2016-01-01 10:30:00

Iweni wajenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, udugu, amani na utulivu!


Baba Mtakatifu Francisko ameuanza Mwaka 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na Siku ya 49 ya kuombea amani duniani ambayo kwa mwaka 2016 inaongozwa na kauli mbiu “Sinda kutojali, ambata amani”. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawataka waamini daima kuanza na Mwenyezi Mungu, kuwa na mang’amuzi ya historia pamoja na kuambata bahari ya huruma ya Mungu katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utimilifu wa nyakati ulipowadia Yesu Kristo alizaliwa. Hiki ni kipindi cha historia kinachoshuhudiwa na tawala zenye nguvu kama vile Ufalme wa Warumi; vita pamoja na ukosefu wa uhuru; mambo ambayo yaliacha ukakasi katika maisha ya watu wa nyakati zile. Kumbe, mwelekeo wa kijiografia si sifa inayopambanua utimilifu wa nyakati, bali utimilifu huu unapaswa kuangaliwa kwa kuanzia na Mwenyezi Mungu, anayeamua kutimiza ahadi zake na kwamba, si historia iliyoamua kuzaliwa kwa Kristo Yesu.

Ujio wa Kristo ulimwenguni umeiwezesha historia kufikia utimilifu wake. Kwa kuzaliwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, huu unakuwa ni mwanzo mpya unaotekeleza ahadi zilizotolewa na Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale. Mwenyezi Mungu ambaye alinena zamani kwa njia ya Mababu wa imani na Manabii, lakini nyakati hizi za mwisho amezungumza na watu wake kwa njia Mwanaye wa pekee, aliyemweka kuwa mrithi wa mambo yote na tena kwake Yeye aliuumba ulimwengu. Yeye ni mng’ao wa utukufu wa Baba na chapa ya Nafsi yake anayevichukua vyote kwa amri ya uweza wake.

Baba Mtakatifu anasema, kumbe, utimilifu wa nyakati ni uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee katika historia ya mwanadamu. Kwa jinsi hii, waamini wanaweza kuuona utukufu wa Mungu uking’ara katika umaskini unaojionesha kwenye Pango la kulishia wanyama, kwa uwepo wa Neno wa Mungu aliyefanyika “mdogo” akawa mtoto na kwa njia yake, nyakati zinapata utimilifu wake.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kwa bahati mbaya Fumbo hili linakumbana na kinzani katika mang’amuzi ya historia. Kila siku ya maisha badala ya watu kuonja alama za uwepo wa Mungu kati yao wanashuhudia alama hasi zinazowapelekea watu kudhani na kufikiri kwamba, Mungu hayupo pamoja nao! Utimilifu wa nyakati unakinzana na uwepo wa matukio mengi ya ukosefu wa haki yanayoendelea kuujaza ulimwengu.

Bado kuna jeuri na kiburi kinachowatala wanyonge; chuki na uhasama; mambo yanayosababisha mateso makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia; wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, njaa, dhuluma na ukosefu wa haki msingi. Bado kuna umaskini mkubwa unaowapelekea watu wengi pia kutenda dhambi; mambo yote haya yanakinzana  na utimilifu wa nyakati uliotekelezwa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwa Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu anaendelea kukaza akisema, pamoja na mambo yote haya, lakini bado bahari ya huruma ya Mungu inaendelea kufurika duniani, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuzama katika bahari hii, ili kupyaisha maisha yao, ili kushinda kutojali kunakokwamisha mchakato wa mshikamano; hali ya kukosa msimamo katika maisha, tayari kutoka kimasomaso kushirikishana na wengine. Neema ya Kristo Yesu inayotekeleza matumaini ya wokovu inawasukuma waamini kuwa ni washiriki wa ujenzi wa misingi ya dunia inayosimikwa katika haki, udugu, amani na utulivu mintarafu mpango wa Mungu katika kazi ya Uumbaji.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanzo mwa Mwaka Mpya, Kanisa linafanya tafakari juu ya Umama wa Bikira Maria, kielelezo cha amani ambaye ahadi za kale zinapata utimilifu wake kwa Mama huyu! Aliamini maneno ya Malaika, akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kwa njia hii akawa ni Mama wa Yesu. Na kwa njia ya kukubali kwake, nyakati zimefikia utimilifu wake. Naye Bikira Maria akayaweka yote haya na kuyatafakari moyoni mwake. Bikira Maria ni chombo cha kumbu kumbu endelevu ya Yesu na Kikao cha Hekima ambamo waamini wanaweza kujichotea ujuzi na maarifa ya kufafanua mafundisho ya Yesu.

Bikira Maria anawawezesha waamini kufahamu maana ya matukio mbali mbali katika maisha, matukio yanayowagusa kama watu binafsi, familia, nchi na ulimwengu katika ujumla wake. Pale ambapo ufahamu wa wanafalsafa unashindwa kufika au muafaka wa makubaliano ya wanasiasa unaposhindikana; hapo imani inayobeba neema ya Injili ya Kristo inafika kuwawezesha watu kuwa na mang’amuzi na mielekeo mipya.

Bikira Maria amebarikiwa kwani ameukirimia ulimwengu Mwana wa Mungu na kumwamini. Ni Mama mwenye imani aliyembeba Mwana wa Baba wa milele moyoni mwake, hata kabla ya kutungwa mimba tumboni mwake, ili kuweza kuwa kweli ni Mama wa waamini wote. Baba Mtakatifu mwishoni, anamwomba Bikira Maria awaombee neema na baraka katika maadhimisho ya Siku hii maalum iliyotengwa kwa ajili yake sanjari na kuwaonesha Uso wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo anayewakirimia walimwengu huruma na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.