2016-01-01 10:09:00

Waamini iweni mashuhuda wa imani, ukarimu, udugu na amani!


Baba Mtakatifu Francisko ameufunga Mwaka 2015 kwa Ibada ya Masifu ya jioni katika Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu; akaongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Te Deum. Baba Mtakatifu alipata pia nafasi ya kwenda kutembelea Pango la Mtoto Yesu lililoko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema, tangu karne ya nne, Mama Kanisa amekuwa akimwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kutambua uwepo wake katika matukio mbali mbali ya kihistoria. Kanisa linafahamu fika kwamba, wakati mwingine maneno hayatoshi, ndiyo maana linaomba pia kupata nguvu kutoka kwa Watu wote wa Mungu, ili kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani. Katika utenzi wa “Te Deum” Kanisa linawaalika Malaika, Manabii na Viumbe vyote kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa ajili ya mpango wa Mungu, ambamo mwanadamu anagundua pia muhtasari wa maisha yake katika kipindi cha mwaka mzima uliopita.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Mama Kanisa anamwomba Kristo, ili aweze kuwajalia watoto wake huruma ili kutambua yale waliyotenda katika maisha; anamwomba matumaini ili yaweze kuwasindikiza wakati huu wanapoyaanza mapambazuko ya Mwaka Mpya. Mwaka uliopita umesheheni matukio ya furaha na uchungu pamoja na kutambua uwepo endelevu wa Mungu anayewajalia nguvu ya kufanya yote mapya pamoja na kuwategemeza kwa njia ya msaada wake.

Imekuwa ni fursa ya kutafakari ikiwa kama kweli matukio mbali mbali yaliyojiri katika kipindi cha mwaka uliopita yalikwenda kadiri ya mapenzi ya Mungu au wametoa kipaumbele cha pekee kwa miradi ya kibinadamu ambayo mara nyingi inajikita katika mafao binafsi kwa kumezwa na uchu wa madaraka ambao umekuwa pia ni chanzo cha maafa makubwa katika maisha ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake mwishoni mwa mwaka 2015 anapenda kukazia kwa namna ya pekee upendo wa huruma ya Mungu. Kuna matukio ya vita, maafa, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia; wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao; watoto na wanawake wasiokuwa na makazi maalum, chakula wala msaada.

Lakini kwa upande mwingine, Kanisa limeshuhudia matendo ya wema, upendo na mshikamano yaliyosheheni kwa namna ya pekee katika mwaka 2015. Bahati mbaya matendo kama haya si sehemu ya habari zenye mvuto na mashiko kwa vyombo vya habari! Ni matukio ambayo yanamezwa kwa ubaya, lakini ikumbukwe kwamba, wema daima utashinda ubaya, ingawa wakati mwingine wema unaweza kuonekana kana kwamba ni dhaifu na wala hauna nguvu.

Baba Mtakatifu Francisko amegusia matukio mbali mbali ya kiulimwengu ambayo yamelitikisa hata Jiji la Roma. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi Jijini Roma, wanaalikwa kwa namna ya pekee kusonga mbele kwa matumaini kwa kuvuka mwelekeo wa sasa, ili kuweza kukumbatia tunu msingi za maisha ya binadamu zinazojikita katika huduma, uaminifu na mshikamano utakaowawezesha kuvuka wasi wasi na mashaka ambayo yametawala kwa kiasi kikubwa matukio mbali mbali katika kipindi cha mwaka uliopita.

Hizi ni dalili za kutokuwa makini kwa ajili ya mafao ya wengi. Wakristo wanahamasishwa kutoa ushuhuda makini katika ustawi na ujenzi wa Jiji la Roma kwa kuzingatia historia na kwa maombezi ya Bikira Maria afya ya Warumi, awasaidie kweli kuwa ni mashuhuda wa imani, ukarimu, udugu na amani. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya matumaini ya waamini na kwamba, hakuna atakaye changanyikiwa daima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.