2016-01-07 08:53:00

Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kukuza na kudumisha amani duniani


Nia ya jumla ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Januari 2016: ili majadiliano ya kweli kati ya waamini wa dini mbali mbali yaweze kuzaa matunda ya haki na amani. Baba Mtakatifu anasema, watu wengi duniani wanajitambulisha kuwa ni waamini wenye dini na imani zao, kumbe, kutokana na mwelekeo kama huu, watu wengi zaidi wanaweza kushiriki katika majadiliano ya kidini. Ni kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kutoa kisogo kwa kinzani, vita na migogoro inayoibuka kwa kisingizio cha udini; sanjari na kuondokana na ubaguzi pamoja na hali ya watu kutovumiliana.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mchakato wa amani duniani. Waamini waendelee kusali na kuombea amani duniani pamoja na kushirikiana hata na wale wanaofikiri na kutenda kinyume cha matarajio ya wengi. Baba Mtakatifu anawauliza waamini na watu wenye mapenzi mema, Je, wangependa kufanya jambo la maana zaidi? Basi, ikiwa kama wanataka kutekeleza jambo hili basi washiriki kikamilifu katika kusambaza nia yake kwa mwezi Januari 2016, ili mchakato wa majadiliano ya kidini uweze kuzaa matunda ya haki na amani.

Watu wengi wanafikiri na kutenda katika mielekeo tofauti; wanamtafuta na kukutana na Mungu kwa njia mbali mbali. Baadhi yao wanakiri kwamba, hawana imani, wala hawatambui ikiwa kama Mungu yupo au hapana. Baadhi ya watu wanatangaza kwamba, wao si waamini. Huu ndio mwelekeo wa jumla kwa wanadamu katika ulimwengu mamboleo; kwa wale wanaoamini na wale wasioamini, lakini wote kwa pamoja ni watoto wa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.