National ICT Broadband Backbone -NICTBB) kwa kutumia mfumo wa baharini (SEACOM, July 2009) na (EASSY April,2010) tayari nchi jirani za Rwanda, Zambia na Kenya zimeunganishwa na mkongo huo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani, amesema miundombinu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yeyote ile duniani. Tanzania na Japani zimeshirikiana katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, mfano barabara za Dodoma –Iringa, Namtumbo –Tunduru, Dodoma – Babati inayoendelea kujengwa, upanuzi wa barabara ya Gerezani pamoja na ‘fly over’ ya TAZARA.

Naye, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Takatoshi Nishiwake amesema, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipotembelelea Japani alisema angependa kuona Japani na Tanzania zinashirikiana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu. Ameendelea kwa kusema kuwa, Serikali ya Japani inapenda kubadilishana ujuzi na Tanzania katika masuala ya miundombinu, pia ni matumaini yake kuwa washiriki kutoka pande zote mbili wanapata fursa ya kubadilishana ujuzi na kujifunza zaidi. Vile vile kupitia mkutano huu mahusiano ya nchi hizi mbili yataimarika zaidi.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini, Eugene Kayihura. Ambapo amemuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Rwanda. Akizungumza na Balozi Kayihura Jumatano 13, 2016 ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo kwa kumtembelea na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano ulipo baina ya nchi hizi mbili. “Nia yetu ni kushirikiana kwa pamoja kwa kuunganisha wafanyabiashara wetu, kwa kutumia Bandari ya Dar es salaam na reli ya kati, ambayo tutajenga kwa kiwango cha kisasa ‘standard gauge’ ili ziweze kubeba mizigo mingi na kwenda mwendo wa kasi” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda, Kayihura amesema Tanzania na Rwanda ni nchi marafiki na zinafanyakazi wa pamoja, Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania kikanda na kimataifa. “Tunatumia Bandari ya Dar es salaam na Mombasa, tunashukuru kwa namna ambavyo mnaboresha Bandari ya Dar es Salaam, kwani Rwanda inafaidika pia kwa vile mizigo yetu mingi karibu asilimia 75 husafirishwa kupitia bandari hii” alisema Balozi Kayihura.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.