2016-01-06 11:06:00

Kanisa linapania kudumisha mafao ya wengi, haki na amani nchini DRC


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo linasema, linapenda kuwahamasisha wanasiasa na wadau mbali mbali nchini humo ili kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kukamilisha ratiba ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwezi Novemba, 2016. Lengo ni kutaka kuendeleza mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani, demokrasia na umoja wa kitaifa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wananchi wote wa DRC.

Hivi karibuni, ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC umekutana na kuzungumza na viongozi wa Tume huru ya Uchaguzi nchini DRC, INEC. Maaskofu, kama wachungaji wakuu, wanapenda kuona kwamba, uchaguzi mkuu unafanyika kadiri ya ratiba, taratibu, sheria na kanuni, ili uweze kuwa wa kweli, huru na wazi. Ratiba ya uchaguzi mkuu bado haijapitishwa na Bunge la nchi hiyo, ratiba ambayo inapaswa kuzingatia hali halisi ya DRC pamoja na kukubaliwa na wengi.

Mchakato wa ratiba ya uchaguzi unapaswa kushughulikiwa na Bunge la DRC, Serikali pamoja na Tume huru ya uchaguzi nchini DRC. Uchaguzi wa Rais na Wabunge unapaswa kupewa msukumo wa pekee katika upatikanaji wa muafaka kuhusiana na tarehe rasmi ya uchaguzi.  Itakumbukwa kwamba, tangu uchaguzi mkuu wa DRC uliofanyika mwezi Novemba 2011, kumekuwepo na machafuko ya hali ya kisiasa nchini humo, hali ambayo imesababisha maandamano makubwa kutoka kwa wapinzani. Kuhairishwa kwa uchaguzi mkuu wengine wanasema, ni njama za Serikali ya Rais Joseph Kabila za kutaka kuendelea kubaki madarakani kinyume cha Katiba ya nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.