2015-12-31 07:52:00

Mshikamano wa upendo na sala kwa waathirika wa majanga asilia!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumatano tarehe 30 Desemba 2015, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati na wale wote waliokumbwa na majanga asilia kwa siku za hivi karibuni huko: Marekani, Uingereza, Amerika ya Kusini, hususan Paraguay; na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Baba Mtakatifu anawaombea wote walioguswa na kutikiswa na  maafa haya faraja na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kupata mahitaji yao msingi.

Nchini Marekani, taarifa zinazonesha kwamba, kuna mafuriko makubwa yanayoendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa makazi ya watu pamoja na miundo mbinu. Miji iliyoathirika vibaya ni Missour, St. Louis, Texas, New Mexico, Alabama, Mississippi na Georgia. Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza kuwa mji wa Oklahoma uko katika hali ya hatari kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha huko usiku na mchana.

Amerika ya Kusini, imekumbwa na mvua za El Nino na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao huko Uruguay, Argentina na Brazil. Taarifa zinaonesha kwamba, Paraguay ni kati ya nchi za Amerika ya Kusini ambazo zimeathirika zaidi kutokana na mafuriko yanayoendelea katika ukanda huu. Watu wanaendelea kupoteza maisha na mali zao pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi maalum.

Habari zaidi zinaendelea kusema kwamba, Uingereza katika siku za hivi karibuni imekumbwa na mafuriko makubwa kiasi cha kuleta uharibifu mkubwa kwa makazi ya watu pamoja na miundo mbinu ya barabara. Zaidi ya familia 5500 hazina huduma ya umeme majumbani. Wataalam wa masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa wanasema zote hizi ni athari za mabadiliko ya tabianchi. Mwaka 2015 umekuwa ni mwaka ambao umekumbwa na majanga asili ana hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si anaitaka jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake, vinapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.