2016-01-06 15:09:00

Kanisa linapenda kuwasaidia watu kumwona, kukutana na kumwabudu Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, amewakumbusha waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwamba, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliokwenda kumwona na kumwabudu Masiha ni kielelezo cha ulimwengu ambamo Mama Kanisa anataka kuhakikisha kwamba, watu wote duniani wanapata fursa ya kukutana na Yesu, ili kuonja upendo wenye huruma.

Kristo aliyekuwa amezaliwa punde tu, hakuwa anaweza kuzungumza, lakini watu wote wanaowakilishwa na Mamajusi waliweza kukutana, kumfahamu na kumwabudu, kama walivyoshuhudia Mamajusi walipofika mjini Bethlehemu na kumsimulia Mfalme Herode. Mamajusi walikuwa ni wasomi wa hali ya juu kutoka dini na tamaduni mbali mbali, waliofunga safari kuelekea Israeli ili kumwabudu Mfalme aliyekuwa amezaliwa hivi punde.

Kwa njia ya ushuhuda wa Mamajusi hawa, Kanisa daima limeona ubinadamu unaofumbatwa katika ushuhuda huu na kwa njia ya maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, linataka kuhakikisha kwamba linawaongoza watu kuheshimu binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wanaomwelekea Mtoto Yesu aliyezaliwa kwa ajili ya wokovu wa wote.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wakati wa Usiku wa Noeli, Yesu alijifunua kwa wachungaji, watu waliokuwa wanyenyekevu na ambao hawakuthaminiwa sana na jamii iliyokuwa inawazunguka. Siku kuu ya Tokeo la Bwana, inawaonesha Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali wanaovutwa kwa mshangao wa ajabu kwenda kumwona Mtoto Yesu. Makundi haya mawili yanatofautiana na kusigana kwa mambo mengi, lakini yanaunganishwa na jambo moja yaani mbingu!

Wachungaji walitimua mbio kwenda kumwona Mtoto Yesu aliyekuwa amezaliwa si kwa sababu walikuwa ni wema na watakatifu, bali walikuwa wanachunga mifugo yao, huku wakikesha, lakini walipoinua macho yao juu mbinguni wakaona alama, nyota angavu, iliyowasilisha fumbo na kuanza kuitafuta. Wachungaji na Mamajusi wanawafundisha waamini kwamba, ili kumwona Yesu hawana budi kuinua macho yao mbinguni, bila kujitafuta wao wenyewe, bali kwa kuwa na moyo na akili wazi ili kugundua mwelekeo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani Mwenyezi Mungu daima anaendelea kumshangaza mwanadamu, ili kupokea ujumbe wake na kuutekeleza kwa utayari na ukarimu.

Mamajusi walishikwa na furaha kuu walipoiona ile nyota angavu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupata faraja wanapoiona nyota au pale wanaposikia kwamba, wanaongozwa na nyota hii bila kutelekezwa. Nyota hii angavu anasema Baba Mtakatifu ni Injili, Neno la Mungu, taa inayoangazia miguu ya waamini katika mapito yao ya kila siku. Hii ni njia inayowaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Bila kuwa wasikivu makini wa Neno la Mungu si rahisi sana kuweza kukutana na Kristo. Mamajusi waliongozwa na nyota hadi kufikia mahali alipokuwa amelazwa Mtoto Yesu, hapo wakamwona Mama na Mwanaye, wakamsujudia na kumpatia zawadi zao.

Huu ni mwaliko wa kuona matukio mbali mbali katika maisha kama fumbo la ufunuo wa Mungu. Kamwe watu wasikwazwe na matukio madogo madogo ya maisha na umaskini, lakini watambue ukuu, unyenyekevu na kuwa tayari kuyapigia magoti, ili kumwabudu Kristo Yesu. Bikira Maria aliyewapokea Mamajusi mjini Bethlehemu awasaidie waamini kuinua macho yao mbinguni na kujiachia ili waweze kuongozwa na Nyota ya Injili, ili kukutana na Yesu, tayari kujinyenyekeza ili kumwabudu. Baba Mtakatifu anasema, kwa njia hii, waamini wataweza kuwapelekea wengine nuru ya mwanga wa Kristo na kuwashirikisha ile furaha ya hija yao ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.