2016-01-11 10:45:00

Ratiba elekezi ya Ibada zitakazoongozwa na Papa Francisko Januari-Februari


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Februari 2016 anatarajiwa kuadhimisha Masifu ya Jioni kwa ajili ya Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, mwalimu na  mtume wa mataifa, hapo tarehe 25 Januari 2016. Hii itakuwa ni siku ya kufunga Juma la kuombea Umoja wa Wakristo ambalo kwa mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu “Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu”. Tafakari za maadhimisho kwa mwaka huu zimeandaliwa na Umoja wa Wakristo kutoka Lithuania. Ibada ya Masifu ya jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma itaanza saa 11: 30 kwa saa za Ulaya.

Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 2 Februari 2016, Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican majira ya saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko atafunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliozinduliwa wakati wa Kipindi cha Majilio cha Mwaka 2015.

Tarehe 10 Februari 2016, Jumatano ya Majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, mwaliko kwa waamini kutubu, kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma kiroho na kimwili; Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Ibada ya kupaka majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Hii itakuwa siku ambayo Wamissionari wa huruma ya Mungu watatumwa sehemu mbali mbali za dunia ili kuwaondolea waamini dhambi ambazo kimsingi zimetengwa kwa ajili ya Kiti cha kitume au Maaskofu peke yao, ili kuwaonjesha waamini utajiri wa Fumbo la huruma ya Mungu.

Hawa ni ishara hai ya namna Baba anavyowapokea wale wanaotafuta msamaha wake. Watakuwa ni Wamissionari wa huruma kwa sababu watakuwa wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamejikita katika ubinadamu, chimbuko la wakovu, wajibu na mwanzo mpya ili kushinda vikwazo vinavyomwandama mwanadamu. Wamissionari hawa wataongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi, ili awarehemu wote” (Rom. 11:32). Waamini wote wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kupokea wito wa huruma. Wamissionari wanapaswa kuuishi wito huu kwa kumkazia macho Yesu Kuhani mkuu mwenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu.

Ratiba elekezi ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha kwamba, kuanzia tarehe 12 hadi 18 Februari 2016, atakuwa na hija ya kitume Nchini Mexico, ambako anapenda kwenda kutoa heshima zake za dhati kwa Bikira Maria wa Guadalupe, msimamizi wa Amerika ya Kusini. Ratiba ya yale yatakayojiri wakati huo, itatolewa kwa wakati muafaka.

Tarehe 22 Februari 2016 katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:30 kwa saa za Ulaya. Hii itakuwa pia ni siku ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu yaani “Curia Romana”. Hivi ndivyo anavyofafanua Monsinyo Guido Marini, Mshehereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.