2016-01-07 09:46:00

Frt. Dastan Mushobolozi Balayangaki, kupewa Daraja la Ushemasi, Roma!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, katika mkesha wa Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, Jumamosi, tarehe 9 Januari 2016 anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Frate Danstan Mushobolozi Balayangaki, Mmissionari wa Shirika la Consolata, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Parokia ya  “SS Crocifiso” iliyoko Jimbo Kuu la Roma majira ya saa 10: 30 jioni kwa saa za Ulaya. Frate Mushobolozi anaweka nadhiri za daima Ijumaa, tarehe 8 Januari 2016, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Seminari kuu ya Waconsolata iliyoko Bravetta, Jimbo kuu la Roma. Ifuatayo ni historia ya Shemasi mtarajiwa!

Mimi Danstan Mushobolozi Balayangaki, mmisionari wa Consolata, nilizaliwa katika Parokia ya Ishozi Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania, 06/12/1981, mwana wa Benedikto R. Balayangaki (miaka 61) na Magreth Kokutora ( miaka 53). Nikiwa mtoto wa kwanza katika familia  ya watoto sita. Mwaka huu kwangu ni mwaka wa neema, Mungu amenipenda zaidi kwani ameniangalia kwa macho yake yenye huruma na kutaka kunihesabu kati wa watumishi na kutufanya kuwa chombo chake cha kuwagawia watu wake huruma na mapendo. Kama Baba Mtakatifu Francisko anavyozungumzia juu ya miito katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwa namna ya pekee kabisa kutualika sisi  wabatizwa kuwa na furaha na kugundua kuwa wito wa Kikristo unatoka kwake kama zawadi na neema amabayo kila mtu anapewa kwa huruma na upendo wake kwetu. Si kwa mastahili yetu ila anatuchagua tu, na kutaka tumtumikie katika hilo.

Baba Mtakatifu anasema tendo la huruma kwetu kutoka kwa Mungu Mwana ni kusamehe dhambi zetu na kutuita katika maisha mapya ya kuwa wafuasi wake na kila mmoja ana mpango naye. Anaendelea kusema, kila wito una chanzo chake katika mtazamo wa huruma wa Yesu kama alivyomwona Mathayo mtoza ushuru (Mt. 9,9-13; Mk. 2,13-17) au alivyomwona Zakayo (Lk 19,1-10), hivyo hivyo anamwona kila mmoja wetu na kumuita katika kazi yake na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ni sauti ya Mungu inayopita kwa kila mmoja wetu ikisema "Shuka leo nashinda kwako". Basi  mwaka 2016 naona macho yake yenye huruma yameniangalia na kusikia sauti yake ya upendo ikiniambia niwe chombo chake cha huruma na faraja kama mmsionari wa Consolata (faraja). Najisikia kushirikishwa katika nafasi muhimu sana ya kufariji, wapi? Sijui!!! vipi? Sijui!!! Hila natumainia neema yake, kwenda na kuongozwa na yeye anitiaye nguvu. Ndiyo maana naamini sana kuwa, “niyaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Fil. 4,13).

Historia fupi

Ilikuwa ni tahere 01/10/2005, ndipo nilipofika Morogoro, Tanzania kwenye nyumba ya malezi ya Wamissionari wa Consolata. Safari ilianza na wenzangu 6. Tukawa na mwaka mmoja wa malezi kabla ya Falsafa, baada ya hapo tukajiunga na Chuo cha Wasalvatori kilichoko Kola, Jimbo Katoliki la Morogoro kwa ajili ya mafunzo ya Falsafa.  Safari iliendelea baada  falsafa mwaka 2009, wawili kati yetu walikwenda Msumbiji kwa ajili ya Unovisi na mimi na wenzangu watatu tukaenda Kenya ata sisi kwa ajili ya malezi ya Kinovisi.

Tukabahatika kuweka Nadhiri za kwanza tarehe 17/07/ 2010. Baada ya hapo tukasambaratika, mmoja alikwenda Afrika Kusini, Mwingine Congo (DRC) , mmoja akabaki Kenya nami nikatumwa Italia – Roma, kwa ajili ya Masomo ya Taalimungu. Baada ya masomo hayo hapa Italia nimepata muda wa mwaka mmoja wa kufanya mazoezi ya uchungaji,  huko Kusini mwa Italia, Puglia katika mkoa wa Taranto sehemu hiitwayo Martina Franca.

Hapa nilionja uzuri wa huduma hii kwa kuhamasisha na kujifunza kwa vijana, kupeleka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na kutembelea wazee, vikundi vya walemavu;  kushiriki katika ofisi ya jimbo kuhusiana na masuala ya uhamiaji, kwa kushirikiana na Utume wa hutoa huduma ya kiroho kwa mabaharia pamoja na kuishi maisha ya jumuiyai ndogo ya shirika ambapo tulikuwa wanashirika wanne, tukitoa faraja katika eneo hilo. Maisha ya Kijumuiya yamenisaidia kutambua na kugundua uzuri, utakatifu, dhamana na changamoto za maisha ya kitawa ndani ya Kanisa na katika ulimwengu kwa ujumla. Ninaweza kuyaambata ya mbeleni kwa ujasiri na moyo mkuu katika Yeye anitiaye nguvu!

Kwa sasa nimerejea tena Jijini Roma nikiendelea na masomo, na niko kwenye maandalizi  kuweka nadhiri za milele tarehe 08/01/2016 na ya daraja la Ushemasi tarehe 09/01/2016. Nakuomba mpendwa msikilizaji unikumbuke na kuniombea ili kweli niweze kuwa ni chombo cha huduma na huruma ya Mungu kwa njia ya Daraja la Ushemasi wa mpito!

Umissionari

Naomba sala zenu kwa ajili ya kazi hii ya Kimissionari ambayo sote tunashikiriki kama wabatizwa. Sisi hatufanyi lolote jipya ila baada ya kuhubiriwa Injili miaka zaidi ya mia moja na hamsini ya Kanisa nchini Tanzania sasa na sisi tunarudisha na kuwamegea wengine ile imani tuliyorithishwa. Hapa ni kama tunalipa deni. Inatia moyo sana kuona tunajaribu na tunawakilisha dini yetu, imani yetu, na utanzania wetu. Kanisa la Afrika ni tumaini la Kanisa zima.

Na Danstan Mushobolozi Balayangaki, mmisionari wa Consolata.








All the contents on this site are copyrighted ©.