2016-01-09 11:17:00

Tanzania na Finland kuendelea kushirikiana kwa Finland kuwekeza zaidi!


Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa siku ya Ijumaa tarehe 8 Januari 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Bwana Pekka Hukka. Akizungumza na Balozi Hukka, alipomtembelea ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo kwa namna ambavyo nchi ya Finland imeendelea kuisaidia Tanzania na kumwomba waendeleze uhusiano mwema uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

“Ninashukuru na kutambua mchango wa nchi yako wa kuisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali ikwemo Utalii na Biashara, ninashukuru sana kwa hilo” alisema Waziri Mkuu Majaliwa. Pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Finland kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda na kuendeleza maeneo ya ukanda maalum wa uwekezaji (EPZ) ili kuongeza thamani ya mazao pamoja na kutatua tatizo la ajira nchini.

Waziri Mkuu, pia ameendelea kwa kusema Serikali imedhamiria kukusanya mapato kikamilifu na kuzuia mianya ya upotevu wake, hivyo ameiomba Serikali ya Finland isaidie katika kujenga uwezo wa namna bora zaidi ya utekelezaji wa dhamira hiyo, kwa kuwa Finland ni kati ya nchi zenye mifumo bora na madhubuti ya ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake, Balozi Hukka amesema nchi yake kupitia Balozi za Tanzania na Finland zimeanza jitihada za kuandaa utaratibu kwa ajili ya kuwekeza nchini Tanzania na kuna baadhi ya makampuni ambayo yako tayari nchini Tanzania katika mchakato wa kuwekeza vitega uchumi katika sekta mbali mbali za uzalishaji na utoaji huduma.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Namibia ambaye anamaliza muda wake,nchini Tanzania Bwana Japhet Isaack. Akizungumza na Balozi Isaack, ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es salaa, Waziri Mkuu ameshukuru Balozi huyo na kumumwomba waendeleze uhusiano mwema ulipo baina ya nchi hizi mbili ambao ulianza tangu enzi za kupigania uhuru ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizi mbili.

“Namibia ni nchi yenye uchumi unaokua haraka, na mmefanikia katika baadhi ya sekta , hivyo ningependa Tanzania ijufunze kutoka kwenu hasa katika sekta za Utalii, Afya, na Elimu,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa. Pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha raia wa Namibia kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwanda na kuendeleza maeneo ya ukanda maalum ya uwekezaji (EPZ) ili kuongeza thamani ya mazao pamoja na kutatua tatizo la ajira nchini.

Kwa upande wake, Balozi Isaack amesema kwa kipindi alichokaa Tanzania amejifunza mengi, na amefurahishwa ambavyo Waziri Mkuu pamoja Serikali kwa ujumla inavyofanyakazi kwa kasi na kwa mafanikio makubwa. “Hongera, ninafurahishwa na unavyofanya kazi hongera sana”, alisema Balozi Isack. Pia, amefurahi sana kipindi chote alichokaa Tanzania kwani kimekuwa na matukio mengi yenye kumbukumbu nzuri kwake. Balozi Isack ameomba mahusiano ya nchi hizi mbili yaendelezwe ili zishirikiane zaidi katika masuala mbalimbali ya kukuza uchumi.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri mkuu, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.