2016-01-04 08:28:00

Uzinduzi wa Parokia ya Mt. Francisko Xavieri, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, Africae munus anakazia umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kuwekeza katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ili kusaidia kuwafunda vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano ndani ya jamii, changamoto kubwa kwa Kanisa Barani Afrika! Hii ni nafasi pia ya kuhakikisha kwamba, vijana wanafundwa vyema kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa; kwa kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuleta amani na utulivu ndani ya jamii sanjari na kuunda mioyo ya vijana wa kizazi kipya katika mwanga wa Injili.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Askofu mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, hivi karibuni amezindua Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko Xavier iliyoko Chuo kikuu cha Dodoma na kumsimika Padre Magnus Tegete, C.PP.S. Mmissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kuwa Paroko wa kwanza katika Parokia hii na kwamba, Parokia hii, itahudumiwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Jumuiya ya nyumba ya Malezi ya Miyuji, ambayo itakuwa ni makazi ya muda!

Akizungumza kwa niaba ya Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Kanda, Shirika la Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania, amemshukuru kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya kwa kuamua kuunda Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko Xaveri na kuamua kuwakabidhi Wamissionari wake kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa utume kwa vijana, amana na jeuri ya Kanisa  katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Huu ni mwendelezo wa ndoto ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanapoendelea kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia mbili tangu Shirika hili lilipoanzishwa na kwa namna ya pekee, Kanisa linapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya licha ya kutambua changamoto zilizopo kwenye Chuo kikuu cha Dodoma, ameamua kuanzisha Parokia mpya ili kusogeza huduma za maisha ya kiroho kwa wanafunzi wanaoishi na kusoma Chuoni hapo pamoja na maeneo ya jirani. Uwepo wa idadi kubwa ya waamini Chuoni hapo ni sababu tosha kabisa ya kuanzishwa kwa Parokia mpya. Waamini hawa wanapaswa kumshuhudia Mungu katika ukweli na maisha ya kiroho. Hii ni fursa makini kwa waamini hao kuwa mashuhuda wa imani inayoungamwa, inayoadhimishwa, inayomwilishwa katika Amri za Mungu na kushuhudiwa katika maisha ya sala yanayojikita katika matendo ya huruma, changamoto pevu wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Historia ya Parokia hii inayoundwa na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma ilianza kunako mwaka 2009 kwa kupitia hatua mbali mbali hadi kufikia uamuzi wa kuwa ni Parokia kamili kunako mwaka 2015. Parokia hii inaundwa na vigango sita na kwamba, ina waamini 4, 311 idadi inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Dodoma. Parokia hii inaundwa na vyama vya kitume kumi na viwili, vinavyoshiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Parokia hii imezinduliwa chini ya uongozi wa ndugu Deodatus Chaula kama mwenyekiti akisaidiwa na viongozi wengine wanne kutoka Chuo kikuu cha Dodoma. Parokia ina rasilimali ya kuiwezesha kusonga mbele kwa siku za usoni. Pamoja na mambo mengine, Parokia inapenda kujielekeza zaidi katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, maisha ya Sala pamoja na ushuhuda wa maisha yanayoambata huruma na upendo wa Mungu. Parokia hii inataka kuendelea kujipambanua kuwa ni kitovu na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Parokia inatambua changamoto zilizoko mbele yake hasa katika mikakati ya kulitegemeza Kanisa kwani sehemu kubwa ya waamini wa Parokia hii ni wanafunzi wanaotegemea kwa kiasi kikubwa msaada kutoka kwa wazazi na walezi wao. Waamini wengi wa Parokia hii ni watu wenye makazi ya muda kulingana na kazi zao. Bado wanakabiliwa na deni la kugharimia ununuzi wa kiwanja kwa ajili ya maendeleo ya Parokia kwa siku za usoni. Usafiri bado ni tatizo kubwa kwa waamini wanaoishi kwenye kitivo cha elimu, ili kuweza kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu.

Licha ya changamoto zote hizi, waamini wa Parokia ya Mtakatifu Francisko Xaveri wanapenda kujikita kikamilifu katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa njia ya: Katekesi makini, semina na makongamano pamoja na kuendelea kuimarisha umoja, upendo na mshikamano kati ya waamini wa Parokia hii, ili kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.