2016-01-08 09:02:00

Papa Francisko kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 26


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Jumapili tarehe 10 Januari 2016 majira ya Saa 3:30 kwa saa za Ulaya, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 26. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko hapa mjini Vatican.

Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu zinawaingiza waamini katika Jumuiya ya Kikristo, tayari kupokea zawadi ya maisha ya Kimungu ndani mwao, ili kuanza hija inayowapeleka katika utimilifu wa upendo; maisha ya utakatifu pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kielelezo makini cha Uinjilishaji mpya.

Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, ni njia ya utakatifu wa maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu na mlango unaowawezesha waamini kupata Sakramenti nyingine za Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanawekwa huru kutoka katika dhambi ya asili na kuzaliwa upya kama watoto wa Mungu; wanakuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, tayari kushiriki utume na maisha ya Kanisa.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaifia dhambi na kufufuliwa katika maisha mapya, tayari kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka, ili waweze kuwa ni watoto wa nuru! Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko ataendeleza Mapokeo ya kuwabatiza watoto wachanga wakati wa Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, unaowakumbusha Wakristo wote kuambata ahadi zao za Ubatizo na kwamba, wanashiriki pia ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, hasa wakati huu, Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.