2016-01-11 07:08:00

Mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu tuendelee kuyatia fukuto maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kwa kujaribu kudadafua tunu tunazoshirikishwa na watawa wa mashirika mbalimbali. Kama tulivyokwisha kusikia, utawa ni wito mtakatifu, ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuita watu kuyaishi maisha ya kitawa. Na hao walioitika kweli, wanajitoa kikamilifu kwa Mungu kwa njia ya nadhiri, ahadi au aina nyingine ya vifungo vitakatifu ili waweze kumtumikia Mungu ndani ya Kanisa, huku wakiimwilisha Injili ya Kristo kwa kuyaishi mashauri ya Injili.

Lakini ni muhimu sana kujua kwamba, pamoja na kujitoa kwa Mungu kwa njia ya vifungo hivyo, watawa bado wanawiwa kujishikamanisha na Mungu kwa njia ya sala, sadaka na majitoleo mbalimbali; huku daima wakitegemea msaada na neema za Mungu. Wao wenyewe hujiombea kila siku, huliombea Kanisa na Ulimwengu mzima. Hivyo, maisha ya watawa hawa tunaowaona, yanaambatwa na utume wa sala kila siku ya maisha yao. Wanamsifu Mungu kwa mawazo yao, vinywa vyao, kazi zao na maisha yao yote. Na hapo ndipo penye siri ya utamu wa maisha ya kitawa.

Pamoja na yote wanayoyatenda, mmoja ya zawadi kubwa sana wanayotupatia watawa ni kutuombea daima kwa Mungu. Na hawa watawa wanaomfuasa Kristo fukara, msafi wa moyo na mtii, nao pia ni fukara kama Kristo, wasafi na watii. Sisi tunaweza kuwaomba msaada wa sala tu, huku nasi tukijibidisha kuwasindikiza kwa sala zetu za kila siku, ili neema ya Mungu iwasindikize katika maisha na utume wao, ili yule mwovu asiwaweze.

Daima mwovu anataka kuchafua kazi ya watawa. Mwovu anajua kabisa kuwa watawa ni maua ya Kanisa, wanaleta uzuri katika Kazi ya Mungu. Hivyo mwovu kwa visa vyake anadumu kuwasumbuasumbua na kuwababaisha. Ni mwito kwetu sote: kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Utawa na watawa na kuwaombea watawa wetu wadumu katika wito wao mtakatifu.

Katika kipindi kilichopita, tuliujiuliza swali la msingi kwamba “Katika maadhimisho ya mwaka huu wa watawa, sisi tusio watawa tunajifunza nini”? Au kwa maneno mengine “watawa wanatuambia nini kwa mfumo wa maisha na utumishi wao”? Tulijaribu kuona baadhi ya tunu ambazo kwa macho wazi twaweza kuzijifunza kutoka kwa watawa na utumishi wao.

Leo mpendwa msikilizaji, tuendelee kulijibu swali lile lile kwa kujaribu kuona kaulimbiu za mashirika mbalimbali ya kitawa kadiri zilivyotolewa na waanzilishi wao au zilivyotoholewa katika safari ya maisha na utumishi wao.

Kwanza kabisa tuwaone watawa wa Mtakatifu Augostino: hawa wanajulikana kama Waagustiniani. Ni shirika la kitawa lililoanzishwa na Mtakatifu Augostino Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Kaulimbiu yao kwa lugha ya kilatini ni “Anima una et cor unum in Deum”, yaani Roho mmoja na moyo mmoja katika Mungu.

Ni kauli mbiu inayotualika kujenga umoja  kati yetu. Ni kauli mbiu inayopinga kila aina ya migawanyiko, ubaguzi na minyanyapaano ya kila sampuli. Kwa kujua kuwa sote tumeumbwa na Mungu yuleyule aliye Baba wa wote; tunapaswa katika yeye huyohuyo, kuwa na roho mmoja na moyo mmoja. Waagostiniani wanaimwilisha kauli mbiu yao hiyo katika shughuli za kichungaji sehemu mbalimbali za mission, kuyaambata maisha ya kitaaluma kwa kuleta mwanga wa elimu kwa watu.

Pili, tuwatazame ndugu zetu Wabenediktini: hawa ni watawa walioanzishwa na Mtakatifu Benedikto kunako karne ya 6. Wao huishi kwa kufuata Kanuni na tasaufi ya Mtakatifu Benedikto kama inavyojieleza katika Kanuni yake kwa Wamonaki. Kadiri ya mapokeo ya zamani sana, Kauli mbiu ya Wabenediktini ni ”Ora et Labora” yaani Sala na Kazi.  Kutokana na mageuzi na maboresho ya kihistoria, kumetokea matawi mbalimbali ndani ya Utawa wa Mtakatifu Benedikto, ndiyo maana tuona katika nyakati zetu hizi kuna matawi mengi ndani ya Familia ya Kibenediktini. Huo muungano wa Familia ya Kibenediktini ukajiongezea kauli mbiu ya ”Pax”, kama mchocheo wa wito na utume wao ndani ya Kanisa na kwa ulimwengu.  Hivyo kwa sasa kaulimbiu ya Watawa Wabenediktini inasimama kama ”Pax, Ora et Labora”.

Hakika, katika ulimwengu wetu huu ambao unaloweshwa damu kila kukicha, tunataka amani. Katika familia zetu ambazo zimejaa kila aina ya hasira, kisirani na visasi, tunataka amani, katika maisha yetu ambamo watu tumejaa roho mbaya, uchokozi na virusi vya vurugu, tunataka amani! Katika maisha yetu yaliyojaa kujichanganya na kuchanganyikiwa, kunakotokana na tamaa ya sifa, umaarufu, mali na madaraka hadi tunachuruzisha damu za watu; tunataka amani!! ”Pax in terris”!, Amani Duniani.

Lakini tukumbuke kwamba, amani ni tunda la Roho Mtakatifu, na amani huanzia katika mioyo yetu, nayo ni dhana ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuijenga kichwani na kuamua kuwa chombo cha amani. Nayo amani hutafutwa kwa bidii, hulindwa na huchochewa kwa maneno na matendo ya kila siku.

Na zaidi ya amani, Wabenediktini wanatufundisha kupenda kufanya kazi. Wanatualika kuungana kupinga kabisa tabia ya uvivu na kula vya bure; au tabia ya kujilemaza na kupenda kusaidiwa tu maisha yote. Tangu mwanzo wa ulimwengu, sote tulialikwa kufanya kazi, maandiko matakatifu yanatuhimiza kufanya kazi, ili tujipatie mkate wetu wa kila siku, na kwa mkate huohuo tuwasaidie na wengine, wenye kuhitaji zaidi. Lakini tufanye yote hayo, kwa nguvu ya Mungu, huku sala ikipewa nafasi ya kwanza kabisa.

Tatu, tuwaone ndugu zetu Wadominikani: Hawa ni watawa wanaoishi Roho ya Mtakatifu Dominiko. Ni Shirika linalojihusisha zaidi na kuhubiri Neno la Mungu na ndiyo maana wanaitwa Shirika la wahubiri. Kauli mbiu yao kwa lugha ya kilatini ni “Laudare, Benedicere, Praedicare”, yaani kusifu, kubariki na kuhubiri. Mtakatifu Dominiko alianzisha shirika hili ili kuhubiri kwa nguvu zaidi Neno la Mungu kama namna ya kusahihisha uzui na upotoshwaji unaotolewa na wapinga Kristo na Kanisa lake. Na kwa sababu hiyo Wadominikani wanakazia zaidi maisha ya kitaaluma. Wakishakuelimishwa sawasawa katika elimu ya Mungu na elimu-dunia, huku wakijisimika katika imani ya kweli katika Mungu, ndipo wanakuwa wahubiri wa kweli. Nasi wanatupatia mchocheo huo huo, ili tujitoe kutangaza neno la Mungu kwa bidii timilifu, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda. Uinjilishaji ni jukumu la kila mbatizwa ndani ya Kanisa. Tupende kuyasoma na kuyajifunza Maandiko Matakatifu na kutangaza ujumbe wa wokovu kwa watu wote. Tusilale wala kuzubaa!! Yule mwovu anayeliharibu Kanisa halali usingizi. Tulinde imani yetu kwa kufundisha ukweli na kuiambata imani yenyewe.

Nne, tuwaone ndugu zetu Wafranciskani: hawa ni watawa wanaofuata mafundisho na nidhamu ya kiroho kama alivyofundisha na kuishi Mtakatifu Francisko. Mtakatifu Francisko alijiambua na malimwengu, kwa kuacha mali na malimbwende ya dunia,  na akaamua kumfuasa Kristo katika ufukara mtimilifu. Leo hii kuna familia kubwa sana ya Wafransiskani sehemu anuai duniani. Kauli mbiu yao kwa lugha ya kilatini ni “Pax et Bonum”, yaani Amani na Wema, kaulimbiu inayotualika kutenda yote kwa amani na wema. Pamoja nalo, ndugu hawa wanatufikirisha juu ya hali halisi ya sisi walimwengu wa leo, wapenda mali na umaridadi hata kwa gharama za vichwa vya watu. Wangapi tunawaona wanajilundikia mali, lakini wanakosa amani, na wanakosa hata usingizi? Ukitaka amani katika maisha yako, ebu jaribu kurekebisha mahusiano yako na mali.

Tano na mwisho kwa leo, tuwaone ndugu zetu Wajesuiti. Hili ni Shirika lililoanzishwa na Mtakatifu Ignasi wa Loyola, kwa lengo la kutetea na na kulinda Haki za Baba Mtakatifu na uthabiti wa Kanisa takatifu la Mungu. Kauli mbiu yao kwa lugha ya kilatini ni “Ad Maiorem Dei Gloriam inque Hominum Salutem”, yaani Kwa ajili ya utukufu mkuu wa Mungu na kwa wokovu wa watu. Kwa mantiki hiyo Wajesuiti nao huyaambata maisha ya kitaaluma kwa kiwango cha juu sana ili kuweza kushiriki vema katika utume wao na kusaidia katika mchakato wa kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili. Hawa wanatualia nasi, kujibisha kutenda mambo yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu. Yale yote ambayo hayampi Mungu utukufu na yanakwamisha wokovu wa mwanadamu, ni sherti tuyakwepe. Hamu ya moyo wa kila mkristo na kila binadamu aliyeumbwa na Mungu, iwe ni kumpa Mungu utukufu katika mambo yote.

Basi mpendwa msikilizaji, kwa vile muda si rafiki, kwa siku ya leo tunaahirisha mada yetu hadi wakati mwingine tena. Kukuletea makala hii kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mmi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.