2016-01-05 15:43:00

Mamajusi walivyopiga chenga ya mwili Mfalme Herode!


Utabiri wa tabia na bahati ya mtu kadiri ya nyota ni wa zamani sana. Watabiri wa nyota walipanga tabia na maweza ya mtu kadiri ya mpangilio wa nyota na matangamano yake ya angani – constellations. Watabiri wamepanga majina kumi na mbili ya nyota na bahati yake, hadi umezuka msemo: “Kila mtu na nyota yake.” Wako wapenzi wa nyota wanaofuatilia kwa karibu sana utabiri huo, lakini wengine wanaona utabiri huo wa nyota ni upuuzi na ushirikina. Kuwa na nyota yoyote au kudhihirika kwa nyota aina yoyote ile kwa mtu au kikundi cha watu, kunaitwa epifaniaNeno hilo ni la lugha ya Kigiriki lina maana ya kutokea, au kuonekana. Kwa Wagiriki epifania hiyo limaanisha kuonekana kwa miungu yao katika matukio ya pekee yaliyolikumba taifa lao. Mathalani nchi inapokumbwa na vita au janga, hapo kulitokea – epifania – ya miungu, inayoweza kutabiri ushindi au kushindwa. Epifania hiyo ilikuwa nguvu ya kimiungu inayoingilia kati maisha yao. Watabiri wa epifania hiyo ya nyota waliitwa majusi au waganga wa jadi. Mara nyingi epifania hiyo ilikuwa uwongo.

Kadhalika katika Maandiko matakatifu (Biblia) hasa kitabu cha Hesabu kulitabiriwa kutokea kwa nyota epifania katika taifa la Israeli. Katika kituko cha Barak, mfalme wa Moab alimwita majusi Balaam aliyetakiwa kutoa unabii wa kulilaani taifa la Israeli. Kumbe badala ya kulaani yeye akatangaza kutokea nyota ya pekee – epifania ­– katika Yakobo. Nyota hiyo ni mfalme wa Israeli atakayeleta utawala mpya ulimwenguni pote. Mwandishi wa kitabu cha Hesabu alidhani kuwa nyota hiyo angekuwa Uzia mfalme wa wakati wake lakini baada ya kupita muda mrefu ikagundulika kuwa unabii huo wa Uzia haikutimilika, na Waisraeli wakaendelea kungojea epifania ya nyota hiyo.

Leo tutawashuhudia Majusi watatu kutoka Mashariki, waliiona nyota ya pekee iliyowaongoza hadi ikaenda kutua pahala alipozaliwa mtoto mchanga. Huyu ni Mungu wa kweli, Yesu Kristu. Kwa hiyo toka awali kanisa linasherehekea epifania au sikukuu ya tokeo la Bwana. Epifania hiyo ni pia sikukuu ya kuzaliwa kwake (Noeli), na ubatizo wake. Wakristu wa kwanza waliwafananisha Majusi na wafalme wanaotajwa katika kitabu cha Isaya 49, na katika Zaburi 72 kama ilivyonukuliwa na Mwinjili Mateo: “Wafalme wa sheba na saba wataleta vipaji.”

Majusi hawa ni utimilifu wa Agano la kale. Aidha kwa vile zawadi zilikuwa tatu, hata wafalme waliozitoa walikuwa watatu, nao ni Melkior, anayeoneshwa kuwa mzee mwenye ndevu nyeupe akitoa zawadi ya dhahabu. Baltazar ni mtu mzima mwenye ndevu nyeusi anatoa Manemane au manukato, halafu Gaspar anaoneshwa kuwa kijana asiye na ndevu anatoa zawadi ya Ubani. Watu hawa wanaotofautiana umri, kabila na taifa ndiyo wanaoifuata nyota ya Noeli yenye mwanga wa Mungu aliye maana ya maisha yao.

Epifania ya Wakristo haina miungu ya pekee inayotisha, bali ni mtoto mchanga wa kawaida kabisa aliyeviringishwa nguo na kulazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Hiyo ndiyo epifania yenyewe ya upendo wa Mungu usio na mipaka kwa binadamu. Kutokana na aina hii ya epifania tunayakuta makundi mawili tofauti yanayoipokea. Mosi, ni Majusi wapenzi wa nyota. Pili, ni wakuu wa dini na wana siasa wanaoipuuza nyota hiyo. Yesu alizaliwa Betlehemu ya Yuda wakati wa mfalme Herode. Majusi walisafiri toka Mashariki (Persia na Arabia) hadi Yerusalemu wakiongozwa na nyota. Majusi wanaifuata nyota lakini siyo ile ya isemwayo katika kitabu cha Hesabu bali nyota mpya ya utawala wa Yesu. Walitaka kumpigia magoti mfalme mpya aliye mbadala wa wafalme wa kale.

Kikundi hiki cha majusi kinawawakilisha wale wote walioangazwa na kustaajabishwa na mwanga huo katika injili. Mathalani, Zakaria anapoongea juu ya mwanga ulioshuka toka juu. Mzee Simoni anasema: “Mwanga wa kuwaangazia taifa lake Israeli.” Malaika anapowatokea wachungaji usiku wanasema “mwanga umewatokea na utukufu wa Bwana umewafunika kwa mwanga.” Mwanga huo ni Yesu anayeangaza ulimwengu mzima. Hii ndiyo Epifania ya  Mungu, mwanga wa kweli ulio ufunuo kuwa Mungu ni upendo, na Yesu amekuja kuufunua hapa duniani.

Tabia ya majusi hao, kwanza wanainua macho na kuangalia nyota angani, yaani ni watu wanaotafakari mambo ya juu. Huko angani wanaona mwanga wa utukufu wa Mungu kisha wanasifu au kuabudu kazi ya mikono yake. “Kazi ya mikono yako hutangaza utukufu wako.” (Zaburi ya 19). Kwa hiyo mtu akitaka kulingana na majusi hawa, budi ainue macho yake angani na kuhoji uwepo na hatima ya maisha yake. Pili majusi husikiliza na kutekeleza sauti inayowakereketa mioyoni mwao na hawafuati miyumbisho ya maisha isiyo na maana.

Majusi ni watu wanaowakilisha wote wanaotafakari na kufuta mambo muhimu ya maisha. Tatu, majusi hawakai kiwetewete mchele wa mama waliwa na ndege, bali daima wanashughulika. Daima wanatafuta kujua ufalme mpya, mahusiano mapya, utawala mpya na mwanga mpya. Majusi wanapoingia mjini Yerusalemu, nyota iliyowaongoza inazima mwanga wake na inapotea. Kwa hiyo Majusi wanalazimika kwenda kuuliza. Hapo ndipo wanapokutana na kikundi cha pili kinachopuuzia  na kuchukia epifania hiyo ya nyota.

Mosi, yuko Herode, yeye anaposikia juu ya nyota anashtuka – Parasein. Kwa kigiriki parasein maana yake ni kuchefuka nyongo kama machafuko ya bahari. Hapa Herode anawakilisha wanasiasa wote, na wale walio katika mfumo wa dini usiotaka mabadiliko. Watu hao wana picha ya Mungu inayotokana na mfumo wao wa dini uliofungwa, na wameridhika na mambo. Wao wanamtaka Mungu anayetetea maisha yao, mfumo wao wa utawala, uongozi na ukuu wao. Watu hao wameshalewa ukuu, madaraka na kutaka kuonekana kwa nje.

Herode na  wataalamu wa maandiko na makuhani wanalo neno la Mungu na wanalifahamu, wangetakiwa kuwa asili ya maisha, na kupokea mwanga. Mwanga huo unapong’aa kwa watu wa kila umri, katika mazingira yoyote yale, yabidi kufungua akili ya moyo. Kadhalika kwa Herode aliyekuwa mwuaji mkuu pamoja na makuhani hawa wangeweza kuongoka na kuacha maisha yao ya awali kutokana na kulifahamu neno la Mungu. Kumbe, wanapoteza fursa hiyo. Mapato ya kutopokea mwanga wa nyota ni kuwa waongo na wauaji.

Herode anawaagiza Majusi kwamba, “waende huko wakamwabudu kisha warudi wamweleze kusudi naye aende kumwabudu.” Ama kweli wadanganyifu na waongo tu ndiyo wanaoweza kutetea ulimwengu na utawala wa kale, kwa vile wanaogopa mwanga mpya. Wao wanafanya kazi katika giza. Wenye mamlaka hata ya kisiasa au serikali ya kiraia hakuwezi kuwa watu wa ukweli, daima waongo na wadanganyifu. Kadhalika, kutokana na kuchefuka nyongo Herode anaamua kuwaua watu wake na watoto wasio na hatia.

Katika mazingira hayo mwanga wa nyota hauwezi kung’ara. “Funika kikombe mwanaharamu apite.” Ndiyo maana Majusi wanapoondoka na kutoka nje ya mji mara moja wanaiona tena ile nyota na kwamba: “Walipoiona tena nyota wakapata furaha kubwa sana.” Ile nyota ikasimama pangoni juu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kumeshafanyika utafiti na kutolewa maelezo mengi na mazuri juu ya zawadi walizozitoa Majusi kwa mtoto Yesu. Lakini tuone kifupi utafiti wa kibiblia juu ya zawadi hizo dhahabu, ubani na manemane.

Katika Biblia Waisraeli wanatambulika kuwa ni taifa la kifalme, la kikuhani (mapadre) na la bi-arusi (Israeli wa kike) wa Bwana. Zawadi tatu zinawakilisha sifa hizi tatu Waisraeli. Sifa hizo sasa zinaelekezwa kwetu wapagani – yaani wote tunaopokea mwanga wa nyota hii. Ufalme huo sasa umetolewa kwetu nasi taifa la ufalme mpya tunamtolea Bwana dhahabu. Ubani ulitolewa na makuhani. Sasa hata sisi tunaifukizia ubani hiyo nyota.Kwa hiyo sisi au Kanisa ni taifa la kikuhani. Manemane  au marashi anajipaka bi arusi, tazama Wimbo ulio Bora unaonukuliwa mara nyingi. Manemane ni alama ya harufu ya upendo wa bi arusi. Hivi sasa bi arusi siyo tu waisraeli bali sisi binadamu wote ni bi arusi wapendwa na Bwana. Majusi we achana nao hawa ni moto wa kuotea mbali!

Heri kwa sikukuu ya epifania.

Na Padre Alcuin Nyirenda OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.