2016-01-01 14:01:00

Onesheni furaha mnapokutana na Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe Mosi, Januari 2016 amewatakia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema matashi mema kwa mwaka 2016, wakiwa na matumaini kwani si yote yataweza kubadilika kwa kuanza mwaka mpya. Liturujia ya Neno la Mungu katika Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu inajikita katika matumaini na baraka inayomiminika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya wema wote.

Bwana awabariki na kuwalinda, awaangazie nuru ya uso wake na kuwafadhili; Bwana awainulie uso wake na kuwapatia amani. Hii ni Sala ambayo Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale aliitumia kwa ajili ya kutoa baraka kwa watu wake. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, amewatakia baraka hizi waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili waweze kuwa na furaha wanapokutana na Sura ya huruma ya Mungu katika maisha yao ya kila siku. Wawe tayari kuutafuta Uso wa Mungu ili kupyaisha maisha yao, kwani Mungu anampenda binadamu.

Mwenyezi Mungu anawataka waamini kufanya mabadiliko kutoka katika undani wa maisha yao kwa kuambata uvumilivu na upole, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuingia katika maisha ya waamini wake kama mvua ili aweze kuwakirimia matunda anayokusudia. Lakini anawasubiri na kuwaangalia kwa jicho la huruma na mapendo. Kila siku wanapoamka wawe na ujasiri wa kusema, “Bwana uniangazie nuru ya uso wako.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, tarehe Mosi, Januari 2016 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Shinda kutojali, ambata amani”. Mwenyezi Mungu anapenda kupandikiza mbegu ya amani sehemu mbali mbali za dunia, itakayotunzwa na kuendelezwa na binadamu, changamoto ya kuendeleza mapambano ya maisha ya kiroho ili kumshinda adui wa amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, adui wa amani si tu vita bali pia hali ya kutojali inayowafanya watu kukumbatia ubinafsi kiasi cha kujifungia katika undani wao kwa kuweka vizingiti pamoja na kuwa na woga usiokuwa na mashiko. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuzingatia ukweli wa mambo kwa kutambua mahitaji ya ndugu zao katika Kristo. Wanaweza kuanza kufungua mioyo yao na kuwajali jirani na wahitaji zaidi. Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kuambata amani.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu aliyebahatika kuyaweka yote na kuyatafakari kutoka katika undani wa moyo wake. Hii ni furaha ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Aliweka moyoni mwake umaskini na unyonge wa Mtoto, mzaliwa wake wa kwanza katika Hori la kulishia wanyama kwani walikosa hifadhi kwenye nyumba za wageni na wala hakuwa na uhakika wa maisha ya Mtoto Yesu kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini, wasi wasi, moyo wa shukrani pamoja na matatizo na yote yaliyokuwa yanajiri katika maisha yao, yalihifadhiwa moyoni mwa Bikira Maria, yakawa ni chemchemi ya sala na majadiliano ya kina na Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutunza ndani mwao furaha na machungu katika maisha yao ya kila siku, huku wakiendelea kuambatana na Yesu. Baba Mtakatifu anaendelea kuombea amani na huruma ya Mungu katika maisha ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.