2016-01-04 10:50:00

Watawa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, tunakusalimu kutoka katika studio za Radio Vatican tukisema Tumsifu Yesu Kristo na heri kwa Mwaka Mpya 2016. Tunawatakieni nyote baraka tele za Mwenyezi Mungu kwa mwaka mzima na nyakati zote. Sote tuombeane na kubarikiana kwa Andiko lile tulisomalo katika Kitabu cha  Hesabu tukisema “BWANA akubarikie, na kukulinda; akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; akuinulie uso wake, na kukupa amani.” Hesabu 6:24-26.

Mpendwa msikilizaji, katika mwaka huu tunasafiri na maadhimisho mawili ndani ya Kanisa. Mosi, bado tukingalimo katika maadhimisho ya Mwaka wa watawa duniani, ambao tutauhitimisha hapo tarehe 2 Februari 2016, katika Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni ambayo pia ni Siku ya Watawa Duniani kama ilivyoasisiwa na MtakatifuYohane Paulo II.

Na papo hapo tutaendelea na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, unaoongozwa na kauli mbiu: Misericordes sicut Pater, yaani “Iweni na huruma kama Baba” ambapo Baba Mtakatifu Francisko anatualika sote kuikimbilia na kuiambata huruma ya Mungu; mwaliko wa kuwa na huruma kama Baba wa Mbinguni.

Tunapoyaunganisha hayo mawili, tukumbuke kwamba, hata uwepo wa watawa ndani ya Kanisa, nao  pia ni mpango wa huruma ya Mungu. Mungu anatenda kazi za huruma na upendo kwa watu wake kwa njia ya watawa. Ndiyo maana tunasema, watawa wameitwa kuimwilisha huruma ya Mungu kwa njia ya maisha na kazi zao.

Sote twashuhudia katika nyakati zetu hizi katika mazingira mbalimbali, jinsi ambavyo watawa wanajimega na kujimaliza kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu katika nyanja mbalimbali za maisha. Ndiyo maana kama waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tunaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Utawa, kuwaombea watawa wetu, kuwapatia mazingira bora ya kutuhudumia kwa kuwahakikishia amani na usalama. Zawadi yoyote ni vema itunzwe vizuri. Nasi sote tunapotunza vizuri zawadi ya utawa na watawa katika Kanisa, hapo tutakuwa tunamtukuza Mungu aliyetujalia zawadi hii.

Leo mpendwa msikilizaji, tunaendelea kuchambua juu ya utawa na maisha ya kitawa kwa kujiuliza swali la msingi: Katika maadhimisho haya ya Mwaka wa watawa duniani, ulimwengu unaachiwa chapa gani? Haitoshi tu kwamba, watawa wanatuhudumia kwa namna mbalimbali! Ni vema kuona hawa watu wanatufundisha nini!

Tutakumbuka kwamba, maisha ya kitawa ndani ya Kanisa yanajipambanua kwa karama mbalimbali kadiri waanzilishi wa mashirika hayo walivyovuviwa na Roho Mtakatifu. Lakini jambo la juu kabisa linalounganisha mashirika hayo mbalimbali, ni ile roho ya kutaka kujikamilisha zaidi katika safari ya Ukristo kwa kuambata mashauri ya Injili na ufuasi tikitiki kwa Kristo.

Ndani ya maisha ya kitawa, wapo watawa ambao kwa mujibu wa asili yao huishi katika jumuiya, wakiongozwa kwa kanuni maalumu ya maisha ya pamoja yenye kufafanua roho ya Injili na chini ya uongozi maalumu. Muungano huo wa kijumuiya ni mfano wa Kanisa linalosafiri kuelekea makwetu ya mbinguni, ambamo waamini wanapiga mbio kwa msaada wa Neno, Sakramenti, Mafundisho ya Kanisa na taratibu maalumu; pamoja na kwa msaada wa waamini wenzao, wanakaza mwendo kuelekea ukomo wa hija yetu, yaani muungano na Mungu. Mtakatifu Augostino Askofu na Mwalimu wa Kanisa analisema kusema, roho ya mwanadamu haiwezi kutulia hadi pale itakapoungana na Muumba wake!

Maisha ya jumuiya ni sadaka na yataka moyo kweli kweli! Ambapo kila mmoja anayasadaka mapendeleo yake binafsi, anajitoa kwa ajili ya kuujenga, kuuendeleza na kuuenzi muungano wa kijumuiya pamoja na wengine, kwa ajili ya mafaa yao binafsi na mafao mapana ya Kanisa na ya Familia nzima ya Mungu.

Katika maisha hayo, kwa mwangwi wa vifungo vya Injili, mtawa anausadaka uhuru wake, ili kwa utii mnyoofu na mfurahivu ajitoe ili kumtukia Mungu tu kwa njia ya huduma mbalimbali kadiri anavyotumwa na wakubwa halali wa Shirika lake. Katika utawa, mtawa anajisadaka pia hata haki zake asilia, kwa kuyaambata maisha ya useja mtakatifu, kwa kujikatalia haki ya ndoa na watoto, ili kuwa na muda mwingi zaidi wa kuwahudumia watu wa Mungu popote pale duniani na wakati wowote, na katika mazingira yoyote, pasipo kufungwa na wajibu msingi wa kifamilia.

Katika utawa, mtawa pia anajinyima haki na uhuru ya kujitafutia na kujimilikisha mali binafsi. Kwa kufuata mashauri ya Injili, mtawa anauambata ufukara mtakatifu, ili katika roho hiyo ya ufukara na kujinyima, pasi na kujing’ang’amanisha na mali, ajitoe katika utajiri wote wa nafsi, akili, mwili na roho ili kumtumikia Mungu katika ukamilifu wote, huku akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa fukara ili kwa njia ya maskini aweze kuwapata wote!

Hao ni watawa katika undani wao! Tunarudi katika swali letu! Watawa wanatuachia nini katika maisha yetu sisi waamini? Watawa wanatuambia nini? Kwa leo, kamata haya machache.

Mosi, watawa wanatufundisha roho ya udugu na umoja: Katika ulimwengu wetu huu uliovamiwa na roho ya ubinafsi, ule udugu wetu wa kibinadamu unaelekea kutoweka. Wengi tunaelekea kujipendelea sisi wenyewe tu, bila kuguswa na mahitaji ya jirani. Roho ya mimi nipate – wote wakose, au tukose wote, ndiyo inaelekea kuwa falsafa ya maisha. Uaminifu na kuaminiana kunatoweka, kila mtu anaelekea kuwa na wasiwasi na mwenzake. Chuki dhini ya utu wa mtu na ubinadamu inaelekea kupamba moto, hali inayojipambanua katika misigano mingi na isiyokoma ya kifamilia na kijamii kwa ujumla, vitendo vya kigaidi na kupenda kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Udugu na mshikamano wetu wa kibidamu umeingia dosari kubwa!.

Tufanye nini basi? Watawa wanatupa mwanga. Kila mmoja wetu aitikie wito wa kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuanza kwanza kabisa kujitakatifuza sisi wenyewe. Kutakatifuza mawazo yetu: yaani namna zetu za kufikiri, ili tuweze kujiwazie sisi wenyewe mema na kuwawazia wengine mema; tutakatifuze midomo yetu, ili daima itoe kauli njema zenye kujenga amani katika ya watu: tutakatifuze matendo yetu, ili  kuweza kuwa wajenzi wa madaraja ya watu kukutana na kuishi kwa amani na upendo.

Pili, watawa wanatufundisha kujisadaka kwa ajili ya wengine: Katika ulimwengu wetu huu uliovamiwa na watu wabinafsi, wenye kujifikiria wao wenyewe tu, bila kuguswa na shida za wengine, hadi kufikia kuhalalisha mifumo-dhambi ya maisha yenye kulinda maslahi binafsi, tunahitaji roho hiyo ya kuona kwamba, kila mmoja anawajibu juu ya hali njema na usitawi wa jirani.

Ili kuweza kujenga kweli jumuiya ya watu wanaoishi kwa amani na upendo, ni mwaliko kwa wote kujisadaka, kujitoa, kujimega, kujimaliza kwa ajili ya mafao mapana ya wote. Jisadake maelekeo yako hasa yale yanayoleta ukakasi katika maisha ya wengine, yasadake mapendeleo yako kwa ajili ya usitawi wa jirani, jisadake hata uhuru wako, kwa kufuata vema taratibu za jamii unamoishi, kwa ajili ya kujenga mafao ya wote.

Tatu, watawa wanatufundisha kujibidisha katika kumtafuta, kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu. Mpendwa msikilizaji, safari ya kumwendea Mungu ni ndefu, ina kona nyingi, utelezi na makorongo wakati mwingine. Ili kusafiri salama, tunahitaji kuwa makini, kuwa na bidii ya moyo, kujitoa kikamilifu bila ya kujibakiza, tukijibidisha huku tukitegemea msaada wa Mungu peke yake. Safari hiyo isindikizwe kwa sala, kusoma na kuyajifunza maandiko matakatifu, kujifunza mafundisho tanzu ya Kanisa, kuambata matendo ya huruma kiroho na kimwili; huku tukikumbuka kwamba, tumeitwa ili tuwe chumvi na nuru ya dunia.

Tunatia nanga ya makala hii kwa siku ya leo tukisema, watawa ni hazina katika Kanisa, wanaomwilisha huruma na upendo wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu! Tukutane tena kipindi kijacho panapo majaaliwa. Kukuletea makala hii kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.