2016-01-08 11:34:00

Mungu ni upendo na asili ya upendo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 8 Januari 2016 anasema, Mungu ni upendo na asili ya upendo wote na kwamba, Yeye ndiye anayeanza kupenda kwanza kabla ya mtu awaye yote! Haijalishi ikiwa kama binadamu anaogelea katika dimbwi la dhambi! Mungu ni mwenye huruma na mapendo, mambo ambayo anapenda kumshirikisha binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani kama anavyosimulia Mtakatifu Yohane katika Nyaraka zake, wakati huu wa Kipindi cha Noeli.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amri ya upendo kwa Mungu na jirani ni muhimu sana kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Inapendeza kuona mwamini akijikita katika upendo, unaomwezesha kukua na kukomaa katika kujisadaka na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Neno upendo linaonekana kana kwamba, ni neno la kawaida kabisa katika maisha ya watu wengi. Upendo usipokuwa na mwelekeo sahihi utazimika kama kibatari kwani upendo wa kweli unabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mungu ni upendo!

Mtakatifu Yohane anafafanua kwamba, moja ya sifa za Mungu ni kwamba, Mungu ndiye kielelezo cha upendo, hali inayojionesha katika muujiza wa kugeuza mikate mitano na samaki wawili kwa ajili ya kuulisha umati mkubwa wa watu uliokuwa umekusanyika kwa ajili ya kumsikiliza Yesu akihubiri. Yesu aliwaangalia watu hawa akawaonea huruma na kuamua kuwalisha kwa mikate mitano na samaki wawili ili kuonesha huruma na upendo wa Mungu unavyomwilishwa katika maisha ya watu. Upendo wa Mungu unawashirikisha watu ili kugawana hata kile kidogo walichokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Upendo huu wa Mungu unajionesha katika mifano mingi ya Injili kama ule aliomwonesha Zakayo mtoza ushuru; Natanaeli na Mwana mpotevu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, pale binadamu anapokosa na kutenda dhambi, Mwenyezi Mungu daima anakuwa tayari kumpokea na kumkumbatia, ili kumwonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kipimo. Mwenyezi Mungu anataka kuwahakikishia watoto wake kwamba, anawapenda upeo na kwamba, upendo ndiyo zawadi anayotaka kuwashirikisha. Lakini, jambo la msingi ni kwa mwamini kufungua lango la moyo wake na kutambua kwamba, anastahili kupokea upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Pale waamini wanapoelemewa na dhambi wasione aibu kukimbilia huruma ya Mungu na kumwambia kwamba, wanashindwa kumpenda zaidi kutokana na kusongwa na dhambi zinazochafua upendo wao kwake. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, atawajalia waja wake huruma na msamaha kama alivyofanya kwa Mwana mpotevu alipokimbilia huruma yake, baada ya kutafuna fedha na mali ya Baba yake na makahaba. Waamini wanahamasishwa kukumbatia upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.