2016-01-11 15:00:00

Papa akutana na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Vatican


Kama ilivyo kawaida kwa kila mwanzo wa mwaka, kwa Khalifa wa Mtume Petro, kukutana na Mabalozi na wawakilishi wa Nchi Vatican, kwa nia ya  kutakiana mema kwa Mwaka Mpya,  Papa Francisko, Jumatatu hii alikutana na Mabalozi na wawakilishi wa Nchi Vatican. Kundi hilo la Wanadiplomasia liliongozwa na Balozi Armindo Fernandes do Espirito Santo Veira , Balozi wa Angola, ambaye kwa sasa ndiye Dekano wa Mabalozi. 

Papa kwa namna ya kipekee katika  salaam zake , aliwakumbuka Marehemu Balozi Rodney Alejandro  Lopez Clemente wa Cuba na Balozi Rudolfo p. Von Ballmoos wa Liberia , waliofariki mwezi uliopita.

Aidha Baba Mtakatifu aliitumia nafasi ya Mkutano huu kuwakaribisha Mabalozi wote wapya na alionyesha kufurahia ongezeko la Mabalozi wanaoshi Roma ikilinganishwa na mwaka uliopita, akisema  ni ishara nzuri na muhimu yenye kuonyesha kwamba,  jumuiya ya kimataifa,  inafuatilia kwa ukaribu shughuli za kidiplomasia za Jimbo la Papa. Na kwa namna ya kipekee Papa alifanya rejea katika  baadhi ya  juhudi za kidiplomasia zilizofanikisha uwepo wa makubalino kati ya Jimbo la Papa na nchi ya  Italia na Marekani , katika tafakari makini za wajibu wa Jimbo la Papa katika kuonyesha uwazi  kwenye mtandao wa masuala ya kiuchumi, pamoja na  makubalino mengine yaliyolenga kwenye utunzaji wa kanuni msingi muhimu kwa ajili ya maisha ya kanisa na shughuli zake katika mataifa mbalimbali,  kama ilivyoridhiwa pia mjini Dili, Jamhuri ya Timor,  na pia huko Chad,  Palestina na Kuwait , ambako kati ya mengine, kumeonyesha inawezekana  kudumisha  amani  kati ya wafuasi wa imani mbalimbali za kidini.Lakini katika iwapotu  uhuru wa kidini utatambuliwa na kujengwa mshikamano katika utendaji kwa ajili ya manufaa ya wote, kupitia uwepo wa  roho ya kuheshimu utambulisho wa dini zote.

Kwa mtazamo huo, Papa alimewakumbusha Mabalozi kwamba, kila tendo la kweli la kidini hukuza amani.  Maelezo ya Papa yalirejea ukuu wa sherehe za siku hizi za mwisho wa mwaka, hasa  Sikukuu ya Kuzaliwa Mkombozi wa Dunia, Bwana wa Amani, akisema, ni  tukio linalokumbusha kwamba,  licha ya Ukuu wake, Mungu Mwenyezi ,  Baba wa Milele na Mfalme wa Amani, anazaliwa kama mtoto wa kawaida kati ya watu, anazaliwa katika mazingira duni,  ili kila binadamu apate  kuiona sura ya halisi wa Mungu, kwamba yeye Mungu ni Upendo,  na ni  mnyenyekevu, asiyetumia mamlaka, wala mabavu au uharibifu,  lakini ni upendo mwenye kutawala kwa haki  na si kwa  kisasi, Yeye ni Mungu wa huruma.

Katika mwanga huo, Papa alirejesha mawazo ya Mabalozi ,  kwa nini alipenda kutangaza  mwaka huu kuwa Mwaka Mtakatifu wa Jubilee maalum ya Huruma ya Mungu, Jubilee aliyoizindua kwa namna ya kipekee,  akiwa Bangui Jamhuri ya Afrika, wakati wa Ziara yake ya Kitume, ya  kutembelea mataifa Matatu ya Afrika- Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika Kati.  Papa aliendelea kufanya rejea katika hotuba yake ya Bangui ambako alikemea utumiaji wa jina la Mungu kufanya ghasia au mauaji, akisema ni itikadi potofu kutumia jina la Mungu kuua watu wasiokuwa na hatia, kama inavyofanywa sasa na mashambulizi mengi ya kigaidi, huko Afrika , Ulaya na Mashariki ya kati .

Hotuba ya Papa kwa Mabalozi iliendelea kurejea pia ziara zingine alizozifanya mwaka uliopita ambamo  alitembelea mji wa Sarajevo,  kwa nia ya kutoa ujumbe wa kujenga madaraja ya amani kati ya mataifa na dini, akihimiza umoja, ushirikiano na kuheshimiana kama vipengere muhimu katika maisha ya jamii kwa manufaa ya watu wote. Ameasa kwamba, ujenzi wa madaraja kati ya mataifa na dini  inawezekana tu  kupitia uaminifu katika majadiliano yenye kuheshimu tunu za utamaduni wa kila mmoja na katika kukubali mema yote yatokanayo na uzoefu wa wote.  Papa alieleza bila kusahau kutaja ziara nyingine aliyofanya huko Bolivia, Ecuador na Paraguay , Cuba na Marekani, ambako aliweza kuhudhuria pia Mkutano wa Dunia wa Familia , na tukio la Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu, iliyolenga zaidi katika kutazama changamo za Kanisa katika maisha ya familia na jamii kwa ujumla.

Aidha Papa amewaangalisha Mabalozi katika kipeo cha uhamiaji na wakimbizi , watu wanaolazimika kuacha nchi yao na mali yao kutokana na madhulumu yaliyoko mbele yao.  Papa amewatia  moyo Mabalozi kwamba hakuna sababu za kutishwa na vipeo hivyo,  kwa kuwa Mungu yu pamoja na  watu wake kila mahali, kama inavyodhirishwa katika Maandiko Matakatifu.

Papa aliendelea kuweka bayana baadhi ya sababu zinazokuza wimbi hili la uhamiaji, akionyesha kujali ucheleweshwaji wa majawabu yanayoweza kupunguza kasi ya wahamaiji na wakimbizi,kwamba, sababu hizo zingekuwa zimepata ufumbuzi siku nyingi za nyuma, kabla haijachelewa mno, hadi kuwepo maafa mengi yanaweza kuzuiwa na badala yake kuwepo juhudi za kujenga amani.  Maelezo ya Papa yalirejea katika tabia na mazoea yenye kukumbatia ubinafsi hasa katika mifumo mbalimbali ya kijamii, yenye kushinikiza ghasia na uharibifu usiokuwa na manufaa kwa yoyote, akitoa mfano wa uwepo wa mfumo mbovu wa biashara za silaha, teknolojia na  sera za kifedha mbovu kwa kisingizio cha maendeleo vyenye kukuza ubadhuilifu  rushwa na magendo.

Amehimiza mipango yote kitaifa na kimataifa ni lazima kuzingatia utoaji wa msaada wa kuonekana kwa wakimbizi , pamoja na uboreshaji wa maendeleo na maisha katika nchi wanakotoka, hasa uwepo wa sera zenye kuvuvia umoja na ushirikiano katika nchi wanakotoka au katika nchi wanakokimbilia. Na pia alitazama suala ya ubabe wa kidini na ugaidi unaofanywa kwa kisingizio cha kutunza kanuni za kidini. Na wakati huohuo akaonyesha mtazamo chanya kwa wimbi la uhamiaji akisema , linazua hoja muhimu ya kutafuta jawabu linalofaa kutatua  changamoto zinazojitokeza. Na metaja moyo wa kuwapokea na kuwakubali  wageni, kwamba inakuwa ni nafasi nzuri inayoweza kuleta maridhiano mapya na mitazamo mipana zaidi kwa pande zote husika, kuwajibika kwa  kuheshimu utamaduni na sheria za jumuiya husika na pia katika kuuona mchango mzuri unaoweza kutolewa na wageni katika jamii wanaoyohamia kwa ujumla.

Kwa mtazamo huo,  Papa amerudia kutaja  jukumu la Jimbo la Papa,  katika ujenzi wa mahusiano ya kiekemene  na kati ya dini kupitia  njia za mazungumzano  katika hali za kuheshimu utambulisho wa kila mmoja kwa ajili ya ukuzaji wa maelewano na umoja kati ya watu wa tamaduni na jamii mbalimbali.

Papa ameonyesha matumaini yake kwamba, mizozo iliyojitokeza inakuwa ni nafasi ya kuinua saiti zaidi kwa ajili ya ujenzi wa amani na utayari wa kufikia muafaka.  Papa ameeleza na kutoa mfano wa mafanikio yaliyoonekana  katika Uchaguzi wa ksiasa katika  Jamhuri wa Afrika Kati , akisema ni ishara nzuri ya kutembea pamoja kwa ajili ya kufika katika  umoja kamili wa kitaifa. Na pia ametaja kile kinachoendelea huko Cyprus na Colombia ,  pia  Syria na Iraki, akitoa wito kwa watu wawe jasiri, waachane na ghasia badala yake warejeshe moyo wa mapatano na umoja kwa manufaa ya taifa lao na dunia kwa ujumla.

Papa ameomba mwaka huu 2016 na uwe mwaka wa majadiliano na maridhiano, kwa ajiliya kuimarisha yaliyo mema kwa wote, hasa katika mataifa yanayopambana na migawanyiko ya kisiasa kama ilivyo katika  mataifa ya Burundi, DRC, na Sudan Kusini , pia huko Ukraine. Wakati huohuo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa,nchi binafsi na mashirika ya misaada ya kibinadamu,  kujitoekeza kwa wema zaidi , kusaidia mataifa hayo yaliyozingirwa na mizozo na ghasia.

Amewaambia Mabalozi kwamba, kw awakati huu changamoto kubwa iliyoko mbele yao, ni jinsi ya kushinda tofauti zilizoko na kufanyakazi kwa ushirikiano kwa ajili ya kujenga amani na mema kwa watu wote. Aidha amewahakikishi kwamba, anasali ili kwamba,  mwaka huu mpya,  uweze kuponya makovu makubwa yenye kutenganisha nchi ya  Israel na Palestina .

Na kwamba , Jimbo Takatifu  litaendelea kupaza sauti yake kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa amani katika mipaka yote ya dunia. Na hivyo Sekretariat ya Nchi ya Vatican , iko tayari kushirikiana na kila Balozi, katika ufanikishaji wa majadiliano kati ya Jimbo Takatifu na nchi wanazowakilisha , kwa manufaa ya familia nzima za binadamu. Na kwamba Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya Huruma ya Mungu alioutaja kuwa ni zawadi muhimu kutoka kwa Mungu, na uweze kubadli hofu na mashaka yote, kuwa upendo na amani.  Kwa maoni hayo Papa alirudia kutoa baraka zake kwa Mabalozi na familia zao na nchi wanazoziwakilisha hapa mjini Vatican.

  

 








All the contents on this site are copyrighted ©.