2016-01-08 15:02:00

Familia za Kikristo zinahamasishwa kuwa ni vitalu vya miito mitakatifu


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa apoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, anamshukuru Mungu kwa familia nyingi kuendelea bado kuwa kweli ni chemchemi na vitalu vya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya.

Askofu mkuu Rugambwa, anaendelea kuwahimiza wazazi na walezi kuwaelekeza vijana kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao kwa njia ya maisha ya kitawa na kipadre. Anatambua kwamba, vijana wana uhuru na maamuzi yao ya maisha, lakini wazazi na walezi wawasaidie vijana kuwa na mang’amuzi sahihi kuhusu wito na maisha yao, kwa kutambua kwamba, inalipa pia hata katika wito wa kitawa na kipadre, kwani hapa wanajisadaka kwa ajili ya mambo matakatifu kwa ajili ya Mungu na jirani zao.

Familia ya Mungu inapaswa kutambua kwamba, miito inazaliwa, inakuzwa na kudumishwa katika Jumuiya ya waamini, kumbe malezi ya awali na endelevu ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa ni Jukumu la familia, vyama vya kitume na waamini katika ujumla wao. Kila mtu atambue dhamana na wajibu huu na kuutekeleza kwa ari na moyo mnyofu, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda na unyofu wa maisha. Vijana wengi wanavutwa kwa mifano bora ya maisha kuliko hata maneno.

Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Protase Rugambwa anawapongeza watawa wa Mashirika mbali mbali ndani ya Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, unaotarajiwa kuhitimishwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Anawaalika viongozi mbali mbali wa Kanisa kuonesha umoja, ushirikiano na mshikamano wa dhati na watawa, ili kwa pamoja waweze kuchangia katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa njia ya karama na mapaji mbali mbali ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kuzingatia wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, watawa wanaendelea kuhimizwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wanaowahudumia katika medani mbali mbali za maisha, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kukombolewa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.