2016-01-13 09:34:00

Familia ya Mungu Barani Afrika ijikite katika haki, amani na upatanisho!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kwa mwaka 2015 imekuwa ni changamoto kubwa kwa familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Lakini, ikumbukwe kwamba, amani inajikita kwa namna ya pekee katika msamaha, ukweli na uwazi; maridhiano pamoja na maelewano kati ya watu.

Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati walikuwa na kiu ya huruma ya Mungu inayojikita katika msamaha na ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko akaonesha upendeleo wa pekee kwa kufungua Lango la huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, tayari kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko na changamoto kwa familia ya Mungu nchini humo, kuambata misingi ya haki, amani, upendo, msamaha na maridhiano, tayari kuandika ukurasa mpya wa historia ya nchi yao.

Wanamchi wa Afrika ya Kati walikuwa na  mambo makuu matatu waliyomwonesha Baba Mtakatifu Francisko: Amani, Asante na Heshima! Familia ya Mungu nchini Afrika ya kati ilikuwa na wasi wasi ikiwa kama ingepata fursa ya kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao. Alipowasili, wakamshukuru kwa kuonesha ujasiri wa imani unaovuka woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko. Familia ya Mungu imeteseka sana nchini humo, kumbe, hija ya Baba Mtakatifu imeonesha kwamba, hata katika shida na mahangaiko pamoja na umaskini wao, lakini Kanisa bado linawaheshimu na kuwatambua kwamba ni watoto wa Mungu!

Hija ya Baba Mtakatifu Franciskonchini Uganda ilipania pamoja na mambo mengine kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha; tayari kwa wakristo wote kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake. Kenya, Baba Mtakatifu alitaka kuimarisha majadiliano ya kidini, kisiasa na kitamaduni, ili familia ya Mungu nchini Kenya iweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani, kikolezo kikuu cha ustawi na maendeleo ya watu.

Baba Mtakatifu ametoa hamasa kwa familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba inapambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; kwa kukazia utawala bora unaozingatia sheria na Katiba ya Nchi. Ni wajibu wa familia ya Mungu Barani Afrika kupambana kufa na kupona na umaskini wa hali na kipato kwa kuwa na sera nzuri zinatoa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana pamoja na kutunza mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila mwananchi anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika ujenzi na ustawi wa Kanisa na taifa katika ujumla wake.

Majadiliano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Vijana wa kizazi kipya nchini Kenya, yamekuwa ni muhimu sana kwa vijana katika mikakati yao kwa siku za uosni kwa kutambua kwamba, wanahamasishwa kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi yao na kamwe wasikubali kutumiwa na wajanja wachache katika mambo yanayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Vijana wawe ni mashuhuda wa Injili ya furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Kanisa Barani Afrika linaendelea kucharuka katika maisha na utume wake; ni Kanisa linalojitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili anasema Kardinali Filoni na liko tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika ongezeko la viongozi wa Kanisa tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kuna Maaskofu, Mapadre na Watawa mahalia wanaotekeleza dhamana na wajibu wao barabara.

Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba, Wakleri na watawa wanapata majiundo na malezi bora zaidi: kiroho, kiakili, kiutu na kichungaji. Kuna baadhi ya nchi ambazo kuna ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa, haya ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kulikwamisha Kanisa Barani Afrika. Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, litaendelea kushirikiana na Makanisa mahalia Barani Afrika, ili kutoa malezi na majiundo makini kwa Wakleri na watawa.

Ikiwa Kanisa Barani Afrika litakuwa na Mapadre waliofundwa vyema, ni rahisi pia kupata Maaskofu wema na watakatifu kwa ajili ya Kanisa la Mungu Barani Afrika. Kanisa Barani Afrika halina budi kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho, ustawi na maendeleo ya wengi. Waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuishi kwa amani na usalama, kwa kusaidiana na kushirikiana kwa hali na mali. Tofauti za kidini ni utajiri unaopaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.