2016-01-10 11:37:00

Sikilizeni na kujibu kilio cha amani huko Syria!


Bwana Michel Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Caritas Internationalis inasikitika kusema kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ya vita na kinzani za kijamii nchini Syria, kuna maelfu ya watu wampoteza maisha yao; mamillioni ya watu yamelazimika kuikimbia nchi yao na kwa sasa wanaishi katika mazingira hatarishi kwa maisha na ustawi wao wa siku za usoni.

Mwaka 2016 unapaswa kuleta mabadiliko kwa Syria kuachana na vita na kuanza kuambata misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Taarifa zinaonesha kwamba, kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha kutoka na baa la njaa na utupu huko Syria, kiasi kwamba, Umoja wa Mataifa umeamua kuanzisha mchakato wa msaada wa dharura kwa maelfu ya watu hawa. Katika kipindi cha miezi kumi na miwili kuanzia sasa, Caritas Internationalis inataka kuendesha kampeni inayopania kujenga na kudumisha misingi ya amani nchini Syria kwa kuwahusisha wadau mbali mbali.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na wajumbe wa Caritas Internationalis kutoka Ukanda wa Mashariki ya Kati, wanaowahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria. Watu wanataka kuona msingi wa amani ukijengwa na kudumishwa kwani hii ndiyo kiu yao kwa wakati huu na wala hawahitaji jambo jingile lolote lile! Kutokana na ombi la kilio la amani huko Mashariki ya Kati, Caritas Internatuionalis imeamua kukivalia njuga kilio hiki hadi pale amani itakapopatikana huko Syria.

Lengo ni kutaka kuwahusisha wadau mbali mbali ili kuondokana na hali ya kutojali na kwamba, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee ili amani, utilivu na maridhiano yaweze kufikiwa kwa njia ya majadiliano na wala si kwa mtutu wa bunduki ambao kwa miaka mitano umeshindwa kutoa jibu muafaka kwa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Syria. Katika medani za kisiasa, Caritas Internationalis inawataka wakuu wa Serikali kuguswa na mahangaiko ya raia wao, tayari kuanza mchakato wa kuandika ukurasa mpya wa amani.

Caritas Internationalis inakaza kusema, watu wameanza kuzoea kusikia vita kiasi kwamba, leo hii Syria si sehemu ya habari za kimataifa hata kama kuna mamillioni ya watu wanaendelea kuteseka. Darfur, Sudan imesahaulika kwa wakati huu baada ya miaka kumi na miwili ya vita na mipasuko ya kijamii. Haya ni maeneo ya vita ambayo yamekuwa ni soko kubwa kwa mataifa na mashirika ya kimataifa yanayozalisha na kuuza silaha kiasi cha kusahau kwamba, fedha wanayovuna kutoka Syria na Darfur, Sudan inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Umoja wa Ulaya umechukua mwelekeo na sera mpya kuhusu wahamiaji na wakimbizi, baada ya kuona wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji hifadhi na usalama wa maisha likibisha hodi Barani Ulaya. Caritas Internationalis inawaalika wadau mbali mbali kuendelea kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kufungua nyoyo na akili za wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ili haki, amani na maridhiano viweze kupatikana huko Syria. Jambo la pili ni kuitaka Jumuiya ya Kimataifa na Makampuni ya Kimataifa kutofanya biashara ya silaha na Syria, ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Tatu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka Syria wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa pia kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa wananchi wa Syria. Bado kuna wakimbizi na wahamiaji wengi wanaohudumiwa huko Yordani, Uturuki, Lebanon na Iraq, hawa wasisahauliwe na Jumuiya ya Kimataifa, vinginevyo watakufa kwa baridi na njaa kali. Watu millioni nne wako kwenye hatari na wasi wasi wa kukumbana na maafa wakati wowote. Watu hawa wanapaswa kusaidiwa kwa hali na mali kwani peke yao hawawezi kumudu kishindo cha gharama ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.