2016-01-02 09:39:00

Waethiopia millioni 10. 2 wanakabiliwa na baa la njaa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia katika mkutano wake wa kawaida wa 38 uliohitimishwa hivi karibuni limepembua kwa kina na mapana hali ya usalama wa chakula na tatizo la njaa kali inayowakabili wananchi wa Ethiopia wapatao millioni 10. 2. Hawa ni watu ambao wameathirika kutoka na ukame wa muda mrefu ambao kwa sasa unatishia maisha ya watu na mifugo. Maaskofu Katoliki Ethiopia wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Ethiopia hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

“Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha”. Hii ndiyo kauli mbiu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Ethiopia ambao wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linapenda kuungana na wadau mbali mbali katika kuwahamasisha Wasamaria wema kugusa na mahangaiko ya wananchi wa Ethiopia wakati huu wanapokabiliwa na baa la njaa ambalo halijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anakaza kusema, waathirika wa mabadiliko ya tabianchi ni watu wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani, hawa ndio wale akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi. Hili ni kundi kubwa la jamii linalotegemea ustawi na maendeleo yake kutokana na mazingira na ekolojia, ili kushiriki katika shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi. Nchi Maskini hazina uwezo wala rasilimali fedha na teknolojia ili kudhibiti athari za mabadililo ya tabianchi, kumbe zinahitaji kuonjeshwa upendo na mshikamano unaojikita katika kanuni auni.

Baa la njaa nchini Ethiopia ni kubwa. Inakadiriwa kwamba, kunahitajika walau kiasi cha dolla za kimarekani billioni 1. 4 ili kupambana kikamilifu na baa la njaa pamoja na utapiamlo wa kutisha nchini Ethiopia. Serikali ya Ethiopia kwa kushirikiana na wadau mbali mbali inaendeleza mchakato wa kutafuta fedha ili kuweza kudhibiti baa hili kabla halijasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kanisa Katoliki Ethiopia kwa kushirikiana na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa na Kitaifa linaendelea kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia wananchi waliokumbwa na baa la njaa nchini Ethiopia.

Maaskofu wanakaza kusema, mchakato wa kudhibiti baa la njaa nchini Ethiopia pamoja na mambo mengine ya kuokoa maisha ya watu wengi, lakini pia unalenga kuziimarisha familia kutosambaratika kutokana na baa la njaa; kuokoa kundi kubwa la vijana linaloweza kujikuta limekata tamaa na hivyo kuamua kukimbia nchi na hivyo kuhatarisha maisha zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo kikubwa cha vita, maafa, kinzani na mipasuko ya kijamii. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 821, 400 ambao hawana makazi maalum kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan mafuriko na ukame wa kutisha.

Baa la njaa lisipodhibitiwa kikamilifu familia zitasambaratika na vijana wengi watazamia Ulaya ili kutafuta usalama na ubora wa maisha wanasikitika kusema Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia. Wadau mbali mbali wanapaswa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, baa la njaa linadhibitiwa kwa kupata chakula cha msaada, kwa kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko pamoja na kulinda mifugo ambayo ni rasilimali inayotegemewa na wafugaji wengi kwa ajili ya kipato chao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linawahamasisha wadau mbali mbali kuunga mkono jitihada hizi ili kuokoa maisha ya wananchi wengi wa Ethiopia ambayo kwa sasa yako hatarini. Ombi hili la msaada wa dharura limetiwa sahihi na Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.