2016-01-11 11:48:00

Vatican ina uhusiano wa Kidiplomasia na Nchi na Mashirika ya Kimataifa 186


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 11 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya kimataifa yenye uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2016, kuna nchi 180 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Licha ya nchi hizi, pia kuna Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Malta, Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina. Hapo tarehe 4 Juni 2015 Vatican imekuwa pia ni mwanachama mtazamaji wa Jumuiya ya Caraibi, CARICOM.

Balozi na Mashirika ya Kimataifa yenye makao yake mjini Roma kwa sasa ni 86 baada ya nchi za Belize, Burkina Faso, Guinea Ekwatorio pamoja na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina kuanzisha makao yake mjini Roma. Umoja wa Nchi za Kiarabu, Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pia ya makazi yake mjini Roma.

Taarifa inaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015, Vatican imeridhia mikataba minne. Mkataba wa kwanza ni kati ya Vatican na Serikali ya Italia kuhusiana na masuala yak odi, uliotiwa sahihi hapo tarehe 10 Juni 2015. Tarehe 26 Juni 2015 Vatican iliweka sahihi mkataba wa jumla na Serikali ya Palestina. Tarehe 14 Agosti 2015 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor  ya Mashariki na Vatican wakatiliana mkataba wa kisheria kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini humo. Tarehe 22 Juni 2015 Serikali ya Chad ikatia sahihi mkataba na Vatican kuhusu masuala ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo. Tarehe 10 Septemba Sektretarieti ya Vatican imewekeana sahihi mkataba wa maelewano na Serikali ya Kuwait kuhusu masuala yanayopaswa kufuatiliwa baina ya nchi hizi mbili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.