2016-01-11 07:26:00

Tunzeni neema ya Utakaso ndani mwenu!


Tunasherehekea Ubatizo wa Bwana – ambapo kadiri ya Mwinjili Yohane ni mwanzo utume wa kimasiya wa Yesu Kristo. Mwanzo wa utume huu wa Kimasiha, utakamilika katika mateso, kifo na ufufuko, ondoleo kamili la dhambi – Yoh. 1:29. Kwa ufupi Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Bwaba inagusia mambo makuu yafuatayo:

  1. Somo la kwanza – laeleza utume wa Yesu kama Masiha, anayetoa neema. Huyu ni mtumishi wangu, ninayependezwa naye. Nimeweka roho yangu juu yake, ataleta amani kwa mataifa.
  2. Somo la pili – Mt. Petro – katika ubatizo – mpakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu, tayari kufanya kazi na
  3.  Injili – Yesu anapokea ubatizo ili kutimiza sheria kadiri ya taratibu za Kiyahudi. Katika tendo hili – linatoka tamko – huyu ni mwanangu mpendwa wangu, msikilizeni yeye. Kwa sababu ya dhambi ya asili, kila azaliwaye huwa na dhambi.

Ibada mbalimbali za Kiyahudi kadiri ya Maandiko Mtakatifu

  1. Kutahiriwa – Lk. 2:21
  2. Kutolewa Kekaluni – Lk. 2:22-23
  3. Ubatizo – Mt. 3:13-17.

Ubatizo wakati huu ulikuwa na maana tofauti:

  1. Kutakaswa
  2. Kujiweka sawa na Mungu
  3. Kuonesha imani kwa Mungu
  4. Kama alama ya toba
  5. Kupata uanachama katika jamii ya Kiyahudi. Yesu anaingia hapa. Yohani alitoa ubatizo wa toba – Mt. 3:13-17, Yesu alikuwa kama sisi isipokuwa dhambi – Fil. 2,7; Ebr. 4;15; Rom.8.3. Yesu alipokea ubatizo ili kujiweka sawa na Mungu, kuzaliwa katika familia ya Mungu

Je Yesu alihitaji kubatizwa? Siyo. Kwa tendo hili, alionesha ushirika nasi. Pia aliweka mwisho kwa ubatizo wa maji na kuanza ule wa Roho. Hakuja tu kufunua Umungu wake kwetu, amekuja pia kujifunua kwetu kama mwanadamu. Ni Mungu kweli na Mtu kweli. Ubatizo wake ni wokovu wetu. Anafanana nasi ila bila dhambi. Anageuza hali yetu toka ubinadamu tu na kuupa hadhi ya kimungu. Hivyo nasi kwa ubatizo, tunakuwa wapendwa wake Mungu. Na kama alivyofanya Yesu baada ya ubatizo – kutangaza kwa maisha yetu yote Ufalme wa Mungu.

Ubatizo wa Kristo – waonesha ni zaidi ya kuoshwa kwa maji au kusafishwa. Mbatizwa huzaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa tendo la ubatizo wa Yesu, utukufu wa Mungu ulifunuliwa kwa Roho Mtakatifu kushuka juu yake – huyu ndiye mwanangu mpendwa, msikilizeni yeye. Inakamilisha fundisho la Yohani Mbatizaji – yeye ajaye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto – Mt. 3:11. Kumbuka mwaliko wa Yesu kwa Nikodemo – mtu asipozaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu, hataingia ufalme wa mbinguni – Yoh. 3:3-5.

Yesu hakubatiza ye yote  - Yoh. 4:2, ila ubatizo aliopokea ni tofauti na ule aliowafundisha wafuasi wake kufanya. Aliwaalika wabatize kwa Roho – Mt. 28;19. Na hapa kuna tofauti na aina ya ubatizo uliofanyika wakati wake. Kwa njia hii, wafuasi walitoa sakramenti ya ubatizo kwa waongofu wote kabla ya kujiuga na imani na kuabudu pamoja nao – Mdo. 2:37-39 – wito wa uongofu – waliposikia hayo walichomwa moyo, na wakamwuliza Petro na mitume wengine, tufanya nini, enyi ndugu? Petro akawajibu, tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina lake Yesu Kristo, mpate kuondolewa dhambi zenu; nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana ahadi hii imefanywa kwa ajili yenu na watoto wenu, na wale wote wa mbali, atakaowaita kwake Bwana Mungu wetu.

Kwa ubatizo wake Kristo, umewekwa msingi wa namna mpya ya kupata neema. Mbatizwa huanzisha uhusiano mpya na – UTATU MTAKATIFU.

Rebirth – kuna kuzaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu, kuoshwa toka dhambi ya asili na kuwa waana wa Mungu. Initiation – tunakuwa wana wa Mungu na watu wa Taifa lake. Consecration – tunapakwa mafuta na kutolewa ili kuwa watangazaji wa ufalme wake. Tunakuwa watumishi wa Mungu. Empowerment – twapokea Roho Mtakatifu, anayetuwezesha na kutupa nguvu dhidi ya shetani.

KKK – 1213 – Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho (vitae spiritualis ianua), na mlango unaowezesha kuzipata sakramenti nyingine. Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru toka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume wake: Ubatizo ni sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika neno.

Mdo. 10:37-38 – mmejua yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya ubatizo aliohubiri Yohani, jinsi Mungu alivyompaka mafuta Yesu wa Nazareti kwa Roho Mtakatifu na nguvu. Na jinsi alivyozunguka katika nchi yote akitenda mema na kuwaponya wote walioonewa na shetani, kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

 Katika Injili ya Yohani tunasoma neno hili –  Yoh. 5:3-9 – humo walilala wagonjwa wengi, vipofu, viwete na wenye kupooza. Pale palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa tangu miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona amelala huko, akajua ya kuwa amekuwa na hali hiyo muda mrefu, akamuuliza, je, wataka kuwa mzima. Mgonjwa akamjibu, bwana, sina mtu wa kunishusha bwawani yanapovurugika maji. Kila ninapojaribu kushuka, mwingine anakuwa amekwisha shuka kabla yangu. Yesu akamwambia, simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda.

Katika kuzaliwa huko upya tunapata:

1. ondoleo la dhambi – Zab.51:5 – kwa maana natambua makosa yangu, na dhambi yangu ipo daima mbele yangu.

2. tunapokea Roho wa kuwa wana na wanachama wa kanisa – Rum. 8:8-15 - .... kwani wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni wana wa Mungu. Kwa maana hamkupata roho ya utumwa mwogope tena, bali mmempokea roho anayewafanya kuwa wana wa Mungu na kuita, ABBA! Baba.

3. tunakuwa warithi wa ufame wa mbinguni – Fil. 3:17-21 – ndugu mniige mimi. Waangalieni wale wanaopanga mwenendo wao kadiri ya mfano tuliowapeni .... bali kwetu ni mbinguni, na kutoka mbinguni atakuja mwokozi, Bwana Yesu Kristo, tunayemtazamia.

Hivyo ubatizo unatuunganisha na Kristo, na katika muungano huu, tunapata nguvu ya kuendelea mbele na kutenda mema katika Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Tunapata neema ya kuishi kama watoto wa Mungu katika imani – Gal. 2:20 – si mimi tena ninayeishi, bali ni Kristo anayeishi ndani yangu. Muda ninaoishi bado mwilini, ninaishi katika imani inayomtegemea Mwana wa Mungu, ambaye amenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

Kol. 2:20 – kama mlikufa pamoja na Kristo katika mambo ya dunia, kwa nini bado mko chini ya sheria zake kana kwamba mnaishi bado ulimwenguni?

Kol. 3:4 – baadaye, Kristo aliye uzima wetu atakapotokea, ninyi pia mtatokea pamoja naye katika utukufu.

Ni wajibu wa wabatizwa sasa kuishi neema hii kila siku ya maisha yetu tukiepuka dhambi – Yoh. 8:34-36.

 KKK – 1227 – Kadiri ya Mtakatifu Paulo mtume, kwa ubatizo, mwamini hushiriki mauti ya Kristo, huzikwa pamoja naye, na hufufuka pamoja naye: Tulipobatizwa katika Kristo Yesu, tulibatizwa katika mauti yake. Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. – Rum. 6:3-4; Kol. 2:12. Wabatizwa wamemvaa Kristo – Gal. 3:27. Kwa njia ya roho Mtakatifu Ubatizo ni kuoshwa kunakotakasa, kunakotakatifuza na kuhesabia haki – 1Kor. 6:11 – 12:13

Sikukuu hii hutupa nafasi ya kutafakari ubatizo wetu. Ubatizo ni zawadi iliyotolewa kwetu kwa mapendo ya Kristo. Katika Mk. 16:16 – aaminiye na kubatizwa ataokoka. Yesu aliweka sakramenti kama njia ya wokovu. Mungu anapenda watu wote waokoke na watambue yaliyo kweli – 1Tim. 2:4.

Pd. Reginald  Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.