2016-01-01 14:30:00

Rais Magufuli awaapisha Makatibu wakuu na Manaibu wao; wote wala kiapo


Makatibu wakuu na Makatibu wakuu wasaidizi walioteuliwa na Rais John Pombe mwishoni mwa Mwezi Desemba 2015, wameapishwa na Rais Magufuli tarehe Mosi Januri 2016 kwenye viwanja vya Ikulu, Jijini Dar es Salaam pamoja na kutia sahihi hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma. Balozi Ombeni Sefu anaendelea kuwa ni Katibu mkuu kiongozi na Bwana Peter Ilomo anakuwa ni katibu mkuu Ikulu.

Wakati huo huo Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewapongeza Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Wakuu, mara baada ya kuapishwa kwao. Amewataka kuwa ni waaminifu, waadilifu na wachapa kazi mahiri pamoja na kuwajibika mbele ya wananchi kwa kuwapatia taarifa muhimu. Ametoa pongezi hizo wakati Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Wakuu wakiwa wametia saini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma mbele ya waandishi wa habari.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewataka viongozi hao, kuwa waaminifu, kuwajibika na kutoa taarifa ya utendaji kwa wananchi. Aidha, alisema kuwa, viongozi wengine watakao apa mbele ya Kamishna wa Tume ya Maadili ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, ikiwa ni hatua ya Serikali kudhibiti na kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha. “Wakuu wa Wilaya watahakikisha fedha zilizoenda katika Halmashauri zao lazima zitumike katika shughuli zilizokusudiwa” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa watanzania kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kuwa itatimiza ahadi zote ambazo Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais walizitoa wakati wa Kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Wakuu hao, wameapishwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, ambapo shughuli hiyo ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Mke wa Mheshimiwa Rais Mama Janeth Magufuli pamoja na viongozi mbalimbali.

Na mwandishi maalum.

Ikulu Dar Es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.