2016-01-07 15:54:00

Ndoto ya Mtakatifu Gaspar inaendelea nchini Tanzania!


Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, tarehe 5 Januari limepata wanashirika wapya watatu ambao ni John Furaha Henjewele, Marco Rafael Loth pamoja na Stephano Furaha Karabyo, ambao wamepokelewa rasmi Shirikani na Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Kanda, Shirika la Damu Azizi ya Yesu Tanzania. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu, Jimbo kuu la Dodoma. Wakati wa Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Wanashirika hawa watatu walipewa Daraja Takatifu la Ushemasi wa mpito katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu na kuhudhuriwa na familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma.

Itakumbukwa kwamba, Mashemasi hawa wapya ni matunda ya kwanza ya Kanda ya Tanzania, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, iliyozinduliwa, Mwezi Agosti 2015 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na Mtakatifu Gaspar del Bufalo! Wamissionari hawa wanasema, kwa hakika ndoto ya Mtakatifu Gaspar, inaendelea Barani Afrika!

Pamoja na mambo mengine, Askofu Mkuu Beatusi Kinyaiya wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuweza kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa darasa la awali hadi kidato cha nne bila kulipa karo. Hayo ameyabainisha wakati wa ibada ya kutoa sakramenti ya daraja takatifu la ushemasi kwa mafrateri watatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania ibada iliyofanyika katika kanisa la Bikira Mama wa Damu Azizi ya Yesu Kisasa Medelii.

Askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa Rais Magufuli ni Rais wa Tatu kwa nchi za Afrika kuweza kufanikisha kutoa elimu bure ambapo nchi ya kwanza kutekeleza utoaji wa elimu bure ni Botwsana, Nigeria na nchi ya tatu inakuwa ni Tanzania. Hata hivyo katika mahubiri yake hayo amewataka mafrateri hao ambao wamepewa daraja takatifu la ushemasi wa mpito kuwa Mabalozi hodari wa kuwasaidia wazazi mahalia pale wanapofanya utume wao, kuwaelimisha na kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao shule kwa ajili ya kupata elimu, kwani elimu ndio ufunguo wao wa maisha ya baadae.

Askofu Mkuu Kinyaiaya katika hatua nyingine ameitaka serikali ya awamu ya tano kutekeleza makubaliano ambayo watakuwa wameyafikia kuhusu utoaji wa huduma za afya kwa wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amesema kuwa hapo awali walikubaliana kushirikiana na Kanisa katika sekta ya afya kwa serikali kutoa watabibu pamoja na vifaa tiba pamoja na kuwalipa mishahara waganga huku taasisi zisizo za kiserikali kutoa vituo vyao vya afya kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye umri kuanzia miaka sifuri hadi miaka mitano pamoja na wanawake wajawazito.

Aidha ameitaka Serikali kuangalia upya suala hilo ili wananchi walipo sehemu mbalimbali ambazo zina upungufu wa huduma hizo za afya waweze kuzipata kupitia vituo vya afya vya taasisi binafsi vilivyopo katika maeneo hayo. Katika hatua nyingine Askofu Mkuu Kinyaiya amewataka watanzanaia kujenga utamaduni wa kujiunga na bima ya afya ili waweze kupata huduma muhimu za afya kwani kwa kujiunga na bima za afya wataweza kujiondoa na kujikomboa na tatizo la kupata huduma za afya muhimu.

Askofu Mkuu Kinyaiya pia amewataka mashemasi wapya ambao wamepewa daraja takatifu siku ambapo Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha sikukuu ya Tokeo la Bwana kwa kutafakari juu ya nafasi na dhamana ya Mamajusii ambao ni Gaspari, Melkiori na Baltazari waige mfano huo kwani wao walikuwa ni watatu na wao walipokea Daraja takatifu ni watatu, wanaowakilisha umoja wa Kanisa na changamoto ya kuutafuta mwanga angavu ambao ni Kristo ili aweze kuwaongoza na kuwasimamia katika maisha, utume na huduma zao kama Mashemasi, wakitambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huduma kwa Kanisa! Ushemasi ni huduma ya upendo kwa Mungu na jirani! Wajitahidi kweli kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu Mkuu Kinyaiya pia amewataka mashemasi hao kuhakikisha kuwa wanafuata nyayo za mwanzilishi wao wa shirika Mtakatifu Gaspari del Buffalo aliyejitoa kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wasiojiweza sanjari na kuyatoa maisha yake katika hali ya ufukara, useja na utii katika Kanisa na kuishi katika maisha adili ndani ya kanisa na jamii iliyokuwa inamzunguka kiasi hata cha kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha. “Mashemasi wapendwa tambueni karama mliyonayo na hakikisheni kuwa wapo wengi walioitwa lakini ni wachache ambao wameitikia sauti ya yesu na kujitokeza hadharani kuitikia sauti hiyo” aliongeza Askofu Mkuu Kinyaiya.

Wakati huo huo, Mashemasi hao walipokelewa shirikani na katika ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa shirika, Kanda ya Tanzania Padre Chesco Peter Msaga. Katika ibada hiyo Padre Msaga aliwataka kujua kuwa wao ni matunda ya wito mtakatifu wa ndoa ya wazazi wao ambao kwa sasa wamewarithisha imani thabiti ya utume mtakatifu. Aliwataka kutambua kuwa wito waliouchagua kuuishi sio wote wanaoufahamu bali ni wachache hivyo kwa ulimwengu wa sasa unayo mambo mengi ukilinganisha na uwepo wa utandawazi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoweza kuwachanganya na kuwakoroga. Alisema msingi wao mkubwa kuishi ni maisha ya Jumuiya chini ya kifungo cha upendo, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu na Utume ambao wanahamasishwa kuhubiri kwa njia ya mifano bora ya maisha yao, hivyo wanapaswa kuhakikisha kuwa maisha yao yanakuwa ni maisha ya useja, ufukara na utii, tayari kutangaza huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Pia Padre Chesco ambaye ni mkuu wa shirika Kanda ya Tanzania aliwaalika waamini kuwaombea vijana hawa ili waweze kujisadaka katika maisha ya kitawa na kipadre. Kwa upande wa wazazi aliwahimiza kumwomba Mwenyezi Mungu achochee miito ndani ya familia mbalimbali ili ziweze kuongeza vijana wenye nia ya kujiunga na miito mitakatifu na kamwe wasiwe ni kikwazo cha watoto wao kutaka kujisadaka katika maisha ya kitawa na kipadre.

Ifuatayo ni historia fupi ya mashemasi wapya wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, ambao kwa sasa wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika huduma ya Neno, Sakramenti kadiri ya Daraja lao, lakini zaidi huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Shemasi John Furaha Henjewele alizaliwa kwa wazazi, John Moses Henjewele na Yusta Thobias Mapunda tarehe 23 Juni 1976 katika Hospitali ya Peramiho. Alikulia katika Parokia ya Litumba, Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma. Alisoma shule ya msingi kuanzia mwaka 1986 – 1992 katika shule ya Litumbandyosi. Elimu ya sekondari ya kawaida aliipata katika shule ya sekondari Ruanda wilayani Mbinga kuanzia mwaka1993–1996. Alichaguliwa kujiunga na kidato cha Tano katika shule ya sekondari Mkwawa mwaka1997 -1999. Mwaka 2000 – 2002 alisomea Stashahada ya Ualimu katika chuo cha Ualimu Mpwapwa mkoani Dodoma. Akiwa mlelewa wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, alitumwa Chuo Kikuu cha Jordani Jimbo Katoliki Morogoro kusoma shahada ya Falsafa kuanzia mwaka 2003 – 2006 na baadaye shahada ya Taalimungu kuanzia mwaka 2011 – 2015.

Shemasi Henjewele alilifahamu Shirika la Wamisionari wa Damu  Azizi ya Yesu kupitia ziara ya Mkurugenzi wa  Miito wakati huo Pd. Chesco Peter Msaga, ambaye kwa sasa ndiye Mkuu wa Shirika Kanda ya Tanzania alipotembelea Shule ya Sekondari ya Mkwawa mwaka 1998. Toka hapo mawasiliano yalianza na hatimaye kuwa mlelewa wa Shirika hili kuanzia mwaka 2002 hadi wakati huu. Alibatizwa tarehe 31 Desemba 1976 katika Parokia ya Mgazini, Jimbo Katoliki la Songea. Alipata Komunyo ya Kwanza mwaka 1988 na Sakramenti ya Kipaimara mwaka 1991 katika Parokia ya Litumba, Jimbo Katoliki la Mbinga.

Alianza Mwaka wa Malezi ya Kwanza Oktoba 2002 hadi Julai 2003. Mwaka wa Malezi ya Pili kuanzia Agosti 2010 hadi Julai 2011 katika nyumba ya malezi ya Mtumishi wa Mungu Yohane Merlini, Miyuji - Dodoma. Tangu Julai 2015 yupo katika mwaka wa kichungaji katika Shule ya Sekondari ya Yohane Merlini chini ya Jumuiya ya Water Project iliyoko Miyuji, Dodoma. Alipewa huduma ya usomaji masomo tarehe 1 Mei 2012 na huduma ya Utumishi altareni tarehe 4 Mei 2013 katika Chuo Kikuu cha Jordani na Askofu Teresphori Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Tarehe 5/ 01/ 2016 amepokelewa  Shirikani rasmi na daima, katika Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na Padre Chesco Peter Msaga mkuu wa Kanda ya Tanzania, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu.

HISTORIA FUPI YA SHEMASI MARCO RAFAEL LOTH: Alizaliwa 27/7/1982 kwa baba Raphael Loth na mama Joyce Daniel, mjini Manyoni Mkoani Singida. Alipata Sakramenti ya Ubatizo 25/12/1982, Komunyo ya Kwanza mwaka 1995 na Kipaimara mwaka 1996 katika Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki Singida. Alisoma Shule ya Msingi Mwembeni iliyoko mjini Manyoni mwaka 1992-1998. Elimu ya Secondari kwa kidato cha I –VI alisoma katika Seminari ya Mt Patrisi Dungunyi, Jimbo Katoliki la Singida mwaka 1999-2005. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro kwa masomo ya Falsafa mwaka 2007-2010 na Taalimungu mwaka 2011-2015.

Alilifahamu Shirika tangu utoto wake kupitia kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu waliofanya na wanaofanya utume katika Parokia ya Manyoni. Mwaka 2006-2007 na 2010-2011 alikwenda nyumba ya malezi ya Mtumishi wa Mungu Yohane Merlini, Miyuji - Dodoma kwa Malezi ya Kwanza na Malezi ya Pili; kwa sasa anafanya mwaka wa kichungaji katika Parokia ya Mkula Jimbo Katoliki la Ifakara. Alipata huduma ya Usomaji 1/5/2012 na huduma ya Utumishi wa Altare 4/5/2013 katika Chuo Kikuu cha Jordani Morogoro na Mhashamu Askofu Teresphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro.  Anawashukuru wote  waliomsindikiza na wanaoendelea kumsindikiza katika safari hii ya wito.

HISTORIA YA SHEMASI STEPHANO FURAHA KARABYO: ni mtoto wa James Matoro na mama Theopista Ndibuzunwaga. Alizaliwa tarehe 17/08/1983 katika Wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza. Tarehe 12/05/1985 alipewa Sakramenti ya Ubatizo, tarehe 21/07/1992 alipokea Komunyo ya Kwanza na tarehe 05/10/1992 alipokea Sakramenti ya Kipaimara, vyote katika Parokia ya Kirumba,  Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza. Alipata elimu ya msingi darasa la I –V kuanzia mwaka 1991 hadi 1995 katika shule ya msingi Ilemela, kisha darasa la VI – VII mwaka 1996 hadi 1997 katika shule ya msingi Kitangiri.

Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2005 alipata elimu ya sekondari kidato cha I hadi VI katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis de Sales, Kihonda – Morogoro.  Mwaka 2007 alianza kufanya masomo ya Falsafa na kuhitimu mwaka 2010 Shahada ya Falsafa. Kisha aliendelea kwa masomo ya Tauhidi mwaka 2011 hadi 2015 katika Chuo Kikuu cha Jordan, Tawi la Chuo kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania.

Alilifahamu Shirika mwaka 2005 kupitia Frt. Gastor Kateule, OFM Cap. aliyekuwa akisoma katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis de Sales. Kwa jinsi ndugu huyo alivyokua akilielezea Shirika la Wamisionari wa Damu akihusianisha na Utume wa Damu. Maelezo yake yalimfanya Frt. Karabyo kuugua moyo kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima na kulifahamu Shirika.

Aliishi miaka ya malezi ndani ya Shirika kama ifuatavyo; mwaka wa I wa malezi 2006/2007, mwaka wa II wa malezi 2010/2011, yote ilifanyika katika nyumba ya malezi Giovanni Merlini, Miyuji - Dodoma. Kwa sasa anafanya mwaka wa kichungaji Procura na Parokia ya Tegeta – Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam. Alipewa huduma ya usomaji wa masomo rasmi kulingana na taratibu za Kanisa Katoliki tarehe 01/05/2012, kisha huduma ya utumishi altareni tarehe 04/05/2013 katika Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro na Mhashamu Askofu Teresphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro.

Na Rodrick Minja,

Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.