2016-01-06 15:47:00

Papa Francisko, Karibu tena Kenya, hakuna matata!


Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anasema, familia ya Mungu nchini Kenya kwa mwaka 2015 ilipata bahati sana ya kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anatembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika. Itakumbukwa kwamba, mara ya mwisho, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Kenya kunako mwaka 1995, hapa vijana wengi wa kizazi kipya walikuwa hawajazaliwa bado. Miaka ishirini baadaye, Baba Mtakatifu Francisko ameleta mwamko mpya katika maisha na utume wa Kanisa nchini Kenya.

Baba Mtakatifu ameacha alama ya kudumu katika mioyo na maisha ya watu. Siku tatu za uwepo wake nchini Kenya zimekuwa ni ushuhuda wa upendo, tafakari, umoja na mshikamano wa kitaifa na ushuhuda wa imani kwa familia ya Mungu nchini Kenya. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi, familia ya Mungu nchini Kenya iliweka kando tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila, wakaungana na kuonesha umoja wa kitaifa katika mchakato wa maandalizi na hatimaye, kumpokea Baba Mtakatifu Francisko alipowatembelea na kuwahimiza kusimama kidete kulinda na kuendeleza Kenya ambayo ni nyumba ya wote, kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kile kijacho!

Kardinali Njue anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko ameihamasisha familia ya Mungu nchini Kenya kupyaisha maisha yake, kwa kudumisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira; kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano, haki, amani, upatanisho, msamaha na maridhiano kati ya wananchi wa Kenya, ili kuganga na kuponya madonda ya utengano, chuki na uhasama unaofumbatwa na udini na ukabila usiokuwa na mvuto wa mashiko kwa maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko ameikumbusha familia ya Mungu nchini Kenya kwamba, adui mkubwa wa amani, ustawi na maendeleo ya wengi ni woga, hali ya kudhaniana vibaya, chuki na uhasama mambo yanayokumbatiwa na umaskini pamoja na hali ya kuchangikiwa katika maisha. Hapa viongozi wa familia ya Mungu wamekumbushwa kwa namna ya pekee dhamana na wajibu wao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu anasema Kardinali Njue, ulitua kwa wakati muafaka kwani Kenya ilikuwa inakabiliwa na kashfa ya rushwa na ufisadi, hali ambayo ilipelekea baadhi ya mawaziri kuachishwa kazi.

Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya umechochea mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kuambata misingi ya haki, amani na mshikamano kwani Mungu ni Mungu wa amani anayewataka wote kuishi kwa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, huku wakiheshimiana na kuthaminiana kwani wote ni watoto wa Mungu. Baba Mtakatifu aliwataka Wakenya kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kupata raia wema na watakatifu, tayari kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Njue anakaza kusema, Baba Mtakatifu aliwataka Wakleri na Watawa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika maisha na wito wao. Wawe ni wamissionari wa matumaini, upendo, urafiki na huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Iwe ni fursa ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote ili kuweza kukabiliana na majanga asilia. Baba Mtakatifu amewakumbusha wananchi wa Kenya kwamba, kuna uhusiano wa pekee kati ya: Mungu, binadamu na mazingira. Hapa Baba Mtakatifu alipanda mti wa kumbu kumbu endelevu ili kuonesha uhusiano wa mambo haya msingi. Upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii umeoneshwa kwa namna ya pekee, pale Baba Mtakatifu alipowatembelea wananchi wa Kangemi na kuitaka familia ya Mungu nchini Kenya kuhakikisha kwamba, inashirikiana kwa pamoja, ili watu waweze kupata makazi bora, maji safi na salama, ili wananchi wote waweze kufurahia amani, ustawi na maendeleo, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko ilifikia kilele chake pale alipokutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya, akasikiliza wasi wasi na matumaini yao kwa Kenya iliyo bora zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu akawataka vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Aliwataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali, ili kuimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu aliwataka wanasiasa kuibua sera makini zitakazowawezesha vijana kupata fursa za ajira pamoja na kushinda kishawishi cha kuwa na misimamo mikali ya kidini inayopelekea maafa kwa watu wasiokuwa na hatia. Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanatoa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya.

Kutokana na changamoto zote hizi, anasema Kardinali Njue, Kanisa Katoliki nchini Kenya linataka kuendeleza moto wa mapendo, matumaini na ushirikiano uliowashwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya, ili atakaporudi tena nchini Kenya akute Kenya ikiwa na mwelekeo mpya zaidi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linamwambia Baba Mtakatifu Francisko, Karibu tena Kenya, “hakuna matata”!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.