Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAWAZA) kwa kushirikiana
n ana taasisi za Kiislam Zanzibar imetoa tamko kuhusiana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar,
tamko ambalo limetolewa kwa waandishi wa habari tarehe 6 Januari 2016 kwenye Ukumbi
wa Umoja wa Walemavu Zanzibar. Viongozi hawa wanawataka wadau wakuu katika mgogoro
huu wa kisiasa na kikatiba kushughulikiwa kikamilifu na mapema kwa kuzingatia misingi
ya ukweli na uwazi.
Wanapinga kauli za uchochezi, chuki na uhasama
pamoja na kumwomba Rais Magufuli kushughulikia mgogoro huu mapema iwezekanvyo. Viongozi
hawa wanawaomba waamini wao kuendelea kutoa dua ili amani, usalama na utulivu viweze
kudumu Zanzibar pamoja na kuhofia kurudiwa kwa uchaguzi, hali ambayo inaweza kuitumbukiza
Zanzibar katika machafuko ya kisiasa! Zaidi unaweza kuendelea sasa!
Awali tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha
kukutana katika hafla hii hali ya kuwa ni wazima; sala na salamu zimfikie Mtume wetu
Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake na wote wanaowafuata kwa wema
hadi Siku ya Malipo.
Ndugu waandishi wa habari, tunawashukuru sana kwa kuitikia wito wetu wa kuhudhuria katika mkutano huu muhimu
wenye lengo la kutafuta maslahi na mustakabali mwema wa nchi yetu. Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislamu Zanzibar tunawashukuru sana Wazanzibari wote
kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu pamoja na kukabiliwa na
mtafaruku mkubwa wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Zanzibar
uliotokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha
kuufuta Uchaguzi wote uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake katika tangazo
lake la tarehe 28-10-2015.
Kitendo hicho cha kuufuta Uchaguzi huo, kimepelekea
nchi yetu kuingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa. Wananchi wa kawaida
ambao ndio wapiga kura wanaathirika kisaikolojia kwa kushindwa kujua khatima ya kura
walizozipiga. Kwa upande mwengine kumekuwa
na ongezeko la ugumu wa maisha visiwani Zanzibar unaotokana na mfumuko wa bei kwa
bidhaa muhimu na mzunguuko wa pesa kuwa mdogo kutokana na baadhi ya Wafanya biashara
kuwa na khofu ya kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa khofu ya kutokea vurugu.
Ndugu waandishi wa habari, sisi tukiwa viongozi wa jamii tumeshughulishwa sana na mtafaruku huu wa kisiasa
unaotukabili ambapo hadi sasa tumechukua hatua zifuatazo kusaidia kufikia ufumbuzi: Tuliwaandikia barua za nasaha viongozi wote wakuu wa kisiasa
wanaoshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huu wa kisiasa.
- Tuliwaandikia barua Mabalozi wa nchi sita waliopo Tanzania kuomba wasaidie katika
kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu katika kuhakikisha kuwa demokrasia inachukua mkondo
wake. Mabalozi wahusika ni kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani,
Norway na Sweeden.
- Tulimwandikia barua Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
John Pombe Magufuli kumkumbusha dhima yake ya kuingilia kati mgogoro huu ili kupatikana
ufumbuzi wa haraka.
- Kupitia hotuba za Ijumaa katika misikiti mbali tumekuwa tukiwanasihi wananchi
wawe na subra ili watoe fursa kwa viongozi wa kisiasa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro
huu kwa njia za amani.
Ndugu waandishi wa habari,
Wananchi wa Zanzibar tulipata matumaini tulipoona kuwa viongozi wakuu wa kisiasa
wanakutana kuzungumzia hali ya kisiasa nchini, tuliamini kuwa katika vikao hivyo Viongozi
hawa wenye kuheshimika wakitawaliwa na busara, hekima, uadilifu na wakiweka mbele
maslahi ya taifa badala ya vyama vyao basi muda si mrefu tungepata ufumbuzi wa mgogoro
huu. Bahati mbaya tunaambiwa ni vikao 8 sasa vimeshafanyika
tokea kikao cha mwanzo cha tarehe 9 Novemba, 2015 hakuonekani kuwa matumanini yale
wananchi waliyoyajenga kwao kuwa yatatimia.
Tunasema hivi kwa sababu kwanza vinaendeshwa kwa
usiri mkubwa mno na hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa umma. Hali hii inawafanya wananchi kutoelewa kinachoendelea na
hivyo kuishi maisha ya wasi wasi na kukosa utulivu hata wa kufanya shughuli zao za
kimaisha. Kasoro nyengine ni kuwa vikao hivi vimechukua muda mrefu sana na hivyo kuibua
maswali mengi na shaka kwa wananchi. Pia tabia
iliyojitokeza ya baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mazungumzo hayo kutoa kauli zinazoshabikia
msimamo wa upande mmoja kunawatoa imani wananchi juu ya kuwepo kwa nia njema katika
mazungumzo hayo na kwamba mazungumzo hayo yanaweza kuivusha nchi yetu katika mkwamo
huu wa kisiasa unaohatarisha usalama wa nchi yetu.
Kutokana hali hii sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam
Zanzibar tunatamka kwamba:-
- JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar zinawataka Viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki
katika mazungumzo kuwajibika kwa kuweka mbele maslahi mapana ya nchi, kuhitimisha
mazungumzo yao haraka iwezekanavyo na kutoa maamuzi rasmi ikiwa ni muongozo wa kutukwamua
hapa tulipo kwa njia ya amani na salama. Tunawatanabahisha kuwa jamii yetu kwa sasa
ni mfano wa bomu linaloweza kuripuka wakati wowote ule.
- Ukimya na uvumilivu wa Wazanzibari uliopo kamwe usichukuliwe kuwa wao ni Malaika
bali ni binaadamu kama walivyo wengine ambao wanaweza kufikia hatua ya kushindwa na
uvumilivu na kutoa maamuzi magumu yanayoweza kutufikisha pahala pabaya na kuigharimu
sana nchi yetu. Hatuombi jambo hili kutokea lakini likitokea viongozi wakuu wa kisiasa
watabeba dhima mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo basi, tunawaomba Viongozi wakuu
wa kisiasa wanaoshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi, ni wakati muwafaka
sasa watoke hadharani na watoe taarifa kwa umma juu ya hatua iliyofikiwa na ikiwezekana
lini mazungumzo hayo yatakamilika na Wazanzibari watarajie nini kutokana na mazungumzo
hayo.
- Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar, tunapinga kwa nguvu zetu zote kauli
za uchochezi zinazoendelea kutolewa na wanasisa ambazo zinazidi kujenga khofu, hamasa
na chuki miongoni mwa wananchi. Aidha, tunasikitika kuona kuwa kauli hizo zinatolewa
bila ya kujali mazungumzo yanayoendelea ya viongozi wakuu ya kutafuta ufumbuzi.
- Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar, kwa heshima kubwa tunamuomba
sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. John
Pombe Magufuli ambaye ameonesha dalili njema za uadilifu na uwajibikaji mkubwa achukue
hatua za wazi na za haraka katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu kabla nchi yetu
haijatumbukia pahala pabaya. Aidha, tunamuomba kusimamia kwa udhati na ujasiri
kuona haki inachukua mkondo wake na maamuzi ya Wazanzibari walio wengi yanaheshimiwa.
- Katika Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 JUMAZA ilikuwa na waangalizi katika
majimbo yote ya Unguja na Pemba, kasoro zilizoripotiwa katika Uchaguzi huu ni kasoro
ndogo ndogo mno na kwa hakika ni afadhali kuliko chaguzi zote zilizopita huko nyuma
tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vyangi. JUMAZA inashangazwa sana na hatua ya kufuta
Uchaguzi huu iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha.
JUMAZA inauliza kwanini wakati tulipokuwa na kasoro kubwa zaidi katika chaguzi za
mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 Uchaguzi haukufutwa na kutakiwa kurejewa tena iwe Uchaguzi
wa mwaka 2015 tu? Na jee kama uchaguzi utakaorejewa nao ukawa na kasoro zitakazolalamikiwa,
utafutwa tena? Tutafanya chaguzi ngapi kwa mtindo huu?
- Taasisi za Kiislam Zanzibar zinawaomba Waislamu wote kuendeleza dua ili kuitakia
mema nchi yetu na kumkabidhi Mwenyezi Mungu kwa wale wote wanaokusudia shari. Aidha,
zinawaomba Maimamu na Makhatibu kukemea kauli zinazohatarisha amani na mshikamano
wa jamii.
- JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar zina khofu kubwa juu ya kurejewa kwa Uchaguzi,
uzoefu unaonesha kuwa nchi zilizorejea uchaguzi katika Bara la Afrika kama vile Nigeria,
Zimbwabwe, Malawi na kwengineko hatimaye zilitumbikia katika machafuko makubwa. Kama
hilo halitoshi Zanzibar tuna historia mbaya ya kurejea Uchaguzi. Wengi tunakumbuka
katika historia ya Zanzibar kile kinachoitwa ‘vita au machafuko ya Juni ‘. Uchaguzi
wa Januari mwaka 1961 ulilazimika kurejewa mwezi wa Juni 1961, ambapo ulipelekea machafuko
makubwa ikiwemo vifo vya watu 68, maelfu kujeruhiwa, nyumba kuvunjwa na kuchomwa moto.
Kwa historia hii JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar hazioni kuwa ni busara kurejewa
kwa Uchaguzi uliofanyika kwa ufanisi na kukamilika. Penye nia njema na utashi wa kisiasa
basi njia ya uadilifu iliyo wazi ya kutukwamua hapa tulipo ni kwa Viongozi wakuu wa
kisiasa kufikia ufumbuzi na makubaliano haraka iwezekanavyo.
Mola wetu Mtukufu tunakuomba kwa rehma zako utuwezeshe kufikia ufumbuzi unaofaa
juu ya tatizo linalotukabili na uziunganishe nyoyo za Wazanzibari kuwa pamoja, kupendana
na kuweka mbele maslahi ya nchi yao. Amiin.
AHSANTENI
MUHIDDIN Z. MUHIDDIN
KATIBU MTENDAJI
JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR