2016-01-02 08:40:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Tokeo la Bwana!


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama Epifania kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari. Hii ni siku pia ya Utoto Mtakatifu, shule ya upendo, huruma, ukarimu na umissionari miongoni mwa watoto wadogo. Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Jumapili hii kwa baadhi ya majimbo kutokana na sababu za kichungaji, ili kuwapatia waamini wengi zaidi nafasi ya kulitafakari Fumbo la mwanga katika maisha yao ya kila siku, tayari kuushuhudia Mwanga wa Mataifa ambaye ni Yesu Kristo, hususan mwaka huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali huku wakiongozwa na nyota walifika mjini Bethlehemu, wakamsujudu Bwana na kumtolea zawadi kuu tatu zinazofumbata maana na utume wa Yesu Kristo hapa ulimwenguni. Ubani unadhihirisha Umungu wa Kristo; Dhahabu inatangaza Ufalme wa Kristo na Manemane inaonesha ubinadamu wa Kristo unaokabiliwa na Fumbo la mateso, kifo na ufufuko.

Huu ndio ufunuo wa Kristo kwa mataifa, dhamana inayoendelezwa pia na Mama Kanisa kwa wale wote wanaomtafuta Kristo kwa moyo mnyofu, ili kwa njia ya imani, waweze kutambua ukuu wake unaofumbatwa katika umaskini na unyenyekevu mkuu, tayari kumwabudu na kumwabata katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kwa kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya: Kanisa, Neno, Sakramenti na matukio mbali mbali ya maisha, waamini waweze kuonja furaha, amani na utulivu wa moyo. Yesu ni ukweli, matumaini na wokovu wa watu wake.

Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana kwa mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yajikite zaidi katika maisha ya kiroho yanayojidhihirisha zaidi katika  imani inayoungamwa; imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa, imani inayoongoza maisha ya waamini kwa kuambata Amri za Mungu na imani inayomwilishwa katika sala inayojielekeza zaidi katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; toba na wongofu wa ndani msingi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kumtambua Yesu Kristo katika Neno, Sakramenti na zaidi kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Tokeo la Bwana liguse na kupyaisha hija ya maisha ya mwamini! Baada ya utangulizi huu, sasa ninakualika ujiunge na Padre Richard Tiganya anayezama zaidi katika tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Tokeo la Bwana.

Ninakuleteeni kwa furaha ujumbe wa Neno la Mungu tunaposherehekea sherehe ya Epifania ambayo huadhimishwa kila terehe 6 Januari katika kipindi cha Noeli. Ni sherehe ambayo Mfalme Masiha anajitambulisha wazi kwa ulimwengu. Ni kwa njia ya nyota, Mamajusi wanaweza kufika mahali alipokuwa na wakaweza kumsujudia na kumpatia zawadi zao. Kumbe Yesu Kristu Masiha ni nyota inayaangaza na kuongoza maisha yetu mpaka mwisho wa nyakati hadi tufike mbinguni.

Katika somo la kwanza tunaona jambo la ajabu na zuri likitokea. Nabii Isaya yuko katika ndoto anaona Yerusalemu iliyokuwa imeharibiwa kwa sababu ya vita na mapigano mbalimbali miaka 600 hivi kabla ya Kristu sasa inakuwa chanzo cha nuru, na utukufu wa Mungu unaonekana juu yake. Mataifa wakiwakilishwa na Mamajusi wanaijia nuru hiyo. Nabii Isaya anaimba akisema “inua macho yako Yerusalemu utazame pande zote za dunia, wote wanakusanyana; wanakujia wewe” Ni wimbo wa sifa kwa Yerusalemu, ni kielelezo cha kuzaliwa Masiha na kwamba atakuwa nuru angavu kwa ulimwengu na mataifa yote watakusanyika kumsujudia na kumtolea zawadi. Habari na uaguzi huu tunauona vema katika Injili ambapo tunawaona Mamajusi wakitokea pande zote za dunia kwa ajili ya kuja na kumsujudia Bwana aliyezaliwa, nyota ya mataifa, nyota ya milele.

Katika somo la pili Mtume Paulo anapowaandikia Waefeso anawaambia juu ya kufunuliwa siri za Mungu kwa njia ya Mitume. Anasema ni kwa njia ya Manabii na Mitume na si wanadamu katika vizazi vingine Mungu amefunua siri yake. Hata hivyo pamoja na kupewa siri hiyo bado mataifa mengine wanashiriki pamoja nasi ahadi ya Bwana ya kurithi ufalme wake. Hivi neno la Mungu linatualika kutambua kuwa sisi sote tuliobatizwa na kupokea mataji matakatifu tumeshirikishwa katika ukoo wa kikuhani kwa ajili wokovu wetu na wokovu wa ulimwengu.

Katika Injili tunapata kuona ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya Mamajusi, wamefika kwa mfalme Herode na wanamwuliza yuko wapi Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumsujudia. Herode anashangaa kwa kufadhaika na anauliza habari kwa wakuu wa makuhani na waandishi Kristu azaliwa wapi? Wanamjibu, amezaliwa Betlehemu. Anawaagiza Mamajusi wakati wakishamwona wamletee habari, ili naye akamsujudie! Mamajusi hawa wanaongozwa na nyota mpaka pale alipo mtoto na hawatarudi kwa Herode kwa sababu Herode anayo nia ya kutaka kumwangamiza Mwana wa Mungu.

Mamajusi wako katika msingi uleule wa Nabii Isaya anaposema Yerusalemu ikiangaza watu wote watakuja na kumiminika katika mji. Kumbe, Mamajusi wanatimiza ule uaguzi wa Nabii Isaya, wanaleta manemane, dhahabu na uvumba. Mamajusi ni kiwakilishi cha watu wote wanaokubali kuongozwa na ujumbe wa amani, ujumbe wa Yesu Kristu Masiha yaani nyota, nuru ya ulimwengu. Ni alama ya Kanisa lililo jumuiya ya watu wenye chimbuko moja yaani Mungu, lakini lugha, tamaduni, umri, kabila tofauti. Watu hawa wote wako mbele ya nyota angavu ndiye Mkombozi aliyezaliwa.

Mpendwa, unaalikwa basi leo na Neno la Mungu kujiweka chini ya maongozi ya Nyota angavu, nyota ya milele ndani ya Kanisa Familia ya Mungu. Ninakutakieni heri na baraka za Mungu, ukazidi kuongozwa na Kristo mwenyewe, daima ukampe hazina stahili kama Mamajusi kwa sifa na utukufu wa Mungu na pia kwa wokovu wako. Heri na baraka kwa wale walio na majina ya Epifania na majina ya Mamajusi yaani Gaspar, Melkiori na Barthazari. Mkakomae katika kusujudu na kumtolea Mungu vipaji na karama zenu kama kielelezo cha kuongozwa naye katika maisha yenu.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.