2016-01-02 14:46:00

Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza!


Mapambano dhidi ya baa la njaa duniani na utapiamlo wa kutisha sanjari na kuambata ekolojia na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mintarafu Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko, Laudato si, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni muhimu sana katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, chanzo kikuu cha umaskini, njaa na utapiamlo. Huu ni mwaliko wa kuendelea kukazia umuhimu wa kilimo bora, mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza.

Hii ni changamoto iliyopembuliwa hivi karibuni na viongozi wakuu kutoka Vatican katika tukio lililofanyika kwenye Chuo kikuu cha “Santa Croce”, kilichoko hapa mjini Roma. Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Roma, yaani, FAO, WFP na IFAD amechambua kwa kina na mapana Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama nyenzo muhimu sana katika kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa binadamu, maendeleo na mafao ya wengi.

Huu ni mchakato wa kupambana na umaskini, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha mambo yanayosababishwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha upendo na mshikamano unaosimamiwa na kanuni auni, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Hapa Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kudumisha mafungamano ya kijamii kwa kuwa na matumizi bora ya mazingira, nyumba ya wote kwani mazingira yanagusa na kutikisa medani mbali mbali za maisha ya binadamu kama vile: kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika maisha ya kiroho.

Monsinyo Fernando Chica Arellano anaendelea kufafanua kwamba, ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuna haja ya watu kujikita katika wongofu wa kiekolojia; kwa kuanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, jamii na hatimaye katika ngazi ya kimataifa. Uzalishaji viwandani pamoja na kilimo ni mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, kwa kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira.

Hii ina maana kwamba, sera za kilimo endelevu zinapaswa kuangaliwa na kushuhughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa, ili kupambana na matumizi mabaya ya rasilimali ardhi kwa kuzalisha nishati uoto badala ya kutumia ardhi kwa uzalishaji wa mazao ya chakula ili kupambana na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea pia kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato.

Kumbe, mapambano ya baa la njaa na umaskini anasema Baba Mtakatifu ni kwa ajili ya kumrudishia binadamu utu na heshima yake, kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na kumjenga uwezo wa kutunza mazingira nyumba ya wote! Sera na mikakati ya pamoja ni muhimu sana kwani athari za mabadiliko ya tabianchi hazibagui wala kuchagua, ndiyo maana kuna haja ya kuwa na sheria, kanuni na taratibu zinazotekelezeka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hapa pia lazima Jumuiya ya Kimataifa iandae mikakati ya kilimo endelevu, kwa kupambana dhidi ya kuenea kwa jangwa, kwa kuwa na nishati mbadala pamoja na kuhakikisha kwamba, misitu na rasilimali mbali mbali za dunia zinatumika kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, anakazia umuhimu wa mchakato wa majadiliano katika ngazi mbali mbali; umuhimu wa kupambana na rushwa pamoja na ubadhirifu wa mali ya umma; watu kuachana na uchu wa mali na madaraka mambo yanayowatumbukiza wengi katika vita na mafarakano ya kijamii. Mkazo uwekwe kwenye siasa bora, sera za mageuzi ya taasisi mbali mbali pamoja na kuwa na matumizi bora ya rasilimali za nchi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Majadiliano yajikite katika ukweli na uwazi kati ya wachumi na wanasiasa ili kwa pamoja kuweza kuangalia baa la umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kuchukua hatua zinazofaa katika kurekebisha hali hii kwa mafao ya wengi. Kuna haja ya kuendeleza majadiliao kati ya sayansi na dini ili kuwawezesha waamini kuwa na sera pamoja na mikakati itakayowasaidia kuwa ni watunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote; kwa kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu, kwa ajili ya utu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Monsinyo Fernando Chica Arellano anakaza kusema, ubinafsi na uchoyo ni sumu kubwa katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa dhati katika mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa na uchafuzi wa mazingira. Hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko watu wabadili tabia na mienendo yao, ili kukabiliana na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Watu wakishirikiana kwa dhati, kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, lakini kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake atekeleze wajibu wake barabara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.