2016-01-04 09:40:00

Tambueni uwepo wa Mungu katika maisha yenu ya kila siku!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iliyozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kugundua hazina iliyofichika ndani mwao, yaani uwepo wa Mwenyezi Mungu anayeandamana na watu wake katika hija ya maisha yao ya kila siku, hadi ukamilifu wa nyakati! Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa wema na ukarimu wake anaoendelea kuwajalia waamini kila siku ya maisha yao, mwaliko wa kuwa kweli ni mashuhuda wa uwepo wa Mungu katika maisha yao, kwa njia ya unyenyekevu!

Hivi ndivyo anavyosema Askofu Maurice Piat wa Jimbo Katoliki la Port-Louis, lililoko nchini Mauritius, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni fursa makini kwa waamini kuweza kusoma historia ya maisha yao, ili kugundua uwepo wa ushuhuda wa huruma ya Mungu unaotolewa na watu wanaokutana nao kila siku ya maisha, huku wakiwaonesha ile Sura ya Mungu mwenye huruma na mapendo. Hapa waamini pia wanahamasishwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika safari ya maisha yao ya kila siku, kwa kutambua kwamba, wema na utakatifu ni mapambano ya kila siku.

Askofu Piat anaendelea kukaza kwamba, Mwenyezi Mungu anamjalia mwamini fursa ya kufanya mabadiliko ya ndani katika maisha yake kwa kujikita katika uhuru kamili na wala hakuna shuruti. Mwamini akiambata mwanga wa matumaini anayokirimiwa na Mungu, anaweza kutumia vyema nguvu ya upendo iliyoko ndani mwake, ili kumwimarisha na kumpatia furaha inayomwezesha kusonga mbele hata wakati wa nyakati za shida na magumu katika maisha. Uwepo wa Mungu katika maisha ya waamini ni chemchemi ya ujasiri, kwani Kristo Yesu kwa njia ya unyenyekevu wake, anaendelea pia kufanya hija ya maisha na waamini wake.

Askofu Piat anaendelea kufafanua kuhusu umuhimu wa familia ya binadamu kama shule ya utakatifu, haki na amani; upendo, huruma na mshikamano wa dhati; familia ni shule ya Injili ya huruma na msamaha; tunu msingi ambazo zinafumbatwa katika Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Pale ambapo familia ya binadamu inaonesha hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wanafamilia, matokeo yake ni mauaji, nyanyaso na dhuluma zinazofanywa kwa sababu mbali mbali.

Hiki ndicho chanzo kikuu cha uwepo wa makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kiwe ni kipindi cha kumwilisha Injili ya furaha katika maisha ya waamini; furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, tayari kuwashirikisha jirani kwa njia ya matendo ya huruma! Maadhimisho haya yajenge msingi wa utamaduni wa kumwilisha huruma ya Mungu hata baada ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwani huduma ya huruma, upendo, msamaha na upatanisho ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya familia ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.