2016-01-08 15:25:00

Wamissionari wa huruma ya Mungu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, limeadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana kwa kuwakumbusha waamini kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wamejitwalia wajibu unaowashirikisha: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo, kumbe, wote wanatumwa kutoka kimasomaso ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwani wao pia ni Wamissionari wa huruma ya Mungu. Sadaka na michango mbali mbali iliyotolewa na waamini imepelekwa kutunisha mfuko wa kimissionari wa kitaifa.

Waamini licha ya kuchangia kwa hali na mali, lakini pia wanakumbushwa kuendelea kusali ili mchakato wa Uinjilishaji mpya uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa watu kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kumpokea Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mkombozi wao. Bado kuna umati mkubwa wa watu ambao haujapata nafasi ya kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu anasema Askofu Jerzy Mazur, Mwenyekiti wa Tume ya Utume wa Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland.

Maaskofu kutoka Poland wanasema kwamba, kuna zaidi ya Wamissionari 2, 040 kutoka Poland wanaoishi na kutekeleza dhamana na wajibu wao kimissionari katika nchi 97. Kwa sasa kuna mihimili 29 ya Injili inayojiandaa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia. Wamissionari hawa wanatumwa kuinjilisha, lakini zaidi kwa kutoa ushuhuda wa Injili ya furaha inayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili watu wanapoyaona waweze kuguswa na kuvutwa zaidi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linakaza kusema,  Wamissionari ni kama nyota angavu ya Noeli wanaoangaza na kuganga umaskini, magonjwa na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika maisha yake. Wamissionari hawa wako tayari kuwaonesha jirani zao mwanga wa Injili ya Kristo, tayari kuukumbatia na kuuambata katika safari ya maisha yao ya kiroho. Maaskofu wanawashukuru waamini kwa kuendelea kuwaenzi Wamissionari wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya sala na sadaka zao.

Itakumbukwa kwamba, kuna Wamissionari 819 kutoka Poland wanaotekeleza dhamana na utume wao Barani Afrika; wengine 797 wako Amerika ya Kusini na Wamissionari 336 wako Barani Asia, 60 wametumwa huko Oceania na 20 wako Marekani. Kati ya Wamissionari wote hawa kuna Maaskofu 24, matendo makuu ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.