2015-12-31 14:50:00

Pueri Cantores wamkuna Papa mstaafu Benedikto XVI kwa nyimbo za Noeli


Kikundi cha vijana waimbaji, maarufu kama “Pueri Cantores” kinaadhimisha kongamano la arobaini la kimataifa mjini hapa mjini Roma. Hiki ni chama cha kitume kinachowaunganisha vijana na wazazi wao kwa njia ya muziki ili kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana wenzao huruma ya Mungu inayojikita katika muziki mtakatifu kwa kutambua kwamba, mtu anayeimba vizuri, huyo anasali mara mbili kama anavyokaza kusema Mtakatifu Augostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa.

Vijana hawa ni wajumbe wa haki na amani na wana umri kati ya miaka mitano hadi miaka ishirini. Ni watoto wanaotoka sehemu mbali mbali za dunia, kila kijana anayo sababu ya msingi iliyomsukuma kujiunga na chama hiki cha kitume. Wengi wao, wanapenda kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kubadilishana mawazo na kujenga umoja na mshikamano wa kimataifa. Vijana wengine wanajisikia furaha wanaposhiriki kuimba na vijana wenzao na kwamba, huu ni utajiri mkubwa katika maisha yao ya kiroho, kiutu na kimatamaduni, cheche za matumaini mapya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Vijana hawa wanataka kujenga na kudumisha umoja na mshikamano dhidi ya vita, chuki na uhasama mambo yanayoendelea kuwagawa walimwengu wakati mwingine kwa misingi ya udini, ukabila na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko! Wazazi kwa upendo wao, wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kugundua vipaji vya watoto wao, ili kuwasaidia kuvikuza kwa ajili ya utukufu wa Mungu na ustawi wa binadamu katika maisha ya kiroho.

Hii ni nafasi ya kujifunza kutoka katika tamaduni za watu wengine na hivyo kujitajirisha, ili kutumia uzoefu huu kwa mambo makubwa zaidi. Furaha ya wazazi inashuhudiwa pia katika furaha ya watoto wao kuwaona wakishiriki kuimba nyimbo za mataifa na makabila mbli mbali ya dunia, inafurahisha moyo!

Wazazi kwa upande wao wanasema, kuna sadaka katika kuwasaidia watoto hawa kutekeleza azma yao, lakini faida ni kubwa zaidi kuwaona watoto hawa wanakuwa ni mashuhuda wa amani, huruma na upendo wa Mungu hususan wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Sadaka na majitoleo haya yanapata faraja ya pekee walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 31 Desemba 2015. Vijana wakamtwanga Baba Mtakatifu Francisko maswali mbali mbali, kwa upole na unyenyekevu, akawajibu na kukata kiu ya udadisi wao wa ndani!

Wajumbe wa mkutano wa Pueri Cantores kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walifurahi kuimba mbele ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, ambaye anapenda sana muziki. Hii ilikuwa ni kwaya ya Vijana 36 kutoka Ujerumaini waliojimwaga kwenye Bustani za Vatican kumwimbia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI nyimbo za Noeli kwa lugha ya Kijerumani. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Vijana wameonesha nyuso za furaha na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akawashukuru na kuwapatia salam na matashi mema kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.