2016-01-12 13:42:00

Serikali ya Tanzania imechangia mill. 35 kukarabati Kituo cha Afya Chipole


Kanisa daima limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwenye sekta ya afya, kwani linapenda kufuata nyayo za Yesu Kristo aliyetangaza Neno, akawaponya wagonjwa na kuwaondolea watu dhambi zao. Kwa njia ya taasisi za huduma ya Afya, Kanisa linapenda kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wahudumu wa vituo vya sekta ya afya vinavyomilikwa na kuendeshwa na Kanisa hawana budi kutambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, kumbe, mbele yao kila mgonjwa anayeteseka ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi kama ilivyojitokeza kwa Kituo cha Afya cha Chipole kuungua moto kunako mwaka 2013. 

Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa imeahidi kukamilisha ukarabati wa Kituo cha Afya cha Chipole, kilichopo Jimbo kuu la Songea kilichopata majanga ya moto baada ya kituo hicho kuungua mwaka 2013 na Ofisi hiyo kutoa fedha za kukikarabati. Akiongea wakati wa ziara ya kukagua ukarabati wa  kituo hicho, tarehe 12 Januari, 2016,  Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi  Msuya amebainisha kuwa kufuatia kuungua kwa hospitali hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa kiasi cha shilingi milioni 35 kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho. “Tumekagua ukarabati wa kituo hiki cha afya  na tumeona pamoja na kuambiwa na uongozi wa hospitali hii kuwa pamoja na fedha tulizozitoa lakini bado kuna mahitaji ya msingi yanahitajika ili hospitali hii iweze kuwahudumia wanakijiji wanao izungunka hospitali hii. Tunaahidi kukamilisha ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti pamoja na maabara” alisema Msuya.

Awali akitoa maelezo ya maendeleo ya ukarabati wa kituo hicho cha afya , Makamu wa Mama Mkuu wa Shirika la Watawa wa Mtakatifu Agnes, Chipole, Sr. Sairis Mkinga, alifafanua kuwa pamoja na mapungufu ya chumba cha maabara lakini bado kituo hicho cha afya kinao upungufu wa vyumba vya kuhudumia wagonjwa. “Tunayo changamoto  bado ya kuwa na sehemu maalum ya Mapokezi ya wagonjwa na wagonjwa kupokea  dawa.

Pia panahitajika mahali kwa akina mama wajawazito kujifungulia kwani kwa sasa vyumba hivi viko karibu sana na vyumba vya wanaume lakini tunahitaji  chumba maalum kwa ajili ya kliniki ya watoto” alisisitiza Sista Mkinga. Kituo cha Afya cha Chipole kilichopo Kata ya Magagura wilayani Songea vijijini kinamilikiwa na Shirika la Watawa  wa Mtakatifu Agnesi Chipole Jimbo kuu la Songea na  kinahudumia takribani wakazi 7,434  wa kata hiyo, hivyo kukamilika kwa Hospitali hiyo kutawezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na uboreshaji wa hali za afya za wakazi hao.

Maboresho ya huduma za afya kituoni Chipole, yanalenga kwa namna ya pekee kuwahudumia wagonjwa, hawa ambao ni sehemu muhimu sana ya utume na maisha ya Kanisa, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa uhai na mauti, kumbe, kila mtu anapaswa kuwa kweli ni shuhuda wa Injili ya uhai!

Na mwandishi maalum.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.