2016-01-02 08:55:00

Bikira Maria ni Mama wa Mungu, Msamaha, Huruma, Neema na Furaha!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila tarehe Mosi, Januari, Jioni, ameadhmisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kufungua Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko mjini Roma. Ibada hii imehudhuriwa na maelfu ya waamini waliokuwa wamefurika ndani na nje ya Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amewakumbusha waamini sala inayomwelekea Bikira Maria kuwa ni Mama wa Huruma ya Mungu; Mama wa Mungu, Mama wa msamaha; Mama wa neema na Mama aliyejaa furaha takatifu. Huu ni muhtsari wa imani kwa Bikira Maria, ambaye waamini wanamkimbilia kwa ajili ya maombezi na kupata faraja.

Bikira Maria zaidi ya yote ni Mama wa Huruma ya Mungu na kwamba, Lango lililofunguliwa ni Lango la Huruma ya Mungu, kila mwamini anayepitia katika Lango hili anapaswa kuambata upendo wa huruma ya Mungu, akiwa na matumaini pasi na wasi wasi wala mashaka kwa kupitia Lango hili atambue kwamba, atasindikizwa na Bikira Maria katika hija yake ya maisha hapa duniani.

Bikira Maria ni Mama wa Huruma ya Mungu kwani amemzaa Yesu, ambaye ni Uso wa huruma ya Mungu; Emmanueli, aliyetumainiwa na wengi; Mfalme wa amani. Huyu ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili ya wokovu wa binadamu na kuwapatia Bikira Maria, ili aweze kufanya hija pamoja nao, bila kuwaacha pweke katika safari ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi, hususan wakati wa mashaka na magumu ya maisha.

Bikira Maria ni Mama wa Mungu anayesamehe na kutoa msamaha na kutokana na sifa hii, Bikira Maria anaweza kuitwa kuwa ni Mama wa huruma. Neno huruma linapata chimbuko na ni tunda la imani ya Kikristo. Kwa mwamini asiyefahamu kusamehe huyo bado hajafahamu maana ya utimilifu wa upendo. Anayependa kwa dhati ana uhakika wa kufikia utimilifu wa upendo pamoja na kusahau ubaya aliotendewa.

Chini ya Msalaba, Bikira Maria alishuhudia maana ya mateso na kuona jinsi ambavyo Mungu anavyopenda kwa dhati; akasikia maneno ya Msamaha kutoka kwa Kristo Yesu, akimwomba Baba yake awasamehe watesi wake kwani walikuwa hawajui wanalolitenda. Tangu wakati ule, Bikira Maria akawa ni Mama wa msamaha, akabahatika kupata neema kutoka kwa Mwanaye mpendwa, kiasi hata cha kuwasamehe watesi wa Mwanaye  ambaye hakuwa na hatia.

Kanisa kwa upande wake linakuwa ni chombo pia cha msamaha kwa wale wote wanaokimbilia huruma ya Mungu. Msamaha uliotolewa pale Mlimani Golgota hauna mipaka kwani unawaambata watu wote kama ambavyo linapaswa kufanya Kanisa, kwa kuiga mfano wa Kristo Yesu pale Msalabani na Bikira Maria chini ya Msalaba na kwamba, hapa hakuna mbadala. Mitume wa Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu wamefanyika kuwa ni vyombo muhimu vya huruma ya Mungu kwa watu wote na kila mahali.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matumaini, neema na furaha takatifu ni fadhila kutoka kwa Kristo zilizoandikwa mwilini mwake, kwa Bikira Maria kuwapatia walimwengu zawadi ya Mwanaye mpendwa, ili kuwakirimia msamaha unaopyaisha maisha yao, ili hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu, chemchemi ya furaha ya kweli kwa mwamini mwenye matumaini katika wokovu unaoletwa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, nguvu ya msamaha ni nyundo inayobomoa masikitiko, machungu ya moyoni na hali ya kutaka kulipiza kisasi. Msamaha ni mlango wa furaha na utulivu; ni chemchemi ya maisha mapya dhidi ya mawazo ya kifo. Machungu ya moyoni na tabia ya kulipiza kisasi yanaongeza masikitiko katika maisha ya mwanadamu, kiasi cha kumnyima mapumziko na amani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupitia katika Lango la Huruma ya Mungu, wakiwa na uhakika wa kusindikizwa na Bikira Maria Mama wa Mungu anayewaombea pia; ili hatimaye, waweze kugundua uzuri wa kukutana na Mwanaye Yesu Kristo. Waamini wafungue wazi malango ya mioyo yao ili furaha ya msamaha na matumaini iweze kuingia ndani mwao, tayari kuwajalia nguvu ya kuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu. Kwa maneno ya Mababa wa Mtaguso wa Efeso, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumshangilia Bikira Maria Mama wa Mungu kwa moyo na upendo wao wote!

Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu alikwenda kwenye Kikanisa ambacho kinahifadhi ya Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus Popoli Romani” akafungua mlango wake na kusali kwa kitambo kidogo. Baadaye, Baba Mtakatifu alitoka nje ya Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma ilikusalimiana na waamini pamoja na mahujaji waliokuwa wamefurika kwenye viwanja vya Kanisa hili, ili kumshukuru Bikira Maria Mama wa Mungu.

Amewatakia wote heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2016, uwe ni mwaka unaosheheni huruma ya Mungu inayosamehe yote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia Kristo malango ya mioyo yao, ili furaha na msmaha wa Mungu uweze kuingia na kupata makazi kwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.