2016-01-07 08:37:00

Ujumbe wa Noeli kutoka kwa Patriaki Cyril kwa Mwaka 2016


Waamini wa Kanisa la Kiorthodox wanaadhimisha Siku kuu ya Noeli tarehe 7 Januari 2016 kadiri ya Kalenda ya Juliani. Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Russia katika ujumbe wake wa Noeli anawaalika Wakristo nchini Ukraine kushikamana katika upendo na huruma na kamwe wasitumbukie kwenye kishawishi cha chuki na uhasama kilichosababishwa na machafuko ya kisiasa yaliyopelekea vita, mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia nchini Ukraine. Waamini waoneshe moyo wa huruma, upendo na msamaha, tayari kushirikiana na wote kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao unaojikita katika umoja na mshikamano wa kitaifa.

Patriaki Cyril anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Ukrain kusali ili kuombea amani na maridhiano kati ya watu kwa kutambua kwamba, Ukraine inaundwa na kujengwa na watu kutoka katika makabila, dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, kumbe, tofauti hizi msingi zinapaswa kuchukuliwa kuwa kama utajiri mkubwa unaowasukuma kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi na maendeleo ya wengi badala ya kuwa ni chanzo cha kinzani na mpasuko wa kijamii.

Patriaki Cyril anasema, umefika wakati kwa Ukaraine kuganga na kuponya madonda ya chuki, uhasama na utengano ambayo yamegusa akili, nyoyo na miili ya watu. Waamini wajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia ujasiri kwa kuanza ukurasa mpya katika maisha yao badala ya kuendelea kusikiliza mtutu wa bunduki unaopandikiza utamaduni wa kifo na uhasama kati ya watu. Waamini wanahimizwa kumwilisha Injili ya upendo katika maisha yao kwa kuwapenda hata maadui zao kama anavyofundisha Kristo mwenyewe. Wawe na ujasiri hata wa kuwaombea na kuwasamehe adui zao, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja aliye mbinguni anayewanyeeshea na kuwangazia jua; wema na wabaya.

Patriaki Cyril anakaza kusema, maneno haya ya Injili yawasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na chuki pamoja na hali ya kutaka kulipiza kisasi, tayari kusafisha akili na moyo, kuweza kukumbatia amani, utulivu, msamaha na maridhiano kati ya watu. Mwenyezi Mungu daima yuko kati ya watu wake, kumbe hawana sababu ya kuogopa pamoja na kuwa na wasi wasi. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya maisha mapya na matumaini; mwanga na dira kwa wote wanaotembea katika mapito yake. Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwavusha waja wake wanaokumbana na vizingiti vinavyowekwa mbele yao kutokana na dhambi za binadamu.

Itakumbukwa kwamba, tarehe Mosi, Januari 2016 kumefanyika maandamano makubwa amani huko Kiev, Ukraine, yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye Makao yake makuu mjini Roma kwa kushirikiana na Kanisa mahalia. Tukio hili limehudhuriwa na waamini wengi pamona na watu wenye mapenzi mema wanaotaka kuona msingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ikitawala akili na mioyo ya watu nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.