2016-01-05 10:06:00

Ujumbe wa utume wa Sala kuanza kutolewa kwa njia ya video!


Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuboresha ujumbe wa nia anazozitoa kila mwezi na kwa sasa kuanzia tarehe 6 Januari 2016 nia hizi zitatolewa kwa njia ya video, huduma inayotolewa na Utume wa Sala kwa kushirikiana na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV. Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Utume wa Sala Kimataifa anasema huu ni mtandao wa Sala ya Baba Mtakatifu kimataifa, kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto zinazomkumba mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Sala hizi ni utume wa Kanisa unaowawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuona kwa jicho la imani changamoto katika maisha ya binadamu, ili kuweza kuwashirikisha watu wengi zaidi. Lengo ni kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo, huruma pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu Francisko alikwisha wahi kusema kwamba, watu wengi wanaguswa na picha za mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa bahati mbaya, hawana lolote wanaloweza kutenda!

Katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu anautaka Utume wa Sala, kuhakikisha kwamba, unasaidia kuwahabarisha walimwengu kuhusu changamoto ambazo Kanisa linakabiliana nazo katika maisha na utume wake, kwa njia ya video. Hii ni kazi inayofanywa na wataalam wa masuala ya video na itakuwa inatolewa katika lugha kumi za kimataifa, ili kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali pamoja na Baba Mtakatifu, ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi kwa imani na matumaini.

Video ambayo itatolewa kila mwezi, itasambazwa kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii na kwamba, ni Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe atakayekuwa anazungumza na kuwasaidia waamini kusali pamoja naye kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizi kwa maendeleo ya binadamu kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu hivi karibuni aliwataka waamini kujiwekea malengo ya kusali zaidi katika kipindi cha mwaka 2016. Kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaendelea kuhamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kutenga muda zaidi kwa ajili ya sala binafsi na zile za kijumuiya, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kwa mwezi Januari, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kudumisha majadiliano ya kidini, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa mataifa.

Baba Mtakatifu atakuwa anatumia lugha ya Kihispania na baadaye, sala hii kutafsiriwa kwa lugha mbali mbali. Kwa njia ya video, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wataweza kufungua malango ya mioyo yao kwa ajili ya jirani zao. Hawa ni wanawake na watoto, wazee na watu wenye shida na magumu katika maisha. Kwa njia ya sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, Kanisa linaweza kuendelea kutekeleza utume wake miongoni mwa watu wa mataifa. Lengo ni kujenga na kudumisha mshikamano wa huruma na mapendo ili kushinda hali ya kutojali, tayari kuambata amani, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.