2016-01-05 14:27:00

Watoto ni wamissionari wa huruma na mapendo!


Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama Siku kuu ya Epifania  kwa Mwaka 2016 ina na umuhimu wa pekee kwani maadhimisho haya yanafanyika wakati Kanisa linaendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wakati wa Siku kuu hii, watoto watakuwa ndio wahusika wakuu, wanaohamasishwa kuwa wamissionari wa huruma na upendo miongoni mwa watoto wenzao kama alivyokuwa Yesu aliyezaliwa katika hali ya umaskini, ili kuwavuta wote kwake kwa kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu.

Hii ni siku ambayo inasimamiwa kwa namna ya pekee na Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari, lengo ni kuhakikisha kwamba, watoto wanajifunza kuwa wakarimu kwa kuvuka na kuvunjilia mbali vikwazo vinavyoweza kuwafanya wasindwe kuwajali watoto wenzao wanaoteseka kutokana na vita au wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta usalama wa maisha. Watoto wanahamasishwa kuonesha moyo wa huruma na ukarimu kwa kushirikiana na Makanisa mahalia.

Wakati wote wa kipindi cha Majilio, watoto wamejiandaa kwa njia ya Katekesi makini ili kuwasaidia kuweza kuadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watoto wametafakari matatizo na changamoto zinazoendelea kuwakumba watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia kutokana na: umaskini, vita, njaa, magonjwa pamoja na majanga asilia. Wamegusia tatizo la matumizi haramu ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo na utalii wa ngono ambamo pia watoto wadogo wanajikuta wametumbukizwa humo

Watoto hawa wameangalia madhara ya watoto kupelekwa vitani na ndoa za utotoni zinavyo athiri ukuaji na maendeleo ya watoto kwa siku za usoni. Bado kuna mamillioni ya watoto wanaotengwa na kutelekezwa; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto ambao wamebaki yatima kutokana na kuondokewa na wazazi pamoja na walezi wao! Haya yote ni matatizo na changamoto zinazowakabili watoto sehemu mbali mbali za dunia, bila kusahau nyanyaso za kijinsia zinazotendeka hata katika kuta za kifamilia.

Familia za watoto hawa zimeshirikishwa ili kuona changamoto hizi katika uhalisia wa mazingira yao, tayari kuchukua hatua makini kwa kuonesha huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Maadhimisho ya Mwaka 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Maskini kama Yesu”. Mwaliko wa kumwangalia Mtoto Yesu aliyezaliwa katika mazingira ya umaskini, tayari kwa watoto hawa kuwa huru kupenda kama Yesu alivyowapenda na kuyamimina maisha yake pale Msalabani ili kuwaondolea dhambi na kuwpatanisha na Mungu.

Wakimbizi na wahamiaji; maskini na matajiri, wote hawa wanapata faraja na hifadhi kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na mapendo. Watoto kwa njia ya Katekesi makini wanaweza kutambua umuhimu wa kupokea huruma ya Mungu katika maisha yao tayari kuwashirikisha watoto wenzao bila kutegemea kurudishiwa chochote! Yote wanayafanya kwa kusukumwa na huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Taarifa mbali mbali zinazowafikia wengi katika familia ni za kukatisha tamaa na kuwajengea watoto hofu na woga kiasi hata cha kuwafanya kujifungia katika undani wao! Lakini wanapaswa kuelimishwa na kusaidiwa kutambua kwamba, wanahamasishwa kuwa ni wamissionari wa huruma na mapendo, kwa watoto wenzao wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya maisha.

Watoto wawe na ujasiri wa kujinyima kidogo, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma kwa watoto wenzao. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwashirikisha watoto hawa furaha ya kuwa Wamissionari wa huruma na upendo wa Mungu, changamoto hata kwa watu wazima kushikamana ili kupambana na baa la njaa, umaskini na magonjwa yanayoendelea kuhatarisha maisha ya watoto wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.