2016-01-13 14:10:00

Asiyekuwa na mwana aeleke jiwe, hapa leo hapatoshi!


Arusi inajulikana na wengi, hata wazamiaji hawakosi katika matukio kama haya! Sherehe zake huandaliwa vizuri sana. Waandaaji huiandaa sherehe ili wanandoa na waalikwa wafurahi bila kuumbuka. Leo tutashuhudia ndoa moja iliyonusurika kuumbuka kwa sababu kulikosekana vinywaji. Bahati nzuri mama mmoja  hatajwi jina, alikuwa katika mazingira hao, akaendea kulia hali kwa mtoto wake aliyealikwa arusini, ndiye aliyeokoa jahazi. Hali halisi ilikuwa hivi: “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Divai  ilipowatindikia mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.” Yesu akafanya muujiza akageuza maji kuwa divai. Kitendo hicho cha kwanza na cha namna yake alichofanya Yesu kinahitimishwa hivi: “Mwanzo huu wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.”

Arusi hii na tendo alilofanya Yesu vimejaa utata na kuzua maswali yasiyo na majibu. Mathalani ukiangalia mazingira ya arusi, hasa kutokana na idadi ya makasiki yaliyolundikana pale nyumbani yaonekana arusi ilikuwa ya watu tajiri, inashangaza kukosekana divai. Aidha, mwandaaji angeweza kuitisha mchango wa papo kwa papo na kununua divai nyingine. Halafu Yesu wenyewe angetaka kuwaridhisha watu angeweza kufanya muujiza wa maana zaidi kuliko kuongeza pombe. Kadhalika tungeweza kuelewa vizuri zaidi endapo “kudhihirika utukufu wake,” kungetamkwa baada ya kumhuisha Lazaro toka wafu kuliko katika tendo la kugeuza maji kuwa pombe.

Kwa vyovyote vile simulizi hili ni la kitalimungu. Yasemwa: “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana ya Galilaya.”Arusi hii ya Kana ni sampuli ya arusi zote zilizoishafanyika na zinazoendelea kufanyika hapa duniani. Aidha, nabii Hosea na manabii wengine wanafananisha arusi na mahusiano yaliyoko kati ya Mungu na binadamu. Kutokana na upendo usio na mipaka alio nao Mungu kwa taifa la Waisraeli, mahusiano yao ni kama ya wanandoa. Ndoa kati ya Mungu na binadamu ilishafungwa pale binadamu alipoumbwa na kuwekwa paradisini. Lakini ndoa hiyo iliingia dosari kutokana na mtu kutomtii Mungu. Lakini ikafungwa tena upya katika maagano ya mlimani Sinai. Hapo Waisraeli wakaambiwa rasmi kuwa wao ni taifa la kifalme, la kikuhani na bi arusi wa Bwana. Ndoa hiyo ikaingia tena dosari hata haikupendeza, ndipo ulipohitajika mkataba mpya wa ndoa ilifungwa rasmi “siku ya tatu,” yaani siku ya ufufuko wa Yesu. Hapo watu wote walialikwa kuwa taifa la kifalme, la kikuhani na bi arusi wa Mwanakondoo yaani Yesu Kristo.

Baada ya maelezo haya tunaletewa mhusika wa kwanza aliyekuwa katika arusi: “Naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.” Mama asiyetajwa jina, atakuwa pia chini ya msalaba. Mama huyu ni Taifa la Israeli lililo bi arusi wa Mungu alimozaliwa Yesu anayetajwa hapa kama mwalikwa.  Mama wa bi-arusi Israeli akaona hali halisi, akajitosha kumweleza mtoto wake hali halisi: “Hawana divai.” Neno hili divai linatokea mara nyingi atika Agano la kale na linafumba maana nyingi kama vile kuburudisha, kuchangamsha, kufurahisha, sikukuu, uzuri, nk. “Divai huburudisha maisha.” (Mhubiri au Kohelethi 10:19). “Jinsi zilivyo nzuri pambaja zako, umbu langu, bibi arusi, ni nzuri kupita divai!” (Wimbo ulio bora 4:10).”Mvinyo ni furaha ya moyo na changamko la roho” Yoshua bin Sira 31:28) “divai inafurahisha moyo wa mtu.” (Zab 104:15) “Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wakeataandaa katika mlima huu sikukuu, na divai nzuri.” (Isaya 25:6). Kwa hiyo “hakuna divai” maana yake arusi haijachangamka. Mama huyu anawawakilisha watu waaminifu wa Taifa la Israeli lililomzaa masiha, anayemwendea mwana wao kuinusuru ndoa yao.

Yesu anamjibu: “Mwanamke, tuna nini mimi nawe?” Jibu hili analotoa Yesu linadhihirisha kuwa hakukuwa mahusiano yoyote kati ya Mungu na binadamu, kwani linalingana na jibu alilotoa mtu yule aliyepagawa na pepo: “Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu?” (Mk 5:7) Kisha Yesu anaendelea kusema: “Saa yangu haijawadia.” Hapa anataka kusema kwamba sasa unaanza uhusiano mpya. Kwa tamko hili Yesu alitaka kusema kuwa amefika kuanzisha mahusiano mapya. “Ya kale hayakooo!” Upendo huo wa Mungu utadhihirika waziwazi Msalabani atakaposema “Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.” (Yoh 12:23).

Wahusika wa pili ni watumishi:“Mama akawaambia watumishi, lolote atakalowaambia, fanyeni.” Maagizo ya mama yanawataka watumishi kuyatii maagizo ya mwanae Yes una kutoka kwa Kristu pekee yake kunapatikana uhusiano mpya. Aidha, ukitaka kuwa na mahusiano ya furaha na Mungu uende kuchota maji kwenye kisima cha wokovu.

Kiini cha fasuli ya leo ni mabalasi yaliyokuwa katika arusi yak ana: “Kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.” Mabalasi haya yanawakilisha madhehebu na dini ya waisraeli ya kutawadha. Yalikuwa Mabalasi sita, namba isiyo kamili. Idadi hiyo ilisubiri kukamilishwa na namba saba. Mabalasi hayo yalikuwa ya mawe kama zile mbao za Amri kumi za Mungu zilizoandikwa katika mawe, amri ambazo zilitakiwa kufuatwa kikamilifu moja baada ya nyingine. Halafu mabalasi yenyewe ni tupu, hayana kitu ndani maana yake yamefilisika sera.

Kwa hiyo, ndoa au mahusiano ya taifa la Israeli na Mungu haikuwa na furaha, kwani ilikosa divai. Kukosa furaha ni alama ya kukata tamaa, kukosa upendo, dira hata mwelekeo wa maisha. Matokeo yake ni kujikatia tamaa mwana kwetu! Ndivyo ilivyo ndoa yoyote ile isiyokuwa na furaha. Tunapokosa furaha hatuwezi kuona tofauti kunapokuwa na sikukuu kwani hakuna upendo. Yatubidi tujihoji endapo Ibada zetu zinatufanya tujisikie kuwa kweli ni waamini wenye furaha na kujumuika kikamilifu kama wanavyodai Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican? Au tunakwenda Kanisa kama watazamaji na wasikilizaji tu?

Wahusika wa tatu ni watumishi, ambao Yesu anawatuma kazi ya kufanya: “Jalizeni mabalasi maji.” Hapa tunaona mchango wa watumishi (diakonia). Hawa watumishi wanalinganishwa na Makatekista na wote wanaojitoa kutumikia Kanisa kwa kuchota maji yatakayogeuzwa kuwa divai, yaani kutangaza upendo unaoleta furaha (divai) na kuchangamsha mioyo ya watu kwa kuwaonjesha huruma ya Mungu, mada inayopigiwa debe wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Mhusika wa nne ni Mkuu wa meza. Yesu akawaambia watumishi, “sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza.” Mkuu wa meza ananukuliwa mara nyingi kuliko anavyotamkwa Bwana arusi. Huyu ndiye aliyeiandaa sikukuu mchochoro isiyochangamsha watu. Mkuu huyu wa meza ni Makuhani waliokuwa wanahangaika kuleta mahusiano na Mungu yasiyoleta furaha. Leo tunao pia Wakuu wa meza wasiotambua kwamba madhehebu hayaleti furaha kwa waamini.  Mkuu wa meza alipoonja ile divai akaona  “hii mpya, kali kupindukia” Kwa Lugha ya Kilatini wanasema,”Bhunu mbundi wasu” Ndiyo maana akamwita bwana arusi, na kumpongeza kama vile angekuwa yeye aliyeiandaa kumbe aliandaa Bwana arusi mpya: “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.”

Ama kweli, Pasaka iliyokuwa “Siku ya tatu” ni ndoa iliyochangamka, Yesu alisema kweli: “libomoeni Hekalu hili nami nitalijenga kwa siku tatu.” Hekalu la kubomoa ni yale mahusiano ya kale kati ya Mungu na binadamu na sasa tusherekee mahusiano mapya ya divai inayochangamsha yaani upendo wa Damu azizi ya Kristo. Pale ambapo divai ya huruma, upendo, msamaha, mshikamano, uvumilivu na udumifu inapokosekana, wanandoa wasifanya masihala, bali chapu chapu wakimbilie katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, hapo atawaombea kwa Mwanaye mwingi wa huruma na mapendo, na furaha, amani na kicheko vitaweza kurejea tena katika maisha ya kifamilia na waamini katika ujumla wao! Yaani sipati picha!

Na Padre Alcuin Nyirenda. OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.