2016-01-14 14:28:00

Ambateni na kushuhudia huruma ya Mungu!


Huruma ya Mungu Baba imekwisha kufunuliwa kwetu kwa njia ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Huu ni ujumbe tunaoupata katika Dominika ya pili ya Mwaka C wa Kanisa. Hivi punde tu tumehitimisha kipindi cha Noeli ambapo tulitafakari kwa kina juu ya asili na utume wa Kristo kwetu wanadamu. Tukiyakariri maneno ya mwandishi wa Waraka kwa Waebrania tunapata fursa ya kuelezea kwa ufupi kuwa Kristo ni ufunuo timilifu wa Mungu kwetu sisi wanadamu: “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema nasi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu” (Ebr 1:1).

Huruma ya Mungu inayofunuliwa kwetu inaturudishia tena hadhi yetu,  inatupatia tena furaha yetu ya asili tuliyoipoteza kwa kumwacha Mwenyezi Mungu. Kristo anapokuwa katikati yetu anakuwa ni sababu ya kuendelea na furaha daima. Katika Somo la Injili tunathibitisha hilo. Bwana wetu Yesu Kristo akiwa pamoja na Mama yake Bikira Maria na mitume wake wapo katika kusanyiko la kawaida la kijamii. Ni tukio la Sherehe ya harusi katika Kana ya Galilaya.

Kwa jamii ya Kiyahudi kama ilivyo kwa jamii nyingine yoyote ile harusi ni tukio la furaha na linalokusanyisha watu wengi. Watu huwa katika hali ya umoja wakifurahi na kushangilia kwa sababu ya familia mpya inayoanzishwa ikiwa ni ishara ya uendelevu wa uhai kati yao. Moja ya vitu vinavyoichagiza sherehe hiyo ni kinywaji aina ya Divai. Katika kusanyiko hili la Kana ya Galilaya kunaingia mtimanyongo: “Hawana divai”.

Uwepo wa Kristo unaondoa kasirani hii inayojitokeza. Anarudisha tena furaha katikati ya watu wake. Somo la Injili linaendelea kutuambia kwamba, furaha hiyo inaonekana kuwa ni kubwa kuliko ya awali: “wewe umeiweka Divai iliyo njema hata sasa”. Hivyo, huruma hii ya Mungu inayofunuliwa na Kristo kati yetu inapata sifa ya ukuu kuliko furaha tunayojitengenezea sisi wanadamu. Kristo anatufunulia huruma ya Mungu ambayo ni Upendo wake alikuwanao kwetu, anaturudisha katika hali yetu ile ya kwanza tuliyokuwa nayo kabla ya anguko la wazazi wetu wa kwanza.

Huruma ya Mungu inayofunuliwa kwetu inathibitisha upendo wake mkuu ulio wa kudumu. “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia”. Ni maneno ya Nabii Isaya katika somo la kwanza yanayotupatia mwanga juu ya uhusiano kati ya Mungu na wanadamu. Mwenyezi Mungu muumba wetu anatupenda sana sisi viumbe wake. Daima anamtazama mwanadamu kwa jicho la huruma na hakomi kumwangaikia “hata haki yake itakapotokea kama mwangaza na wokovu wake kama taa iwakayo”. Mzaburi natuthibitishia hilo kwa kukariri kwamba “upendo wake mkuu wadumu milele” (Zab 136:1).

Mwanadamu pia anaalikwa kuitikia wito wa kuwa ufunuo wa huruma hii ya Mungu. Dominika iliyopita, yaani, Dominika ya Ubatizo wa Bwana tuliomba maneno haya katika sala ya ufunguzi: “utujalie sisi uliotufanya wanao tulipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu tudumu siku zote katika Upendo wako”. Wimbo wa Zaburi umetualika ukisema: “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana nchi yote, mwimbieni Bwana libarikini jina lake”. Huu ndiyo wito tunaopewa katika Dominika hii ambapo tupo mwanzo kabisa mwa kipindi cha kawaida cha Mwaka wa Kanisa. Katika kipindi hiki cha kawaida sote tunaalikwa kuyaadhimisha Mafumbo makuu ya Mungu katika maisha ya kawaida, yaani, kuwa mashuhuda wa Injili kama tunavyoagizwa na Kristo mwenyewe: “nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:8).

Mtume Paulo anatuonesha namna ya kuitikia wito huo. Kwanza anatuthibitishia utendaji wa Roho Mtakatifu katika huduma mbalimbali za kibinadamu na pili anaonesha kuwa kazi zote tuzitendazo ni za Mungu. Nguzo hizi mbili ndizo zinazoweza kutusaidia kutambua umuhimu wa miito yetu na ulazima wa kuitimiliza kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Mwanadamu akiwa tayari kuipokea huduma aliyopewa kama zawadi kutoka kwa Mungu atapata nguvu ya kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitekeleza huduma hiyo barabara.

Kwa njia hii yeye atakuwa ni ufunuo wa huruma ya Mungu kwa wengine, atakuwa ni sababu ya furaha kwa mwanadamu ambaye amejeruhiwa na anahangaika katika kuitafuta furaha itokayo juu. Hivyo, katika Dominika hii tunapewa wito wa kuitambua vyema na kuisikilza sauti ya Mungu kusudi tuwe mashuhuda na vyombo vya kuueneza upendo wake kwa wanadamu wote.

Mama yetu Bikira Maria, Yeye aliyekuwa wa kwanza kuitambua huruma ya Mungu katika harusi ya Kana ya Galilaya na kujifanya mshenga wetu kwa kujongea na kumwomba Mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Krsito, aliye ufununo wa huruma hiyo awe mwombezi wetu daima. Tusisite kumkimbilia yeye Mama yetu wa Huruma kusudi kwa huruma yake ya kimama azidi kutuombea kwa Baba pale tunapotindikiwa na divai. Tudumu katika utumishi wetu, kila mmoja kwa nafasi yake atende jinsi inavyotakiwa kwa wito wake kusudi wote tushiriki vema kuustawisha ufalme wa Mungu hapa duniani.

Tafakari hii inaletwa kwako na Padre Joseph Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.