2016-01-08 09:27:00

Familia ya Mungu Uganda inaomboleza kifo cha Askofu mstaafu 'Imana wa Kabale


Askofu mstaafu Barnabas R. Halem ‘Imana wa Jimbo Katoliki Kabale, Uganda amefariki dunia hapo tarehe 3 Januari 2016, akiwa Jijini Kampala. Marehemu Askofu ‘Imana alizaliwa kunako mwaka 1927, huko Rulangara, Busanza, Wilayani Kisoro, Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Desemba 1958 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Tarehe 29 Mei 1969 akateuliwa na Mwenyeheri Paulo VI kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Kabale, Uganda, lililokuwa limeanzishwa miaka mitatu iliyokuwa imepita chini ya Usimamizi wa kitume wa Hayati Askofu Gervas Nkalanga, aliyefariki dunia hivi karibuni, akiwa ni mtawa wa Shirika la Wabenediktini, Hanga Jimbo kuu la Songea, Tanzania. Askofu Barnabas Halem ‘Imana aliwekwa wakfu tarehe 1 Agosti 1969 na Mwenyeheri Paulo VI wakati wa hija yake ya kwanza kabisa Barani Afrika.

Baada ya kuwaongoza Watu wa Mungu, huku akiwafundisha na kuwatakatifuza kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, hapo tarehe 15 Julai 1995 akang’tuka kutoka madarakani. Marehemu Askofu Barnabas R. Halem ‘Imana amezikwa tarehe 5 Januari 2016 katika Ibada iliyoongozwa na Kardinali Emmanuel Wamala, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda na tarehe 6 Januari 2016, Marehemu Askofu mstaafu Barnabas R. Halem ‘Imana wa Jimbo Katoliki Kabale, Uganda akazikwa Jimboni mwake Kabale. RIP.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.