Mabadiliko katika Kanisa hayaletwi na sala za Mapapa au Maaskofu au Mapadri peke yao lakini huletwi na sala na maombi ya waamini Wakatifu wa Kanisa. Na kwa sala na maombi miujiza hutendeka na huwa na uwezo kuilainisha mioyo migumu, hata iliyosahau huruma ya Mungu. Ni msisitizo wa Mahubiri ya Baba MtakatifuFrancisko, mapema Jumanne hii wakati wa Ibada ya Misa aliyoiongoza katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta mjini Vatican. .
Homilia ya Papa ililenga kutoa ufafanuzi juu ya masomo ya siku hasa kutoka Kitabu cha Samueli linalozungumzia Mwanamke Anna, mwanamke tasa ambaye hakuchoka kutoa maombi na kilio chake kwa Mungu,akiomba kujaliwa mtoto.
Papa ameutaja ujasiri wa sala katika imani kama ilivyokuwa kwa Anna, licha ya hali yake mbaya ya kimaisha kwamba, sala zake zilitoka ndani ya moyo wake, midomo yake ikionekana kunena lakini bila sauti yake kusikika, hata kuonekana kama vile ni mlevi wa mvinyo . Papa anasema ameutaja ujasiri huu wa Anna katika kuomba neema ya Bwana, kuw ani ujasiri katika imani. Kwa hisia hizo Papa Francisko,amewakumbuka wanawake wengi wema ndani ya Kanisa ambao hutoa maombi ya kwa Mungu kwa jasiri na bila kuchoka ,ingawa mara nyingi Kanisa haliwatambui wala kufanya rejea kwao. Amesema ni wanawake wachache tu wanaokumbukwa na Kanisa katika ujasiri wa maombi na sala kama Mtakatifu Monica ,ambaye kwa machozi yake aliweza kupata neema ya kuyaongoa maisha ya mwanae Mtakatifu Augustine. Lakini kumbe kuna wanawake wengi wa namna hiyo.
Aidha Mafundisho ya Papa yalimwelekea Kuhani Eli, mtu maskini ambaye Papa Francisko, anamwonea huruma na kusema anamkubusha mapungufu yake, na kumpa ufahamu zaidi , wa kutambua jinsi gani ilivyokuwa vyepesi kuhukumu watu wengine kwa jinsi wanavyoonekana bila hata ya kujiuliza kwa kina wanayo fikiri nini mioyoni mwao? Na kwamba pale panakosekana huruma ndani ya moyo, daima fikra huelekea katika uovu ,wenye kumweka mtu mbali na mbali na yule anayesali kwa maumivu na uchungu ,ambaye huweka dhamana maumivu na uchungu huo kwa Bwana.
Baba Mtakatifu Francisko aliendelea kulinganisha maumivu na uchungu katika sala kama ilivyokuwa kwa Yesu katika bustani ya Mizeituni, aliposali kwa uchungu na maumivu makubwa, lakini kwa radhi na unyenyekevu alisema, Baba, si kwa mapenzi yangu lakini utakalo lifanyike. Hivyo tunaona kwamba, Yesu pia alitembea katika maumivu na uchungu wa sala kama ilivyokuwa kwa Anna, kuomba kwa unyenyekevu mwingi bila kukoma. Na hivyo ndivyo inavyotakiwa ,kutolea sala zetu kwa upole na unyenyekevu na kumwachia Mungu, mwenywe atoe jibu lake kwa jinsi anavyoona inatufaa. Papa anasema hakuna kukata tamaa ,ni kuendelea kuomba neema ya Mungu kwa uchungu wote wa moyo hadi kupata jibu .
Papa alieleza na kutoa mfano mwingine wa baba mmoja huko Buenos Aires, ambaye binti yake mwenye umri wa 9 alikuwa katika hatua za mwiso wa maisha yake hosptalini alikokuwa amelazwa , ambaye usiku mzima, baba huyo alikesha katika lango la Madabahu ya Mama Bikia Maria wa Luján akiomba neema ya binti yake kupona ambaye siku iliyofuatia,alimkuta mwanae hospitalini akiwa ameponywa kimiujiza. Papa alieleza na kukamilisha homilia yake na himizo kwamba ,watakatifu ni wale ambao wanaamini kwamba, Mungu ni Bwana na anaweza fanya jambo lolote.
All the contents on this site are copyrighted ©. |