2016-01-12 09:08:00

Miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar, mkwamo wa kisiasa na Dr. Magufuli aonesha upendo


Wananchi wa Zanzibar wanasherehea kumbu kumbu ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Dr. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 alisema kwamba, Mapinduzi ya Zanzibar ni kielelezo muhimu sana cha ukombozi na uzalendo wao. Wananchi wanahamasishwa kushiriki kwa wingi katika maadhimishjo haya ili kuendeleza shabaha ile waliyokuwa nayo waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar. Wananchi wasimame kidete kudumisha amani, umoja wa kitaifa na maendeleo ya wengi, kwani haya ni matunda ya Mapinduzi Zanzibar.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar. Akizungumza na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.

“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif. Makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.

Aidha, Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye. Maalim Seif amesema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.  Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi na Baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake. Mbali na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.

Ameitaka ZEC iongozwe na Makamu Mwenyekiti wake kwa mujibu wa Katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi. Maalim Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubali.

Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 11 Januari, 2016 amemtembelea na kumpa pole Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Frederick Sumaye ambaye amelazwa katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Frederick Sumaye alilazwa katika Taasisi hiyo siku nne zilizopita kwa matibabu ya moyo na madaktari wanaomtibu wamemhakikishia Rais Magufuli kuwa anaendelea vizuri ikilinganishwa na wakati alipofikishwa katika Taasisi hiyo. Pamoja na kumpa pole, Rais Magufuli pia amemwombea apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kuonana na Rais, Waziri Mkuu Mstaafu Sumaye amemshukuru Rais Magufuli kwa kwenda kumuona na kueleza kuwa kitendo hicho kimeonesha jinsi alivyo na upendo wa dhati na anavyowajali watu wake. Kuhusu hali yake, Mheshimiwa Sumaye amesema anaendelea vizuri, anapata matibabu mazuri na kwamba kwa kuwa hali yake ni nzuri anatarajia kuruhusiwa kuondoka hospitali hapo baada ya muda mfupi.

Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli amemtembelea na kumpa pole mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere kufuatia kifo cha Mkwewe Leticia Nyerere kilichotokea huko Maryland, nchini Marekani alikopelekwa kwa ajili ya kupata matibabu mapema mwezi huu. Pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli pia amewapa pole wanafamilia wote na amewaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.

Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere Bwana Joseph Butiku amemueleza Rais Magufuli kuwa familia inaendelea na taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani na itatoa taarifa baadaye.

Wakati huo huo, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatoa taarifa kwa umma kwamba:

(a) Kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano amepewa mamlaka ya kuteua Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa namna ambayo itawezesha kila Mbunge kuwekwa kwenye Kamati mojawapo. Katika kufanya uteuzi huo, Spika huzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa katika Kanuni ya 116 (5);

(b) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Job Yustino Ndugai (MB), ametekeleza mamlaka yake ya uteuzi kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo juu, kwa kuwateua kwanza Wabunge Kumi na Tano (15) kuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge. Kamati hiyo imeundwa na kutangazwa kabla ya Kamati zingine ili ifanye marekebisho ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu majukumu ya Kamati zingine za Bunge kwa kuyashabihisha na majukumu ya Serikali kwa kuzingatia Muundo wa Baraza la Mawaziri lililopo sasa. Lengo kuu ni kuleta urahisi, ufanisi na tija kwa Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali;

(c) Kwa msingi huo, Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambayo Spika ndiye Mwenyekiti wake na Naibu Spika ni Makamu Mwenyekiti, Kiongozi wa Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni Wajumbe kwa nyadhifa zao itakutana katika Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 15 Januari, 2016 saa tano kamili asubuhi katika Ukumbi wa Spika. Wajumbe wengine ni: -

(i) Mhe. Makame Kassim Makame, MB. - Jimbo la Mwera;

(ii) Mhe. Tundu Antipas Mughwai Lissu, MB. - Jimbo la Singida Mashariki;

(iii) Mhe. Jasson Samson Rweikiza, MB. - Jimbo la Bukoba Vijijini;

(iv) Mhe. Ally Saleh Ally, MB. - Jimbo la Malindi;

(v) Mhe. Magdalena Hamis Sakaya, MB. - Jimbo la Kaliua;

(vi) Mhe. Salome Wycliff Makamba, MB. - Viti Maalum;

(vii) Mhe. Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, MB. - Viti Maalum;

(viii) Mhe. Zainab Athman Katimba, MB. - Viti Maalum;

(ix) Mhe. Balozi Adadi Mohamed Rajab, MB. - Jimbo la Muheza;

(x)Mhe. Dkt. Charles John Tizeba, MB. - Jimbo la Buchosa; na

(xi) Mhe. Kangi Alphaxard Lugola, MB. - Jimbo la Mwibara.

(d) Spika atakamilisha uteuzi wa Wajumbe katika Kamati zingine za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge tarehe 26 Januari, 2016, Mjini Dodoma ili kutoa fursa kwa Kamati zote kuchagua Viongozi wake na kuandaa Mpango Kazi kwa mwaka 2016/17; na

(e) Wabunge wote wanatangaziwa kuwa wawe wamefika Dodoma tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa kuanza kwa Kamati za Bunge na Mkutano wa Bunge, isipokuwa Kamati ya Wabunge (Caucus) wote wa Chama cha Mapinduzi wanatakiwa kuwa Mjini Dodoma tarehe 17 Januari, 2016 kwa Mkutano wao.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.