2016-01-04 08:14:00

Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 ni moto wa kuotea mbali!


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, Jimbo kuu la Cracovia, Poland ni moto wa kuotea mbali, ikizingatiwa kwamba, ni Siku ambayo inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hadi kufikia tarehe Mosi, Januari 2016 vijana nusu millioni wamekwisha jiandikisha, tayari kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kutoa mwelekeo wa pekee kwa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana.

Jimbo kuu la Cracovia limekwishatenga eneo ambalo linaweza kumudu kutoa hifadhi kwa vijana zaidi ya millioni tano. Waratibu wa Siku ya Vijana Duniani wanasema, hatua ya kwanza imekwishafikiwa na kwamba, wanaendelea kukamilisha maandalizi, ili kuwapatia vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia nafasi ya kushuhudia jeuri ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Maadhimisho haya ambayo yatamshirikisha kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu Francisko, yataanza kutimua vumbi hapo tarehe 25 hadi tarehe 31 Julai 2016.

Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, vijana kutoka Italia ni kundi linaloongoza katika orodha hii, kumbe, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kuhamasishwa ili kujiandikisha mapema kwa kupitia majimbo na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki. Kambi ya huruma ya Mungu ni eneo maalum litakalotumika wakati wa mkesha wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.