2016-01-01 14:12:00

Papa awapongeza wote wanaojikita katika kutafuta na kudumisha amani!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarhe Mosi Januari, amemshukuru Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa salam na matashi mema kwa mwaka 2016 alizozitoa kwake wakati alipokuwa analihutubia taifa kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari. Baba Mtakatifu anamshukuru kwa moyo wa dhati.

Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wadau mbali mbali ambao wamesaidia kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani kwa njia ya maandamano huko Jimboni Molfetta, Italia. Anawapongeza vijana walioamua kuadhimisha mkesha wa Mwaka Mpya kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani.

Baba Mtakatifu anaipongeza pia Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambayo imeandaa maandamano ya amani sehemu mbali mbali za dunia na kuwataka kuendeleza dhamana hii ili kukoleza mchakato wa upatanisho na maridhiano. Anawashukuru wale wote waliokesha kwa ajili ya kuombea amani duniani; umoja na mapatano ndani ya familia za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa mikakati yote hii pamoja na sala zao.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbuka watoto waimbaji wanaongozwa na nyota “Sternsinger” kutoka Ujerumani na Austria wanaopeleka baraka ya Yesu nyumba kwa nyumba. Kwa waamini na wote wenye mapenzi mema, Baba Mtakatifu amewatakia heri, amani na huruma ya Mungu katika kipindi cha mwaka wa 2016, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.