2016-01-05 14:48:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Ni kipindi cha kutafakari: historia, maisha na utume


Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yatakayofikia hatima yake hapo tarehe 2 Februari 2016, wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Hiki ni kipindi muafaka kwa watawa kuhafamu kwa kina na mapana: historia, karama na maisha ya shirika husika kadiri ya mpango wa waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yanawagusa pia hata waamini walei ambao kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo wamewekwa wakfu na hivyo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kielelezo cha imani tendaji. Kumbe, waamini walei wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu ahadi zao za Ubatizo kwa kumkataa shetani na kuambata maisha mapya.

Askofu Mlola anawahamasisha watawa kujifunza kwa kina historia ya Mashirika yao, kuangalia maendeleo yaliyokwisha kupatikana pamoja na changamoto zake, ili kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini; wakiwa tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha. Watawa watambue na kuthamini asili ya mashirika yao ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Kristo.

Askofu Mlola anakaza kusema, Injili kwa waanzilishi wengi wa Mashirika imekuwa ni Kanuni msingi, dira na mwelekeo wa maisha na Katiba kwao ilikuwa ni sehemu ya mchakato wa kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha, ili kufikia ukamilifu wa maisha. Hapa Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili upendo wa watawa kwa Kristo na Kanisa lake uweze kujidhihirisha zaidi. Watawa waendelee kuwa ni chemchemi ya furaha, umoja, upendo, mshikamano na amani, ili kumpendeza Mwenyezi Mungu pamoja na kuwasaidia waamini kutekeleza ahadi zao za Ubatizo kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.